LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 5, 2020

WAZIRI MPINA AWATAKA WAWEKEZAJI NCHINI KUWEKEZA KWENYE VIWANDA VYA USINDIKAJI WA MAZIWA


Charles James, Michuzi TV

SERIKALI imezitaka Halmashauri zote nchini kuzingatia bei elekezi ya chanjo ya mifugo na atakayekaidi hatua kali za kisheria na kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina leo jijini Dodoma wakati akihitimisha wiki ya Maziwa duniani ambapo ametumia nafasi hiyo kuwataka wenye viwanda vya kusindika maziwa kuongeza uzalishaji zaidi.

Waziri Mpina ametumia nafasi hiyo pia kuiagiza Bodi ya Maziwa na Wadau wote wa maziwa kuweka mkakati wa pamoja wa kuhakikisha ndani ya miaka miwili ijayo Tanzania inazalisha maziwa ya kutosha na kusiwe na haja ya kuagiza nje ya Nchi.

Amesema katika kuhakikisha uzalishaji wa maziwa unaongeza serikali imewaunganisha wawekezaji wa maziwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ili waweze kupatiwa mifugo sambamba pia na kutoa msamaha wa kodi kwenye sekta hiyo.

Mpina amesema kiwango cha kunywa maziwa kwa watanzania kinapaswa kuwa Tani 200 lakini hadi sasa kiwango kinachonyweka ni tani 54 hivyo kuwataka watanzania kuongeza unywaji wa maziwa kwani husaidia kuboresha kinga za mwili na kukuza ubongo.

" Maziwa ni mlo kamili hasa katika kuimarisha mifupa na kuweka ubongo sawa, na yana viini lishe vya kuimarisha pia kinga za mwili. Kwahiyo ndugu zangu ni muda sasa wa kuhamasisha unywaji wa maziwa nchini.

Tanzania ni Nchi ya pili kwa kuwa na Ng'ombe wengi nyuma ya Ethiopia. Tuna Ng'ombe Milioni 33 lakini Ng'ombe wanaozalisha maziwa ni Milioni 1.9 na kiwango cha maziwa tunachozalisha ni Bilioni tatu ambacho ni kidogo kulinga na mifugo tuliyinayo, nitoe wito kwenu nyote kuhamasisha uzalishaji na unywaji wa maziwa," Amesema Mpina.

Amesema kwa sasa kuna programu ya kuhamasisha unywaji wa maziwa mashuleni kwa baadhi ya mikoa na kusisitiza sasa ni wakati wa kila mkoa kuweka mkakati wa kuhimiza unywaji wa maziwa kwenye kila shule ndani ya mikoa yao.

Ametoa wito pia kwa wawekezaji nchini kukimbilia fursa ya kuwekeza kwenye usindikaji wa maziwa kwani viwanda vilivyopo kwa sasa vinazalisha asilimia 23 tu ya maziwa na vipo 99.

Awali akizungumzia wiki hii ya maziwa, Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa, Dk Sophia Mrote amesema wiki ya Maziwa imekua ya manufaa sana kwani pamoja na kujadili changamoto zilizopo kwenye sekta hiyo pia waligawa Lita 1650 kwenye maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma.

Amesema ndani ya wiki hiyo ya maziwa walikutana wadau wote wa maziwa na kujadili mambo mbalimbali yatakayoweza kuivusha sekta hiyo ili kufikia hatua ya kuzalisha maziwa mengi na kukuza soko hilo hadi nje ya mipaka ya Nchi.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashata na wa maziwa nchini, Meneja Masoko wa Kiwanda cha Tanga Fresh, Ally Sechonge ameipongeza serikali kwa namna inavyochukua hatua za kukuza sekta ya maziwa huku akiahidi kuwa wataendelea kuzalisha maziwa bora yatakayonyweka na watanzania wote.

" Sisi kama Tanga Fresh tunatambua mchango mkubwa unaofanywa na serikali katika kuinua sekta hii na ndio maana tumeshiriki katika kugawa maziwa lakini pia kugawa vifaa vya kupambana na Ugonjwa wa Corona zikiwemo ndoo za kunawia maji tiririka na Barakoa," Amesema Sechonge.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi akizungumza na wandishi wa habari na wadau wa maziwa leo jijini Dodoma wakati wa kilele cha wiki ya maziwa. 
Wadau mbalimbali wa maziwa wakifuatilia mkutano wa pamoja wa kujadili mambo mbalimbali ya sekta ya maziwa katika wiki ya maziwa ambayo kitaifa imefanyika jijini Dodoma.
 Wadau mbalimbali wa maziwa wakifuatilia mkutano wa pamoja wa kujadili mambo mbalimbali ya sekta ya maziwa katika wiki ya maziwa ambayo kitaifa imefanyika jijini Dodoma.
 Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (wa pili kushoto) akinywa maziwa kuashiria kufunga wiki ya maziwa nchini sambamba na Viongozi wengine akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi (wa tatu kutoka kushoto) na Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa, Dk Sophia Mrote (katikati). 
 Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa, Dk Sophia Mrote akizungumza leo jijini Dodoma wakati wa ufungaji wa siku ya maziwa.
 Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akiwaongoza viongozi na wadau wa maziwa kunywa maziwa ikiwa ni kuhamasisha unywaji wa maziwa nchini.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages