LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 2, 2020

RAIS DK. MAGUFULI APOKEA HATI ZA UTAMBULISHO ZA BALOZI WA MAREKANI NA WA VIETNAM, LEO

Rais wa Dk. John Magufuli akiwa na Balozi wa Marekani hapa nchini Donald John Wright Ikulu jijini Dar es Salaam, alipowasili kuwasilisha hati zake za Utambulisho, leo. Kulia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi.

Ikulu Dar es Salaam

Rais Dk. John Magufuli leo amepokea Hati za Utambulisho za Mabalozi wawili walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa Tanzania na kuwaomba Mabalozi hao kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchini mwao kuja kuwekeza hapa nchini na kwamba Serikali itakuwa tayari wakati wowote kutoa ushirikiano kwao.


Waliowasilisha hati hizo Ikulu Jijini Dar es Salaam ni Dk. Donald John Wright aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Marekani hapa nchini na Nguyen Nam Tien, aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Vietnam hapa nchini.

Katika mazungumzo baada ya kupokea hati hizo, Rais Magufuli amewakaribisha Mabalozi hao hapa nchini na ameeleza kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati yake na nchi hizo.

Akizungumza baada ya kuwasilisha hati zake za utambulisho, Balozi Wright ameeleza kufurahishwa kwake na kurejea Tanzania baada ya miaka 33 tangu alipokuja kwa mara ya kwanza kufanya kazi za kutoa matibabu, na kwamba tangu wakati huo anawaheshimu na kuwapenda Watanzania kutokana na ukarimu wao, upendo wao na jinsi wanavyoishi na wageni kama wanafamilia wao.
 
Balozi Wright amesema Marekani inaiona Tanzania ni nchi imara, tulivu na yenye demokrasia, na kwamba uhusiano wake mzuri na Marekani umeiwezesha kufanya kazi pamoja na anatarajia kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano zaidi na Serikali ya Tanzania.

Pia, Balozi Wright amewasilisha salamu za rambirambi kwa Rais Magufuli kutoka kwa Rais wa Marekani Donald Trump na Serikali ya Marekani kufuatia kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamin William Mkapa na kueleza kuwa Marekani inatambua mchango mkubwa wa Hayati Mkapa kwa Tanzania na Kimataifa.

Nae Mhe. Nguyen Nam Tien amesema Tanzania ni nchi nzuri, Rais wake anafanya kazi nzuri na kwamba anatazamia kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu zaidi ili kukuza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano uliopo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi ameelezea uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Marekani na kwamba Marekani imekuwa ikifadhili miradi mingi akiwemo afya  ambapo imetoa Shilingi Trilioni 1.56 mwaka 2018, miradi 3,179 ya uwekezaji kutoka Marekani ambayo imezalisha ajira 550,000 kwa Watanzania, na pia mauzo ya bidhaa za Tanzania nchini Marekani yamekuwa yakiongezeka ambapo mwaka 2019 bidhaa zenye thamani ya shilingi Bilioni 119 ziliuzwa nchini Marekani.

“Kwa hiyo uhusiano wa Tanzania na Marekani ni mzuri na unazidi kuimarika na tunaamini kuwa kuja kwa Mhe. Balozi Donald John Wright kutaimarisha zaidi uhusiano huo” amesema Prof. Kabudi.

Kwa upande wa Vietnam, Prof, Kabudi amesema Tanzania imekuwa na uhusiano wa kidugu na kihistoria na nchi hiyo ambapo inashirikiana nayo katika mambo mengi ikiwemo uwekezaji wa kampuni ya simu za mkononi ya Halotel.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages