Na Felix Mwagara, MOHA, Morogoro.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amesema kasi ya utendaji kazi wa Kamishna Generali wa Jeshi la Magereza Nchini, (CGP) Suleiman Mzee, imemfurahisha kutokana na mabadiliko makubwa ya maendeleo kwa kipindi cha muda mfupi tangu alipoteuliwa kuliongoza Jeshi hilo.
Akizungumza katika hafla ya kuzindua mashine ya kuchimbia ‘excavator’ iliyofanyika Gereza la Mbigili, Wilaya ya Mvomero, Mkoani Morogoro, jana Waziri Simbachawene alisema Jeshi la Magereza lilinufaisha wachache katika kipindi cha nyuma, lakini tangu kuteuliwa kwa CGP Mzee, mafanikio makubwa yameanza kuonekana.
“CGP tangu ateuliwa kwa muda mfupi tuu, amenunua matipa matatu, basi la timu ya mpira na mashine hii excavator kwa fedha zilizopatikana ndani ya Jeshi, haya mambo yalikuwa ni ndoto jamani, utendaji kasi yake mzuri na anania ya kuleta mabadiliko zaidi ndani ya Jeshi hili la Magereza, nimefurahishwa sana na utendaji kazi wake na fikisheni pongezi zangu,” alisema Simbachawene.
Aliongeza kuwa, askari na maafisa wa Jeshi hilo Nchini, hawapaswi kumpinga, wanapaswa kumuelewa na kumuunga mkono na kuendana na kasi yake katika kipindi hiki ambacho Jeshi limeingia vitani kwa ajili ya kufanyika kwa mabadiliko makubwa.
Pia aliwataka askari Magereza kuendelea kufanya kazi usiku na mchana, na kila mtu akitoka kazini ajiulize nini amefanya kwa siku hiyo, kwa hatua hiyo itawezesha jeshi kubadilika zaidi katika uzalishaji na pia maisha ya askari nayo yatabadilika.
Aidha, Waziri Simbachawene katika hafla hiyo, ameitambulisha kauli mbiu mpya ya Jeshi hilo nchini ambayo inasema ‘Magereza Tanzania, Fikra Mpya, Mtazamo Mpya, Kuchapa Kazi kwa Bidii na Kujitegemea.’
Kwa upande wake Mkuu wa Magereza Mkoa huo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi hilo (SACP), Ismail Mlawa, alimshukuru Waziri Simbachawene kwa jitihada zake za kuliletea mabadiliko Jeshi hilo, na pia anamuomba Mheshimiwa Rais John Magufuli amrudishe katika Wizara hiyo baada ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
“Mheshimiwa Waziri, tunakushukuru sana kwa kuja kuzindua mashine hii mpya, na pia hizi ni jitahada zako pamoja na Afande Kamishna Generali wa Jeshi hili, tunaamini nawe umechangia kupatikana kwa mashine hii pamoja na vifaa vingine, tunakuombea urudishwe kuiongoza Wizara hii hata baada ya uchaguzi,” alisema Mlawa.
Naye Mkuu wa Gereza la Mbigili, lililopo Wilayani Mvomero, Mkoani humo, SSP Muyengi Burilo, akisoma taarifa ya Gereza hilo pamoja na mashine hiyo mpya iliyonunuliwa, alisema mashine hiyo imenunuliwa shilingi milioni 331,060,800 na itakuwa inachimba visima, kung’oa miti, kuchimba mitaro na pia itatumika kukodisha katika Taasisi mbalimbali za Serikali.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇