LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 28, 2020

RAIS DK. MAGUFULI AZINDUA MRADI WA MAJI WA KIBAMBA-KISARAWE WA SH. BILIONI 10.6 ZILIZOKUSANYWA NA DAWASA

Rais Dk. John Magufuli akifungulia maji alipozindua Mradi mkubwa wa maji wa Kibamba-Kasarawe, katika hafla iliyofanyika Wilayani Kisarawe mkoa wa Pwani, leo.

Kisarawe, Pwani
Rais Dk.  John Magufuli leo Juni 28, 2020 amezindua mradi wa maji wa Kibamba – Kisarawe uliotekelezwa kwa gharama ya sh. Bilioni 10.6 ambazo zimetokana na makusanyo ya ndani ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).

Sherehe za uzinduzi wa mradi huo ambao umetekelezwa kufuatia maelekezo aliyoyatoa Rais Magufuli, Juni 21, 2017,  zimefanyika Kisarawe Mkoani Pwani na kuhudhuriwa na wananchi na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, viongozi wa Dini na viongozi wa Mkoa wa Pwani wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhandisi Evarist Ndikilo.

Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA ambayo ndio imetekeleza mradi huo Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema mradi huo wenye mtandao una Kilometa 15.65 za bomba kuu, kilometa 48 za mabomba ya usambazaji, matenki mawili ya lita Milioni 6.5 na pampu 2.

Mradi huu unawanufaisha wananchi wa kata za Kisarawe, Kazimzumbani, Masali, Kibuta, Kiluvya, Kwemba, Kisopwa na Mloganzila. Pia DAWASA inapanua mradi huo kwa shilingi Bilioni 7.7 ili uwafikie wananchi wa Pugu, Gongolamboto, Ukonga, Airwing, Banana, Mongolandege, Kinyerezi, Chanika na Segerea ambapo utaungana na mradi wa maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini. 

Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa amemueleza Rais kuwa pamoja na kutekeleza agizo hilo, Wizara ya Maji imetekeleza agizo lake la kuhakikisha ukusanyaji wa mapato ya maji unaongezeka ambapo DAWASA imeongeza ukusanyaji wa mapato hayo kutoka sh. Bilioni 2.9 kwa mwezi (mwaka 2018) hadi kufikia sh. Bilioni 12.3 (mwaka 2020) na kwamba kazi kama hiyo inafanyika nchi nzima ambapo miradi 192 yenye thamani ya sh. Bilioni 163.78 inatekelezwa kwa utaratibu wa ‘Force Account’ ambapo Serikali itaokoa zaidi ya sh. Bilioni 48.73 ikilinganishwa na endapo itawatumia wakandarasi.

Rais Magufuli ameipongeza DAWASA kwa utekelezaji mzuri wa mradi huo, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuwa na mpango mzuri wa upanuzi wa mtandao wa maji, hivyo ameitaka Menejimenti ya DAWASA kuboresha maslahi ya wafanyakazi wake.

Pia Rais ameipongeza Wizara ya Maji kwa utekelezaji wa miradi ya maji nchini ambapo katika kipindi cha miaka 5 miradi 1,423 imetekelezwa hapa nchini kwa gharama ya shilingi Trilioni 3 na kwamba kutokana na juhudi hizo za Serikali hali ya upatikanaji wa maji nchini imeongezeka kutoka wastani wa asilimia 47 hadi 70.1 (Vijijini) na wastani wa asilimia 74 hadi 84 (Mijini).

Katika sherehe hizo, Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuanza mchakato wa ujenzi wa barabara ya lami kuunganisha Kisarawe na Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na ameiagiza Wizara ya Nishati kuongeza kiwango cha umeme katika Mkoa wa Pwani ili kukidhi mahitaji yote ya kilowati 73 badala ya hali ya sasa ambapo mkoa huo unapata kilowati 50.

Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kepteni Mstaafu George Mkuchika kutengua uteuzi wa Mtera Mwampamba aliyekuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Kisarawe kutokana na kukabiliwa na kashfa mbalimbali na ameagiza Afisa Tawala wa wilaya hiyo Mwanana Msumi ateuliwa kushika wadhifa huo.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages