Arusha, Tanzania
MKUU mpya wa Wilaya ya Arusha, Kenan Laban Kihongosi amesema Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli imeleta mapinduzi makubwa na yanayostahili kupongezwa katika sekta ya afya hapa nchini.
DC Kihongosi aliyasema hayo juzi wakati akifungua mafunzo ya uelimishaji wa tathmini za ulemavu uliotokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi kwa madaktari na watoa huduma ya afya ambayo aliyafungua kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Iddi Hassan Kimanta.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) yalihudhuriwa na madaktari wapatao100 kutoka mikoa minne ya Kanda ya Kaskazini wanashiriki mafunzo hayo
“Serikali imeweza kujenga jumla ya hospitali za wilaya takriban 70 nchi nzima na kila hospitali serikali imekuwa ikitoa shilingi bilioni 1.5 jambo ambalo halijawahi kufanyika tangu nchi ipate uhuru.” Alisema DC Kihongosi
Alisema, serikali pia imeendeleza na kujenga vituo vya afya takriban 352 nchi nzima na kila kituo kimekuwa kikipewa na serikali shilingi milioni 400 hadi milioni 500 na pia kuongeza ajira ya madaktari na watoa huduma ya afya katika maeneo hayo.
Mkuu huyo wa Wilaya alitaja mafanikio mengine yaliyofanyika chini ya Rais Dk. Magufuli kuwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama vile ujenzi wa bwawa kubwa la kufua umeme wa maji la Julius Nyerere (JNHPP) kwenye bonde la mto Rufiji, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR)
“Mradi wa ujenzi wa bwawa kubwa la kufua umeme la Julius Nyerere unagharimu kiasi cha shilingi trilioni 6.5 na ujenzi utakapokamilika maana yake gharama za umeme zitakuwa nafuu sana kwani kiasi cha umeme Megawati 2,115 utazalishwa hivyo tutakuwa na umeme mwingi sana na ziada utauzwa nje ya nchi Watanzania watakwenda kufurahia matunda ya serikali yao na uchumi wa viwanda utakwenda kuimarika kwani umeme wa kutosha na wa uhakika utakuwepo.” Alifafanua.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Bw. Masha Mshomba alisema mafunzo hayo ni ya awamu ya tatu na ni muendelezo wa kuongeza idadi ya madaktari na watoa huduma ya afya katika hospitali mbalimbali nchini watakaokuwa na uelewa wa jinsi ya kufanya tathmini za ulemavu uliotokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi ili hatimaye Mfuko uweze kulipa fidia stahiki na kwa wakati.
“Katika kipindi hiki cha serikali ya awamu ya tano kumekuwa na ongezeko kubwa la viwanda, ongezeko la wafanyakazi lakini pia ongezeko la ajali zitokanazo na kazi na ndio maana inabidi tuelekeze nguvu katika utoaji elimu kwa wataalamu ili tuweze kuwahudumia haraka wafanyakazi aliopata ajali na hata wale wanaopata ulemavu warudi katika kazi zao au kazi mbadala na kwa kufanya hivyo tutakuwa umetimiza lile jukulu la kujenga na kuimarisha nguvu kazi ya nchi ambayo italeta manufaa katika uzalishaji na hivyo kupelekea uchumi kukua.” Alisema Mshomba.
Alisema mpaka sasa jumla ya madaktari 956 kutoka wilaya zote nchini wameshapatiwa mafunzo. “Mfuko umepata mafanikio makubwa katika kutekeleza jukumu lake kwani katika mwaka wake wa kwanza wa ulipaji fidia Mfuko ulilipa kiasi cha shilingi bilioni 1.5 na kufikia mwishoni mwa mwezi huu wa sita 2020 Mfuko unatarajia kulipa fidia kiasi cha shilingi bilioni 8.5.” Alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Kenan Laban Kihongesi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha akitoa hotuba ya kufungua mafunzo hayo. PICHA ZAIDI>>BOFYA HAPA
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇