Luteni Kelly NKurunziza, kijana mkubwa wa aliyekuwa rais wa Burundi Pierre Nkurunziza ametunukiwa tuzo ya shujaa na aliyemrithi baba yake rais Evariste Ndayishimiye katika sherehe maadhimisho ya kupatikana kwa uhuru wa nchi hiyo.
Machi, Kelly Nkurunziza alipewa jukumu na baba yake kuwa mwanajeshi ambaye alikufa ghafla Juni, na kupandishwa ngazi hadi luteni wa pili baada ya kumaliza mafunzo katika kituo cha mafunzo ya kijeshi nchini Burundi.
Alipandishwa cheo hadi luteni siku moja kabla ya sherehe za Julai mosi.
Rais Ndayishimiye alisema, "Kwasababu ya nidhamu yake, ujasiri na ushujaa wake, kila aliyemuona alisema huyu kijana mdogo ana uwezo wa kuwa mfano wa kuigwa".
Bwana Ndayishimiye alisema kijana huyo, ambaye ndio mkubwa wa marehemu Pierre Nkurunziza, alisomea nje ya nchi na punde tu baada ya kumaliza akajiunga na kituo cha mafunzo ya jeshi ambapo alihitimu.
Bwana Ndayishimiye pia aliwatunuku wanajeshi wengine wawili, ambao hivi karibuni walipigana na majirani zao kaskazini katika ziwa Rweru kati ya Burundi na Rwanda. Mwanajeshi mmoja aliaga dunia.
Mei, wanajeshi wa Burundi na Rwanda walipigana katika ziwa hilo lililopo mpakani, moja ya matukio ya kijeshi ya hivi karibuni yanayoakisi hali ya wasiwasi ambayo imekuwepo kwa miaka mitano kati ya nchi hizo jirani.
Na, Jeshi la Rwanda likatangaza kwamba limempiga risasi mwanajeshi wa Burundi katika ziwa hilo.
Aidha katika sherehe hiyo, Bwana Ndayishimiye pia alimtunuku tuzo aliyekuwa rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete, kwa urafiki wake na Burundi.
Bwana Kikwete alihudhuria mazishi ya Nkurunziza pamoja na kuapishwa kwa Ndayishimiye mwezi uliopita. Hafla mbili ambazo viongozi wengi wa kikanda hawakuhudhuria.
Burundi ina mengi ya kumshukuru Kikwete kwa yanayofahamika au hata pengine yasiyojulikana.
Lakini ambalo bado lipo kwenye kumbukumbu za wengi, ni kukaribisha wakimbizi kufuatia machafuko yaliyotokana maandamano nchini humo pamoja na jaribio la kumpindua Nkurunziza.
Baadhi ya wakimbizi hao wangali Tanzania mpaka sasa japo Rais Magufuli mara kadhaa amewataka kurudi Burundi akisema hali ya usalama imeimarika.
Jaribio la mapinduzi lilitokea Nkurunziza akiwa anahudhuria mkutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki mjini Dar es Salaam.
Kikwete akiwa rais wa Tanzania wakati huo anadaiwa kuwa alitoa msaada mkubwa kwa Nkurunziza.
Pia unaweza kutazama:
Taarifa ambazo hazijathibitishwa zinadai wanajeshi wa Tanzania walimpatia ulinzi Nkurunziza hadi kurejea nyumbani na safari yake ikawa salama - ni jambo ambalo wafuasi wengi wa Nkurunziza daima wataendelea kumshukuru Jakaya Mrisho Kikwete.
Aidha, wakati ambapo Kikwete alikuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, iliunga mkono Burundi na kupinga vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya nchi hiyo.
Kwa nchi za Afrika Mashariki, Rwanda haikuunga mkono unamuzi huo huku Uganda na Kenya zikionesha kutokuwa na uhakika.
Lakini Tanzania ilikuwa na uhakika na inachoshikilia kiasi kwamba Jumuiya ya Afrika mashariki ilikataa kutia saini makubaliano ya kiuchumi na Umoja wa Ulaya na kutoa masharti ya kuondolewa vikwazo dhidi ya Burundi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇