Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa
(aliyevaa kofia), akimsikiliza Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Dodoma, Bi. Bertha Bankwa, akieleza kuhusu maendeleo ya upanuzi wa kiwanja cha ndege
mkoani hapo wakati Naibu Waziri huyo alipokagua maendeleo ya upanuzi wa
barabara ya kuruka na kutua ndege na sehemu ya maegesho ya ndege. Kushoto ni Meneja
wa Wakala Barabara (TANROADS) Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu.
Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa
maegesho ya ndege katika kiwanja cha ndege cha Dodoma. Upanuzi huo utakamilika
mapema mwezi Agosti na kukamilika kwakwe kutaruhusu ndege kubwa aina ya Airbus zaidi
ya tatu kupaki kwa wakati mmoja.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa,
akizungumza na wataalam wa Kampuni ya CHICCO inayotekeleza mradi wa upanuzi wa
kiwanja cha ndege cha Dodoma, wakati Naibu Waziri huyo alipokagua maendeleo ya upanuzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege na sehemu ya
maegesho ya ndege.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akitoa
maelekezo kwa Meneja wa Ujenzi na Matengenezo
kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Mhandisi Focus Kadeghe, alipokagua maendeleo ya upanuzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege na sehemu ya maegesho
ya ndege katika kiwanja cha ndege cha Dodoma.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa
(aliyevaa kofia), akitoa maelekezo kwa Meneja
wa Wakala Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu, alipokagua maendeleo ya upanuzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege na sehemu ya
maegesho ya ndege.
Serikali
imewatoa wasiwasi wafanyabiashara na watumiaji wa usafiri wa anga kwa kuahidi
kuanza ujenzi wa Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Msalato jijini Dodoma mara
baada ya taratibu zilizobaki kukamilika.
Akizungumza
mjini humo mara baada ya kukagua maendeleo ya upanuzi wa barabara ya kutua na kuruka
ndege na sehemu ya maegesho ya ndege Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa,
amesema lengo la kutekeleza mradi huo ni kurahisisha usafirishaji kwa kuruhusu
mashirika mengi zaidi kutumia kiwanja hicho.
“Niwahakikishie
watanzania kuwa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato kitajengwa na kwa
wakazi wa Dodoma ambao wanadai fidia, Serikali itahakikisha wanalipwa kabla ya
kuanza kwa ujenzi huo", amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Aidha,
Naibu Waziri Kwandikwa ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaongeza idadi
ya ndege ikiwemo ndege zenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 200 kwa wakati mmoja.
Naibu
Waziri Kwandikwa ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha usafiri wa anga
nchini kwa kuendelea na miradi mikubwa ya uboreshaji wa viwanja vya ndege zaidi
ya kumi na moja nchi nzima vikiwemo vya Lindi, Songea, Shinyanga, Musoma,
Songwe na Mtwara.
Kwa
upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Dodoma, Mhandisi
Leonard Chimagu, amesema mradi umefikia zaidi ya asilimia 70 na kuahidi
kuendelea kumsimamia mkandarasi ili kuhakikisha viwango vinazingatiwa.
Mhandisi
Chimwangu, ameongeza kuwa kwa sasa kazi zinazoendelea na ni kuweka tabaka la pili
la barabara ya kuruka na kutua ndege mara baada ya tabaka la kwanza la
kushindilia mawe kukamilika.
Naye
Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Dodoma, Bi Bertha Bankwa, amesema kuwa kukamilika
kwa upanuzi wa sehemu ya maegesho ya ndege utaruhusu ndege zaidi ya nne kupaki
kwa wakati ikiwemo ndege kubwa ya AIRBUS.
Mradi wa
upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Dodoma, unafanywa na Kampuni ya CHICCO, na
unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti mwaka huu na utagharimu kiasi cha shilingi
bilioni 3.5.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇