LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 22, 2020

RAIS DK. MAGUFULI AMUAPISHA IDD HASSAN KAMANTA KUWA MKUU WA MKOA WA ARUSHA IKULU JIJINI DAR ES SALAAM

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Idd Hassan Kamanta kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam leo tarehe 22 Juni 2020. 
IKULU, Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 22 Juni, 2020 amemuapisha Bw. Idd Hassan Kimanta kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Hafla ya uapisho huo imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo pia Mhe. Rais Magufuli na ameshuhudia Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bw. Loata Ole Sanare akimuapisha Bw. Bakari Rajab Msulwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Idd Hassan Kimanta akiwaapisha Kamishna Msaidizi wa Polisi Edward Jotham Balele kuwa Mkuu wa Wilaya ya Monduli na Bw. Kenan Laban Kihongosi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Dkt. John Marko Pima ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha na Bwana Jerry Daimu Mwaga aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora.

Akizungumza baada ya viongozi hao kuapishwa, Mhe. Rais Magufuli amewataka kwenda kufanya kazi kwa ushirikiano na kwa kuzingatia maadili na viapo vyao vya uongozi, badala ya kuvutana na kugombana hali inachelewesha maendeleo ya wananchi.

Mhe. Rais Magufuli ameeleza kuwa ameamua kutengua uteuzi wa viongozi 3 wa Mkoa wa Arusha ambao ni Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Arusha na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha kutokana na viongozi hao kutoelewana na kugombana bila sababu za msingi licha ya kuonywa mara kadhaa, na ametaka vitendo hivyo visijirudie kwa wateule wapya na viongozi wengine nchini.

Amemueagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi ncini (IGP) Simon Sirro na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Brig. Jen John Mbungo kuwaonya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha Jonathan Shana na Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha Bi. Frida Wikesi kutokana na kufanya majukumu yasiyowahusu.

Pia, Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi aliwaoteua kushika nyadhifa mbalimbali kutosheka na nafasi walizoteuliwa.

Amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt. John Marko Pima kusimamia sheria na amemtaka kwenda kumaliza mgogoro wa ujenzi wa kituo cha mabasi ili ujenzi huo ufanyike haraka na wananchi wa Arusha wapate kituo chao mapema.

Viongozi hao wamekula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Halord Nsekela.


Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo, Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. Laurian Ndumbaro, Katibu Mkuu TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamuhanga, Katibu Mkuu Ikulu Dkt. Moses Kusiluka na viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.

PICHA ZAIDI
 Mkuu wa Mkoa wa Arusha Idd Hassan Kamanta akila kiapo Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Baadhi ya Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi wakila kiapo cha Uadilifu kwa Viongozi wa Umma Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Mkuu wa Mkoa wa Arusha Idd Hassan Kamanta akiwa Ikulu jijini Dar es Salaam mara baada ya uapisho.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bakari Msulwa mara baada ya tukio la uapisho Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akishuhudia Mkuu wa Mkoa wa Arusha Idd Hassan Kamanta akimuapisha Mkuu wa Wilaya ya Arusha Kenan Laban Kihongosi Ikulu jijini Dar es Salaam leo tarehe 22 Juni 2020.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na viongozi mbalimbali mara baada ya kumuapisha Idd Hassan Kamanta kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam leo tarehe 22 Juni 2020.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages