KATIKA
mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2020, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF)
unatarajia kulipa fidia kiasi cha shilingi bilioni 8.5, Mkurugenzi Mkuu wa
Mfuko huo Bw. Masha Mshomba amesema.
Bw.
Mshomba ameyasema hayo katika banda la WCF kwenye maonesho ya 44 ya biashara ya
kimataifa ya Dar es Salaam yanayokwenda na kauli mbiu isemayo “Uchumi wa
Viwanda kwa Ajira na Biashara endelevu”
“Ujio
wa Mfuko wa Fidia umekuwa ni mkombozi, mfanyakazi anaweza kupata ulemavu na
asiweze tena kurudi kazini kwahiyo yeye na familia yake wanakuwa ni tegemezi
lakini kwa uwepo wa Mfuko, hiyo imekuwa ni historia kwasababu sasa Mfuko
unamlipa fidia na hata kwa familia pia pale kwa bahati mbaya inapotokea
mfanyakazi amefariki kutokana na kazi.” Alisema Bw. Mshomba.
“Na
ieleweke kwamba jukumu kubwa la Mfuko ni kulipa fidia kwa Mfanyakazi aliyepata
ulemavu utokanao na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi kwa mujibu wa mikataba
ya ajira na katika hili ulipaji wa Mafao ya fidia tumepiga hatua kubwa sana
kwani katika mwaka wa kwanza tangu tuanze kulipa fidia Julai 1, 2016, tulilipa
shilingi bilioni 1.5 na katika mwaka huu wa fedha ulioisha Juni 30, 2020 Mfuko
unatarajia kulipa jumla ya shilingi bilioni 8.5.” Alibainisha Bw. Mshomba.
Alisema,
sambamba na kulipa fidia Mfuko pia umeweka mkazo kwenye suala la elimu kwa
wadau wa Mfuko wakiwemo waajiri, wafanyakazi lakini pia madaktari na watoa
huduma wengine wa afya.
Akifafanua
zaidi alisema, waajiri na wafanyakazi pamoja na mambo mengine wamekuwa wakifundishwa kuzingatia sheria
ya Usalana na Afya Mahali pa kazi(OSH) ili hatimaye kupunguza ajali au magonjwa
yatokanayo na kazi.
‘’Kundi
lingine muhimu katika kuhakikisha Mfuko unatekeleza majukumu yake kwa ufanisi
na kwa haki ni madaktari na watoa huduma ya afya.
Tumetoa
mafunzo kwa madaktari na watoa huduma ya afya wapatao 1,064 nchi nzima kuhusu
namna ya kufanya tathmini ya ulemavu na magonjwa yatokanayo na kazi (Assessment of occupational injuries and diseases) ili
hatimaye mfuko uweze kutoa fidia stahiki na kwa wakati.” Alisema.
Bw.
Mshomba alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli kwa kutimiza ndoto yake ya kuona nchi inafika katika
uchumi wa kati.
“Mlimsikia
Mhe. Rais wakati akifunga bunge hivi karibuni, alitoa tathmini ya viwanda
nchini na kusema kumekuwepo na ongezeko kubwa la viwanda na sisi kama Mfuko
tunao wajibu mkubwa wa kuhakikisha
tunalinda nguvu kazi ya nchi kwa kuwahudumia wafanyakazi walioko viwandani ili
waweze kurudi kazini haraka na hata wale waliopata ulemavu pengine warudi
katika kazi zao au kazi zingine mbadala na kwa kufanya hivyo tutakuwa
tumetimiza lile jukumu la kusaidia kukuza uzalishaji viwandani na hivyo
kupelekea uchumi kukua.” Alifafanua Bw. Mshomba.
Kuhusu
maonesho hayo ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu huyo
alisema, yametoa fursa ya kuendelea kutoa elimu kuhusu masuala ya Fidia, kama
kauli mbiu inavyosema, hapa ndio mahala pake hasa kwa Mfuko kukutana na wadau
wake muhimu, yaani waajiri na wafanyakazi.
“Sabasaba
imekuwa nzuri sana kwakweli tumepata wageni wengi katika banda letu na kama
kawaida imekuwa ni sehemu nzuri sana ya kuelezea huduma zetu pia nafasi nzuri
ya kuelezea mchango wetu katika serikali ya awamu ya tano chini ya Dkt.John
Pombe Joseph Magufuli.”Alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Masha Mshomba (aliyesimama) akimsikiliza mwananchi huyu aliyefika kwenye banda la Mfuko huo katika viwanja vya Julius Nyerere maarufu Sabasaba ili kupata huduma. Anayemuhudumia ni Afisa Matekelezo Mwandamizi wa Mfuko Bi. Melinda Matinyi.
Muonekano wa banda la WCF Sabasaba
Bi. Melinda akimsikiliza mteja
Afisa Mwandamizi wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSH), Bi. Tumaini Kyando (kushoto) akitoa elimu kuhusu OSH na shughuli za Mfuko kwa ujumla wake.
Afisa msaidizi wa Madaina Tathmini WCF, Dkt. Brian (kushoto) akimsikiliza mwananchi huyu aliyefika katika banda la Mfuko kupata huduma.
Afisa Mwandamizi wa Madai, WCF, Bw. Silvanus Kulosha (kushoto) akimfafanulia kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo shughuli za Mfuko mwananchi aliyetembelea banda la WCF.
Afisa Mwandamizi wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSH), Bi. Tumaini Kyando (kushoto) akitoa elimu kuhusu OSH na shughuli za Mfuko kwa ujumla wake.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇