LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 17, 2020

WANANCHI MAGU WAMSHUKURU RAIS MAGUFULI KWA KUWAJENGEA MRADI WA MAJI WA SH. MILIONI 397.9

Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akijiridhisha na huduma ya maji kwenye mradi wa Matela, Wilayani Magu wakati wa ziara yake ya kukagua ufanisi wa mradi. Wanaoshuhudia ni wananchi wa Kijiji cha Matela.

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Magu, Mhandisi Anna Mbawala (katikati) akiwasilisha taarifa ya mradi wa Matela kwa Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (hayupo pichani). Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli na kulia ni Meneja RUWASA Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Immaculata Raphael.

Na Mohamed Saif, Magu

Wananchi wa Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza wamemshukuru Rais Dk. John Magufuli kwa kuwaondolea kero ya muda mrefu ya ukosefu wa huduma ya maji safi na salama kufuatia  kujengwa wilayani humo mradi wa maji safi ambao umetekelezwa kupitia Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Maji (WSDP) kwa gharama ya sh. milioni 397.9.


Shukrani hizo zimetolewa wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ya kukagua mradi wa maji wa Matela katika kijiji cha Matela wilayani humo, kwa lengo la kukagua miradi ya maji ambayo wakandarsi wake wamechelewa kuikamilisha kwa wakati kama inavyoelekeza mikataba yao.


Alibainisha kuwa Matela ni miongoni mwa miradi ulioisumbua Wizara ya Maji kwani ujenzi wake ulichukua muda mrefu na hivyo kuwacheleweshea wananchi kupata huduma ya maji kinyume na azma ya Rais Dk. John Magufuli.


“Tangu anaingia madarakani, Rais Magufuli aliazimia kuwaondolea kero ya maji wananchi wake, kuna baadhi ya miradi inakwamisha azma hiyo kufikiwa kwa wakati ukiwemo huu wa Matela ambao hata hivyo nafarijika kuona sasa nao umekamilika,” alisema Aweso.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya Naibu Waziri Aweso, wananchi wa Matela walisema licha ya kwamba mradi huo umechelewa kukamilika kwa wakati lakini umeleta faraja katika maisha yao.


Naomi Mbotela, Mkazi wa kijiji cha Matela alimshukuru Rais Magufuli kwa kuwapatia mradi huo ambao alisema umewaondolea kero ya kutembea umbali mrefu na kutumia muda mwingi kufuata huduma ya maji.


“Kwa sasa hatuna shaka kwenye suala la maji, zamani sisi wanawake tuliteseka sana, tulikua tunatoka Saa 11 alfajiri na kutembea umbali mrefu kufuata maji na hii wakati mwingine ilitusababishia migogoro kwenye ndoa zetu,” alisema Mbotela.


Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Matela, Elias Njita alisema uwepo wa mradi huo ni uthibitisho kuwa Rais. Dkt Magufuli ni Rais wa wanyonge.


“Tunamshukuru sana Rais kutuona na kutujali sisi wanyonge huku vijijini, ametoa fedha nyingi kutujengea huu mradi ili sisi wanyonge tupate maji,” alisema Njita.


Aliahidi kuendelea kumuunga mkono Rais Magufuli hasa ikizingatiwa kwamba kwa muda mrefu wananchi wa maeneo ya  vijijini wamekuwa wakisahaulika.


“Tunaahidi sisi tutamuunga mkono Rais, tunaahidi hatutomuangusha kazi anayofanya ni kubwa na ni ngumu sisi wanyonge tulikua tumesahaulika lakini yeye anatujali ili na sisi tuweze kujikwamua kimaendeleo,” aliongeza Njita.


Aidha, kwa mujibu wa msimamizi wa mradi Meneja wa Wakala ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Wilayani Magu, Mhandisi Anna Mbawala ni kwamba ulianza kutekelezwa na Mkandarasi M/S STC Construction Company Ltd Mwaka 2017 na ulipaswa kukamilika 2019 na kuwa umetekelezwa kupitia Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Maji (WSDP) kwa gharama ya shilingi milioni 397.9.


Alibainisha kwamba ulianza kutoa maji rasmi tarehe 02 Agosti, 2020 na kuwa umekabidhiwa kwa Jumuiya ya watumiaji maji ya Nyanguge-Muda kwa ajili ya kuhudumia wakazi wapatao 5,000 wa Kijiji cha Matela na vitongoji vyake.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages