1. Usuli
Duniani kote, kwa miaka mingi, imezoeleka kwamba Jeshini ni sehemu ngumu na ni ya wanaume pekee na pia ni lazma uwe "Mtu wa Vurumai"!. Hata hivyo, mambo yote hayo mawili si sahihi kwani wapo wanawake wengi nchi mbalimbali ambao wamejiunga na Jeshi na si "Watu wa Vurumai".
Mmoja wa wanawake hao ni Meja Jenerali Mstaafu ZAWADI MADAWILI, Mwanamama mtaratibu na mstaarabu, aliyekuwa na weledi wa hali ya juu katika kazi yake jeshini kabla ya kustaafu.
Mwanamama huyu, katika utumishi wake uliotukuka, aliweka rekodi lukuki ndani na nje ya Tanzania; kama ATIKALI hii inavyodadavua.
2. Bi MADAWILI Atoka Kijiji Kimoja na MZEE WA ATIKALI
Bi MADAWILI alizaliwa Malangali, mkoani Iringa ambako pia ndiko atokako MZEE WA ATIKALI ambaye alisoma na mdogo wake Bi MADAWILI (Bi JOELIA) katika shule maarufu sana nchini, "Malangali Secondary School ", Bi JOELIA akiwa "Private student".
3. Bi MADAWILI Afiwa na Mama Akiwa "Kichanga"
Bi MADAWILI, katika safari yake ya maisha hapa duniani, alipata bahati mbaya ya kufiwa na mama yake mzazi akiwa bado "kichanga".
4. BI MADAWILI Alelewa na Bibi
Bi MADAWILI, kutokana na kuondokewa na mama yake angali kichanga, alichukuliwa na kwenda kulelewa na bibi yake mzaa mama.
5. Bi MADAWILI Asomeshwa na Baba Yake
Bi MADAWILI, baada ya kukua na kufikia umri wa kwenda shule, alichukuliwa na baba yake mzazi ambaye alikuwa ameoa mwanamke mwingine , hivyo Bi MADAWILI akalelewa na mama wa kambo.
6. Baba Yake Bi MADAWILI Awa Mwenyekiti wa TANU
Mh. PIUS MSEKWA alitanabaisha hili, tarehe 4.6.2020 ambapo alitiririka kama ifuatavyo:
"Meja Jenerali Mstaafu Zawadi Madawili ni mtoto wa aliyekuwa Mwenyekiti wa TANU wa mkoa wa Iringa".
7. Bi MADAWILI Aweka Historia JWTZ 1972
Toka Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania (JWTZ) kuundwa tarehe 1.9.1964, uundwaji uliochagizwa na maasi ya Wanajeshi tarehe 20.1.1964, ni wanaume tu ndio walikuwa wanaandikishwa JWTZ.
Mwanamke wa kwanza kuvunja mwiko huo alikuwa ni Bi ZAWADI MADAWILI aliyeandikishwa mwaka 1972, kama Taarifa Rasmi ya Makao Makuu ya Jeshi, ya tarehe 27.9.2013, inavyobainisha:
"Meja Jenerali Zawadi Madawili, aliyeandikishwa Jeshini mwaka 1972, ndiye ofisa wa kwanza mwanamke nchini kuandikishwa jeshini".
Baadaye, Afande MADAWILI alifuatiwa na Bi ESTHER KATEMBA na mwanamama wa tatu kuandikishwa jeshini alikuwa Bi GRACE MWAKIPUNDA.
8. Afande MADAWILI Aweka Rekodi
Afande MADAWILI aliweka rekodi ya kuwa Mwanamke wa kwanza nchini kuwa Luteni wa JWTZ miaka ya katikati ya 1970s.
9. Afande MADAWILI awa Mwanamke wa kwanza kuwa Brigedia Jenerali
Mwaka 2003, Afande MADAWILI aliweka rekodi nyingine JWTZ ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Brigedia Jenerali baada ya kuteuliwa kwenye cheo hicho na Mh. Dk. JAKAYA KIKWETE, Rais wa Awamu ya Tatu.
10. Afande MADAWILI Awa Mwanamke wa Kwanza kuwa Meja Jenerali
Nyota ya Mwanamama huyu, Afande MADAWILI, ilizidi kung'ara, pale alipoteuliwa, tarehe 14.10.2007, na Mh. BEN MKAPA, Rais wa Awamu ya Nne, kuwa Meja Jenerali na hivyo kuwa mwanamke wa kwanza TZ kupata cheo hicho; kama Taarifa Rasmi ya Makao Makuu ya Jeshi ya tarehe 14.10.2007 inavyobainisha:
"Hii ni mara ya kwanza kwa JWTZ kwa ofisa wa kike kupanda hadi ngazi ya Meja Jenerali tangu Jeshi hili lianzishwe mwaka 1964".
Uteuzo huo uliochagizwa na uchapakazi mujarab usio mfanowe wa Afande MADAWILI, ulimfanya Mwanamama huyu, si tu kuweka rekodi TZ, bali Afrika Mashariki nzima; kama shirika la habari la BBC lilivyotiririka tarehe 16.8.2018:
"Leo Mkenya Fatma Ahmed anakuwa mwanamke wa pili Afrika Mashariki kuwa Meja Jenerali. Mwanamke wa kwanza kuwa Meja Jenerali Afrika Mashariki alikuwa ni Bi Zawadi Madawili wa Tanzania mwaka 2007".
11. Afande MADAWILI Awa Mkurugenzi wa Wanawake
Afande MADAWILI aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Wanawake ambao walimpenda sana kutokana na aina yake ya kipekee ya uongozi na utendaji kazi.
12. Afande MADAWILI awa Mkuu Kambi ya Mgambo
Baada ya kuwa Mkurugenzi wa wanawake, tarehe 17.1.2008, Afande MADAWILI aliteuliwa kuwa Mkuu wa Kambi ya Mgambo.
13. Familia ya Afande MADAWILI ni ya Kipekee na ya Aina yake TZ:
13.1 Bi MADAWILI ni Muislam Swala 5 na mumewe ni Mkristo sana
Afande ZAWADI MADAWILI ni Mwislamu hodari wa Swala 5 wakati mumewe, Afande GERALD MKUDE alikuwa ni Mkatoliki hodari.
Licha ya kuwa dini zao ni tofauti, wawili hawa walifunga ndoa ya kikristo. Ndoa hiyo ilifungishwa na Mhadhama Kadinali Polycalp Pengo. Hata hivyo, wawili hawa walikubaliana kuwa baadaye kila mmoja ataendelea kufuata imani yake ya dini.
13.2 Mke ana Cheo Kikubwa Kuliko Mume
Kijeshi, Meja Jenerali ni mtu mkubwa kuliko Brigedia Jenerali. Hivyo, Meja Jenerali ZAWADI MADAWILI alikuwa na cheo kikubwa kuliko mmewe, Brigedia Jenerali GERALD MKUDE. Hii maana yake ni kuwa mme alipaswa kumpigia mkewe saluti; na kijeshi ni kosa kutompigia saluti mkubwa wako kikazi!.
13.3 Familia Hii yaweka Rekodi Mujarab JWTZ
Meja Jenerali ZAWADI MADAWILI na Brigedia Jenerali GERALD MKUDE, kwa miaka mingi waliishi Upanga, karibu na Makao Makuu ya Jeshi. Kwa nyumba moja kuwa na "Meja Jenerali na Brigadier Jenerali", hii inamaanisha ndiyo familia iliyokuwa na vyeo vya juu zaidi nchini.
Bahati mbaya, Brigedia Jenerali MKUDE, aliyekuwa pia Mwenyekiti wa Kamati ya Mpito ya Skauti TZ, alifariki mwezi Machi 2018. Misa yake ilifanyika tarehe 12.3.2018 katika kanisa la Mt. Imakulata, Upanga na mazishi yake yakafanyika siku hiyohiyo huko Kimara.
14. Afande MADAWILI Astaafu
Baada ya utumishi uliotukuka kwa Taifa lake, Afande MADAWILI alistaafu jeshini tarehe 30.6.2008.
15. Afande MADAWILI Ateuliwa Mjumbe wa Bodi ya Mishahara
Licha ya kuwa Mstaafu, Taifa lilikuwa bado linauhitaji mchango wa Afande MADAWILI hivyo likawa linamtumia kila linapomujitaji kwa ushauri au ushiriki wake kabisa. Tarehe 16.10.2017, takriban muongo mmoja toka astaafu, Afande MADAWILI aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Mishahara.
16. Afande ZAWADI Apewa ZAWADI na "MWALIMU NYERERE FOUNDATION"
Siku ya Wanawake Duniani, tarehe 8.3.2020 kwenye hotel maarufu ya Double Tree, Dsm, Afande MADAWILI alikuwa ni mmoja wa waliotunukiwa tuzo maalum na Taasisi ya "Mwalimu Nyerere Foundation".
Tuzo hiyo mujarab na ya kipekee iliandikwa:
"A Certificate of Appreciation in Recognition of Service and Dedication to Global Peace and Security".
17. TAMATI
Huyu ndiye "Mnyalukolo" Meja Jenerali Mstaafu ZAWADI MADAWILI, Mwanamama wa kupigiwa mfano, aliyeacha alama na rekodi lukuki si tu TZ bali Afrika Mashariki nzima.
Mwanamama huyu hodari alikuwa mwananke wa kwanza kuandikishwa jeshini mwaka 1972, kitu kilichowatia moyo wanawake wengine wafuate nyayo zake ambapo sasa wamekuwa wengi kama alivyobainisha Luteni Jenerali JAMES MWAKIBOLWA tarehe 31.5.2016:
"Tanzania inazingatia usawa wa kijinsia na sasa 25% ya wanajeshi Tanzania ni wanawake. Aidha, Jeshi la nchi yetu lina wanawake wenye vyeo vikubwa kwani tunaamini mwanamke anaweza".
KONGOLE KWAKO MEJA JENERALI MSTAAFU "MNYALUKOLO" ZAWADI MADAWILI!!!
BY MZEE WA ATIKALI ✍️✍️✍️
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇