Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya NMB imemtangaza Ruth Zaipuna
kuwa Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Benki hiyo uteuzi ulioanza jana Agost
18,2020.
Mwenyekiti wa Bodi ya NMB – Dk. Edwin Mhede alimtangaza Zaipuna
huku akikiri kuwa mchakato wa kumpata haukuwa mwepesi lakini hakukuwa na
upendeleo isipokuwa walitazama wasifu, utendaji na maslahi ya Benki na
Tanzania.
Dk. Mhede alisema katika kipindi kirefu Benki hiyo ilikosa mtu
baada ya aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wake kuondoka na hivyo walibaki na mtu
aliyekuwa anakaimu kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu lakini takwa la kisheria
lilikuwa linawabana kuwa ni lazima wapate mtu.
Zaipuna anakuwa Mtanzania wa kwanza kushika nafasi hiyo tangu Benki
hiyo ilipobinafsishwa ambapo kwa nyakati zote nafasi za juu zilishikwa na
wageni wakiwemo Ineke Bussemaker aliyekuwa Mkurugenzi tangu 2014 – 2018 kisha
nafasi hiyo ikachukuliwa na Albert Jonkergow ambaye alishikiria kwa kipindi cha
mpito cha miezi sita kabla ya Zaipuna kupewa nafasi ya kukaimu.
Mwenyekiti alisema mchakato wa kumpata Mtendaji Mkuu ulikamilika
Juni 30,2020 na jana ilikuwa ni siku ya kumtangaza huku akibainisha kuwa sifa
zote zilizotakiwa katika nafasi hiyo, walijiridhisha kuwa Zaipuna anazo hivyo
hakuna shaka kuhusu utumishi wake katika nafasi hiyo.
‘’Katika kipindi chote tulihangaika kumpata mtu mwenye kufikia
vigezo vinavyotakiwa, lakini wakati mwanamama huyu alipokuwa anakaimu, Benki
imeendelea kufanya vizuri zaidi na kukuza mtaji wake, hakuna mahali paliyumba
chini ya usimamizi wake,hivi kwa hali hiyo mnadhani tungefanyaje,’’alisema Dk.
Mhede.
Alitaja mafanikio makubwa katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu
wa kukaimu kwa Afisa huyo ni faida kubwa ambayo benki imekuwa ikipata ikiwemo
Sh.93 bilioni zilizopatikana katika kipindi cha nusu ya kwanza ya 2020 huku mahusiano
yakizidi kuimarika kati ya benki na Serikali pamoja na wateja wake.
Hata hivyo alimuagiza mtendaji huyo kuhakikisha benki inaendelea
kuwa imara na yenye kutoa matumaini kwa wananchi wake huku akisisitiza
ushirikiano wa timu moja kati ya kiongozi huyo na watumishi wengine ndani ya
taasisi yao.
Akizungumza mara baada ya kupokea uteuzi huyo, Zaipuna alisema
ni uteuzi wa ushindi kwa NMB wala siyo yeye lakini akaahidi kwamba atakuwa
mtumishi kama ilivyo kwa watumishi wengine kwani anaamini kila mmoja anamchango
wake kwa nafasi yake hivyo akaomba wenzake kujitoa zaidi katika kuwahudumia
Watanzania.
Zaipuna alitaja vipaumbele vitano atakavyo anza navyo ikiwemo
NMB kuendelea kukua kila mwaka na kuwa Benki namba moja nchini,Benki kuendelea
kuwa chaguo la wateja, kuongeza na kuimarisha mashirikiano kwa wateja na
watumishi na kipaumbele cha tano ni kuendelea kuboresha maslahi kwa watumishi
ili vijana wa Kitanzania wavutiwe na kutamani zaidi waajiriwe NMB.
Alisema hayo yote yatawezekana ikiwa kila mtumishi atakuwa na
nidhamu ya utekelezaji na kujituma katika ubunifu wa ushirikishwaji wa mipango
lakini kwa upande wake akasema ataendeleza kasi iliyopo ili misingi iliyojengwa
isiyumbe.
Kuhusu wanahisa aliitaja Serikali ya Tanzania na wabia wa benki
ya Rabo ya Uholanzi kwamba waondoe hofu kuhusu NMB kwani ni chombo
kilichosimama kwa ajili ya kutoa matumaini kwa watu hivyo wataendeleza kasi
hiyo wakati wote.
Awali Mjumbe wa Bodi Margaret Ikongo aliwataka wajumbe kutoa
ushirikiano mkubwa kwa CE0 wao mpya kwa kuwa kazi anayokwenda kuifanya ni kubwa
na ndiye mbeba maono wa chombo hicho hivyo ushindi wake utategemea nguvu ya
pamoja na watumishi ikiwemo kumuombea.
Bi.Ikongo alimtaka Zaipuna kufanya kazi kwa kuwashirikisha zaidi
watumishi wenzake na atambue kuwa kila mmoja ana mchango mkubwa kwa sehemu yake
lakini akaomba watumishi kumuombea kiongozi huyo katika cheo hicho kipya
alichokabidhiwa.

No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇