Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera akizungumza na Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa huo, Kakozi Amri pamoja na Wanahabari (hawapo pichani)jinsi ya kuimarisha masoko ya mazao ya wakulima na kusisitiza utumiaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa wakulima wa mkoa huo ili waweze kufaidika na kuwawezesha kuinua maisha ya mkulima mmoja mmoja na uchumi wa mkoa kwa ujumla
Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Katumba AMCOS, Azory Ntondelo akielezea faida walizozipata baada ya kujenga ghala la kuhifadhia pembejeo na mazao yao wakati wa mauzo.
Moja ya ghala la kuhifadhia mazao lililojengwa na chama cha ushirika cha Nsimbo AMCOS kilichopo Wilaya ya Nsimbo, mkoani Katavi.
**********************************
Mpanda, Katavi
Katika kumkokomboa mkulima, mkoa wa Katavi umeanzisha na kusimamia ipasavyo Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ili kumpatia bei nzuri na kuondoa mnyororo wa mtu wa kati aliyekuwa akinunua mazao ya wakulima kwa bei ya chini na kujipatia faida kubwa. Mfumo huu umekuwa ukitekelezwa kupitia masoko ya wazi na soko la bidhaa (TMX).
Akizungumza katika mahojiano maalum juzi, Juni 16, 2020 mjini Mpanda, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Juma Homera, amesema kuwa mkoa wa Katavi umedhamiria kuimarisha masoko ya mazao ya wakulima ili yaweze kuwapatia bei nzuri na kuwezesha kuinua maisha ya mkulima mmoja mmoja na uchumi wa mkoa kwa ujumla.
“Katika kuimarisha kilimo na masoko bora, kwa ajili ya kumkomboa mkulima wa mkoa wa Katavi tuameanzisha Stakabadhi ya Mazao Ghalani ambayo inaendelea kufanya vizuri sana katika mkoa wetu wa Katavi kwa lengo la kukata mnyororo wa mtu wa kati ambaye anakuwa kama dalali katika masoko ya mkulima,” alisema Mhe. Homera.
Mauzo ya Ufuta kwa Vyama vya Ushirika kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala umewezesha jumla ya kilo 1,370,718 kuuzwa katika minada mitatu (3) iliyofanyika mkoani Katavi msimu huu. Kutokana na mauzo hayo, Shilingi 2,767,200 zililipwa na makampuni yaliyoshiriki kwenye minada hiyo. Kati ya fedha hizo wakulima walilipwa Shilingi 2,555,511,910 kupitia akaunti zao za benki.
Aidha, katika fedha hizo jumla ya Shilingi 82,243,080 zimeingia katika Halmashauri za mkoa wa Katavi kama ushuru ambazo zitatumika katika kuimarisha miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo hayo.
Akizungumzia kuhusu umuhimu wa Ushirika, Mkuu wa Mkoa wa Katavi amesema kuwa viongozi wote wa mkoa huo wamekuwa wakihimiza wananchi kujiunga katika vyama vya ushirika kwa kuwa ndiyo moyo wa uchumi wa mwananchi mmoja mmoja katika ngazi zote kuanzia kwenye vijiji, kata, tarafa, wilaya na mkoa.
“Katika Mkoa wetu wa Katavi tumekuwa tukisimamia Ushirika kwa kushirikiana na timu yangu yote ya mkoa na wilaya zake ambapo vyama vya aina mbalimbali vimeanzishwa katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi,” amesema Mhe. Homera.
Kwa upande wake Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Katavi, Kakozi Amri amesema kuwa kumekuwepo na ushirikiano mkubwa katika usimamizi wa Vyama vya Ushirika kati ya viongozi wa mkoa, wilaya, Halmashauri. Ambapo ushikiano huo umewezesha kuongezeka kwa idadi ya vyama, wanchama na idadi ya mazao yanayoshughukiwa na vyama vya ushirika.
“Hapo awali ushirika katika mkoa wa Katavi ulikuwa ukishughulikia zao moja tu la Tumbaku, lakini sasa vyama vya ushirika katika mkoa wetu vinajihusisha pia na mazao ya Pamba, Ufuta, Korosho na Alizeti. Wakulima wameweza kuongeza kipato kutokana na kuuza mazao haya kwa bei nzuri ikilinganishwa na wakati yalikuwa yanauzwa nje ya mfumo wa ushirika,” amesema Kakozi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇