NADIRIKI kusema kwaheri Mzee wa Uwazi na Ukweli, Benjamini William
Mkapa umeondoka Tanzania bila kutuaga, tutakukumbuka daima hasa kwa mambo
makubwa ulioyoifanyia nchi yetu kabla ya
kuwa rais, ukiwa rais na baada ya kustaafu urais.
Pia, nasikitika umeondoka duniani bila kutuaga
watanzania na hasa viongozi wenzako wastaafu akina Jakaya Kikwete, Ali Hassan
Mwinyi na waliopo madarakani , Rais John
Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
pamoja na familia yako.
Kabla ya kuondoka duniani, Mzee wa Uwazi na
Ukweli ulitupa matumaini ulipohudhuria Mkutano Mkuu wa 10 wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Julai 11,2020, kwenye Ukumbi wa
Jakaya Kikwete jijini Dodoma, ambapo hakuna aliyewaza kuwa utaaga dunia siku 12
baadaye.
Siku hiyo nikiwa miongoni mwa wanahabari
walioteuliwa kuingia ndani ya ukumbi wa Kikwete, kuripoti habari za mkutano huo
wa ngazi ya juu wa CCM kitaifa, nilifurahi kukuona wewe na viongozi wastaafu
wenzio pale meza kuu, Jakaya Kikwete na Ali Hassan Mwinyi mkiwa na nyuso za
bashasha huku mkiangua vicheko baada ya kuchekeshwa na vionjo vya hotuba ya
Rais Magufuli.
Kweli nilifarijika sana kuwaona, huku nikiwaza
kwamba laiti angekuwepo Rais wa Awamu ya Kwanza, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere, safu ya marais wanne wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ingekamilika, lakini yote tunamwachia Mwenyezi Mungu kwani ndiye
anayeamua nani atangulie na nani wa kufuata.
Kwa hali niliyoiona ilidhihirisha wazi kwamba mna
ushirikiano, umoja, mashikamano na upendo, pia mmebeba dhamana kubwa ya
kuhakikisha Taifa linaendelea kuwa la amani na utulivu kwa kupokezana madaraka
kwa amani ili nchi yetu iendelee kuongozwa na viongozi mahiri, wazalendo kama
ilivyo kwa kiongozi wetu wa sasa Rais John Magufuli.
Mkapa tutazimisi picha za pamoja tulizozizoea
kuziona mkipiga na pacha wastaafu wenzako, Kikwete na Mwinyi pamoja na Rais
Magufuli huku mkiwa mmeshikana mikono huku mkiwa na tabasamu usoni, kama
mlivyopiga katika matukio ya hivi karibuni, Mliposhiriki ujenzi wa Ikulu ya
Chamwino, wakati wa kuvunjwa Bunge la Jamhuri ya Muungano na mlipokaa kwa mara
ya mwisho meza kuu mlipohudhuria Mkutano Mkuu wa CCM jijini Dodoma, Julai 11,
mwaka huu.
Picha hizo zilikuwa zinatupa faraja kubwa sana
watanzania, lakini pia picha hizo
zilizokuwa zinasambaa kwa kasi duniani kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii,
kilikuwa ni kisu kwa wasioitakia mema nchi yetu kwa umoja na mshikamano tuliokuwa nao.
Baadhi ya wananchi wa
mataifa mengine kitendo hicho kilikuwa kinawafanya waitamani na kuionea wivu
Tanzania, kwani katika nchi zao hakuna tunu kama hiyo.
Samahani kama nitakosea, lakini mimi sijawahi ona
picha kama hizo katika nchi zinazotuzunguka kama vile; Kenya, Uganda, Rwanda,
Burundi, Sudani kusini, DRC Congo, Congo Brazaville, Msumbiji, Zambia, Malawi,
Zimbabwe, Madagascar, Comoro, Angola na hata Afrika Kusini. Hiyo inadhihirisha
jinsi Nchi Yetu ilivyobarikiwa.
Lakini wakati tungali tunahitaji baraka zako,
Mzee wa Uwazi na Ukweli, umeondoka na
kutuachia pengo lingine, ukiwaacha bila
kuwaaga mapacha zako wastaafu, Jakaya Kikwete na Ali Hassan Mwinyi ili jahazi
waliongoze wenyewe. Je, ulikumbuka kuwaachia usia wowote?
Mkapa, au ndiyo ulifanya ujanja wa kuacha wosia
kwa watanzania wote na walimwengu kupitia kitabu chako ambacho kimesheheni
mambo mengi muhimu kwa Taifa letu, Afrika
na Dunia kwa ujumla? Sasa kitabu hicho itabidi tukitafute kwa udi na
uvumba tuusome wosia uliotuachia.
Nadiriki pia kusema kuwa kwa mtindo ulioondokea
Mzee wa Uwazi na Ukweli, Mkapa ni sawa na kwamba 'umewapiga chenga ya mwili' na
kuwaacha hoi wasiamini kilichotokea,
wastaafu wenzako, Mzee wa Nguvu Mpya, Ari Mpya na Kasi Mpya, Jakaya Kikwete na
Mzee wa ruksa, Ali Hassan Mwinyi lakini
pia Rais aliye madarakani, Mzee wa Hapa Kazi Tu, John Magufuli.
Naamini siku hiyo ya mkutano kama ilivyokuwa
kwangu, wengi walifarijika kuwaona lakini vile vile baadhi yetu pamoja na
watanzania wengine waliokuwa wanaangalia tukio hilo kwenye luninga, ilikuwa ni
siku ya mwisho kukuona ukiwa hai hadi Julai 24, aliposikika Mkuu wa Nchi, Rais
Magufuli akiutangazia Umma kwamba hatuko na wewe tena.
Mkapa, mbona kama 'unalipiza kisasi'
ulichofanyiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye alifariki 1999,
mwaka mmoja kabla ya kushuhudia kuapishwa kwako mwaka 2000 kushika kipindi cha
pili cha uongozi wako?
Kama siyo hivyo, kwa nini basi hukusubiri John
Magufuli aapishwe mwaka huu, bali umeamua kuondoka miezi michache kabla ya
tukio hilo muhimu? au lengo lako lilikuwa ni kushuhudia tu jina lake lipitishwe
katika mkutano mkuu wa CCM?
Sasa unapoondoka, bila kuaga, Je, jukumu la
kuendelea kuilea Tanzania yenye amani na utulivu kwa nini umelikimbia na
kuwaachia Mwinyi, Kikwete na Magufuli? Nadiriki kusema umeamua 'kulipiza
kisasi' alichokufanyia Baba wa Taifa.
Mkapa umewaachia machungu marais wastaafu wenzako
na hasa Magufuli aliye madarakani ambaye
umemlea kisiasa na kiuongozi kiasi cha kumuita askari wa mwamvuli namba moja
katika Baraza lako la Mawaziri.
Rais Mkapa enzi za uhai wake akimnadi, John Magufuli alipogombea kwa mara ya kwanza ubunge mwaka 1995 wakati wa kampeni za urais ambapo yeye aligombea kwa mara kwanza kupitia CCM. |
Kwa kukumbuka mambo mengi uliyomfanyia, ndiyo
maana Rais Magufuli alishindwa kujizuia na kuanza kububujikwa na machozi mbele
ya kadamnasi ya waombolezaji wa kitaifa na kimataifa pamoja na wananchi
alipokuwa akitoa neno la kukuaga katika shughuli za kutoa heshima za mwisho
kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam Julai 28, 2020.
Magufuli alikuwa bado anahitaji msaada wako wa
ushauri wa kila hali wa kibinafsi na
kiuongozi, lakini sasa mzigo huo umeamua kuwaachia pacha wastaafu wenzako,
Kikwete na Mwinyi, na kwa hali ilivyo kutokana na uzee alionao Mzee wa Ruksa,
Mwinyi.
Lakini, pasi na shaka jukumu hilo kubwa umemuachia Kikwete ambaye bado anaonekana ana nguvu za kuweza kukimbia huku na kule kumsaidia Rais Magufuli kuishauri na kumwakilisha kuongeza hadhi na heshima ya Tanzania katika baadhi ya matukio makubwa duniani kama ilivyotokea hivi karibuni katika shughuli ya kuapishwa Rais mpya wa Burundi na mazishi ya Rais wa zamani wa Burundi, Pierre Nkurunziza ambapo waliambatana na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
Lakini, pasi na shaka jukumu hilo kubwa umemuachia Kikwete ambaye bado anaonekana ana nguvu za kuweza kukimbia huku na kule kumsaidia Rais Magufuli kuishauri na kumwakilisha kuongeza hadhi na heshima ya Tanzania katika baadhi ya matukio makubwa duniani kama ilivyotokea hivi karibuni katika shughuli ya kuapishwa Rais mpya wa Burundi na mazishi ya Rais wa zamani wa Burundi, Pierre Nkurunziza ambapo waliambatana na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
Mkapa, nakumbuka Desemba 21, 2005, katika uwanja
huo wa Uhuru (zamani Uwanja wa Taifa ama shamba la bibi) ambao Julai 28, 2020,
tumeutumia kukuaga, ulimkumbatia kwa furaha Jakaya Kikwete mara tu baada ya
kumaliza awamu yako na kumkabidhi madaraka ya kuongoza nchi.
Nakumbuka siku hiyo nikiwa mmoja wa wapiga picha
za habari walioshiriki kuripoti tukio hilo, nilishuhudia ukinusurika kuanguka
kwa kukosea kukanyaga ngazi ulipokuwa
ukiondoka kwa furaha iliyopitiliza katika jukwaa maalumu la kuapishia. Kitendo
hicho kiliambatana na furaha ya kuutua kwa usalama mzigo mkubwa wa kuiongoza
nchi na vilevile hukuamini kama kweli umestaafu na kumuachia jahazi hilo Jakaya
Mrisho Kikwete.
Pia, tukio hilo limenikumbusha wakati wa hafla ya
uzinduzi wa kitabu chenye mkusanyiko wa hotuba zako kilichochapishwa na Kampuni
ya Mkuki. ambapo ulimuuliza mchapishaji kuwa Dar es Salaam kuna bookshop ngapi?
Mimi nilikuuliza kwa nini unauliza swali kama hilo? Ukajibu; "Nikiondokana na rokapu (Ikulu) hii
nataka niwe najisomea vitabu." Ukaulizwa tena, kwanini Ikulu unaiita
rokapu? Ukajibu kwa kuhamaki; "Hapa Ikulu si pazuri kabisa, huna
uhuru." Ukaondoka huku ukicheka na kutuacha tukitafakari juu ya hilo.
Pia,nakumbuka ukiwahutubia wananchi kwa mara ya kwanza katika ziara yako ya kwanza ulipopata madaraka ya kuiongoza nchi,kutoka kwa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Kigamboni Dar es Salaam, uliwaambia "Ndugu wananchi mkae mkijua matatizo yenu ndiyo mwanzo wa maendeleo yenu. Kauli hiyo iliwatatiza wananchi hao wa kawaida, wakabaki wanaulizana, hivi Rais amekuja kutudhihaki, yaani matatizo yetu ndiyo maendeleo, wapi na wapi?!!!
Baada ya kuona hawajakuelewa, ukairudia kauli hiyo na kuwaambia kuwa "wananchi huo ndiyo ukweli, bila kuwa na matatizo hamuwezi kupiga hatua za kimaendeleo. Unapotatua tatizo lako linalokukera kwa muda mrefu basi unakuwa umepiga hatua fulani ya maendeleo yako". ulifafana kidogo, lichaya kwamba baadhi yao walikuwa bado hawajakuelewa.
Pia,nakumbuka ukiwahutubia wananchi kwa mara ya kwanza katika ziara yako ya kwanza ulipopata madaraka ya kuiongoza nchi,kutoka kwa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Kigamboni Dar es Salaam, uliwaambia "Ndugu wananchi mkae mkijua matatizo yenu ndiyo mwanzo wa maendeleo yenu. Kauli hiyo iliwatatiza wananchi hao wa kawaida, wakabaki wanaulizana, hivi Rais amekuja kutudhihaki, yaani matatizo yetu ndiyo maendeleo, wapi na wapi?!!!
Baada ya kuona hawajakuelewa, ukairudia kauli hiyo na kuwaambia kuwa "wananchi huo ndiyo ukweli, bila kuwa na matatizo hamuwezi kupiga hatua za kimaendeleo. Unapotatua tatizo lako linalokukera kwa muda mrefu basi unakuwa umepiga hatua fulani ya maendeleo yako". ulifafana kidogo, lichaya kwamba baadhi yao walikuwa bado hawajakuelewa.
Ukifika huko tunaomba uwape salamu zetu baadhi ya
viongozi wetu waliotangulia mbele ya haki; Baba wa Taifa, Julius Kambarage
Nyerere, Rais wa zamani wa Zanzibar, Abeid Aman Karume, Makamu wa Rais, Dk.
Omary Ali Juma, Waziri Mkuu wa zamani, Rashid Mfaume Kawawa, Spika wa zamani,
Adam Sapi Mkwawa, Spika wa zamani, Samwel Sitta na Rais wa zamani wa Zanzibar,
Aboud Jumbe.
Mkapa, tutasema mengi, tutauliza maswali mengi na
kuhoji mengi, lakini hatutaweza kupata majibu ya moja kwa moja kutoka kwako,
kwani Mungu tayari keshachukua roho yako, amekupenda zaidi yetu na ndiyo
aliyetuleta duniani na ana mamlaka ya kutuchukua, lakini tutaendelea kukuenzi
kwa mema na mambo mengi uliyoitendea Tanzania.
Lakini baadhi ya majibu tutaendelea kuyapata
kupitia kwenye kitabu chako cha Maisha Yangu, Kusudio Langu pamoja na hotuba
zako zilizojaa maneno yenye hekima, busara na yenye mafunzo mengi. Pia kizazi
na kizazi kitaendelea kuifaidi mifumo mbalimbali ya kiuchumi uliyoianzisha
wakati wa utawala wako, ambayo nimeitaja kwa uchache hapo chini katika makala
hii. Kweli ulikuwa hazina na utaendelea kuwa hazina yetu.
Ulikuwa ni mmoja wa wanasiasa "senior"
tuliokuwa tumebaki nao Tanzania na Afrika kwa ujumla uliyekuwa na kofia ya
uongozi na kofia ya uanazuoni "intellectual" kwa wakati mmoja. Sio
kwa sababu ya kupita Chuo kikuu. Ni kwa sababu hukuwa "mvivu wa
kufikiri". Unaweza ukasoma sana na bado usiwe msomi
"intellectual".
Mkapa, alikuwa na uwezo wa kuona mzizi, mti ,
matawi na matunda yake kwa wakati mmoja. Ukisikiliza "maoni" yake
wakiwa Afrika ya Kusini pamoja na Rais Thabo Mbeki, Paul Kagame, Olusegun Obasanjo na wengineo anasema "Tatizo la
Afrika tunaangalia matunda tunaacha mzizi, mti na matawi yake. Kwa kweli ujumbe
huu unafikirisha.
“Tunalalamikia viongozi wanatuangusha wakati
"hao viongozi" wanatokana na
aina ya jamii tuliyonayo. Mfano kama jamii imejaa ubinafsi, usitegemee
"mjumbe" asiwe mbinafsi. Kwani mjumbe ni nani? ametoka wapi?
anamwakilisha nani? wengine wako wapi? kwanini sio wajumbe? nani amewazuia?” Ni
baadhi ya maneno yake mkapa yatakayondelea kuishi licha ya yeye kupumzishwa
katika nyumba yake ya milele, kijijini kwake Lupaso, Masasi.
Baadhi mifumo ya uimarishaji uchumi aliyoianzisha
Mkapa (Mr. Clean) wakati wa utawala wake;
• Ilianzishwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuimarisha
ukusanyaji wa mapato Julai 1996.
• Ukaanzishwa mfumo wa VAT Julai 1998
• Public Service and Act pamoja na Public Procurement
Regulatory
Authority vilianzishwa 2001
• Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
Julai 2001
• Taasisi ya Kuzuia Rushwa (Prevention of Corruption
Bureau)
• Regulatory Agencies nyingine zilianzishwa nyingi ikiwa ni
pamoja na
Brela, EWURA, TCCRA, SUMATRA, Viwanja
vya ndege,Maji safi
na taka, TANROADS,na Baraza la Taifa la
Biashara (National Business Council)
Ili kuyapata hayo ikaanzishwa
• Vision 2025
• MKUKUTA
• MKURABITA
• Mini Tiger Plan 2020
• Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
• Bima ya Taifa
• Mageuzi katika Elimu, DEDP na SEDP
• Mradi wa maji ziwa
Victoria,
Mungu ailaze roho yako mahali pema peponi. Amen.
Ndimi, Richard Mwaikenda
Mpigapicha/Mwandishi
0754264203
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇