WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa, amesema upandaji wa zao la michikichi utaanza rasmi Oktoba mwaka huu na kama kuna mtu mmoja mmoja au kikundi wanataka kulima chikichi, waandae mashamba yao na miche ya awali watapewa bure.
“Serikal imedhamiria tulime zao hili kwa wingi na tuwasaidie wakulima kwani tunatumia pesa nyingi sana kununua mafuta ya mawese kutoka nje. Tukilima kwa wingi tutajitosheleza na hatutaagiza mafuta kutoka nje.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Mei 23, 2020) baada ya kukagua kitalu cha miche ya michikichi cha Halmashauri ya Kigoma Ujiji pamoja na kitalu cha JKT Bulombora akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kigoma.
Vile vile, Waziri Mkuu amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Mstaafu, Emmanuel Maganga, ahakikishe JKT Bulombora wanapewa ardhi waliyoomba kwa ajili ya kupanua kilimo cha michikichi.
Waziri Mkuu amesema kwa sasa Tanzania haitaagiza mbegu za michikichi kutoka sehemu yoyote duniani na badala yake itazalisha mbegu zake yenyewe. “Tayari tuna miche milioni 1.8 na wataalamu wetu wanaendelea kuzalisha.”
“Michikichi Kigoma ndio uchumi, tunataka wakulima wengi walime zao hili na Kigoma ndio chanzo cha zao la michikichi, Kigoma ndio iliyotoa chikichi kwenda nchi nyingine.”
Amesema Ilani ya CCM ya 2015-2020 imeelekeza kuwa kufufuliwa kwa zao hilo na Serikali imetekeleza hilo kwa kuanzia Kigoma na kisha yatafuatia maeneo mengine ya nchi.
Waziri Mkuu amesema awali kituo cha utafiti wa zao hilo kilikuwa jijini Dar es Salaam, Serikali ikaona haiwezekani na kuamua kukihamishia Kihuinga, mkoani Kigoma.
Amesema wataalam walihamishiwa Kihinga na tayari wameshazalisha zaidi ya miche milioni 1.8 na kazi iliyobaki ni kuwapa wananchi ili waweze kupanda kwenye mashamba yao.
Pia, Waziri Mkuu amewaagiza Maafisa Kilimo wawasaidie wakulima kulima zao hilo kitaalamu pamoja na wale wenye michikichi ya zamani jinsi ya kuitoa na kupanda michikichi hizi mpya,
Waziri Mkuu amewasisitiza wananchi wajiwekee utaratibu wa kupalilia mashamba yao ili michikichi iweze kustawi na wahakikishe hawachomi moto mapori kwani utaharibu michikichi yao.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka Wananchi nchini kote waendelee kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa COVID-19 na wafuate masharti ya wataamu. Hata hivyo amesema idadi ya wagonjwa wa COVID-19 imepungua sana nchini.
Naye, Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Omar Mgumba, amesema anamshukuru Waziri Mkuu kwa maelekezo yake ya kuagiza miche ya michikichi igawiwe bure kwa wananchi. “Tumetumia sh. bilioni 10.8 kwa ajili ya zoezi hili, na hizi ni jitihada za Rais, Dkt. John Pombe Magufuli.”
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Kasibi, amesema Wizara yao itaendelea kutekeleza majukumu yake hasa katika kuisimamia JKT katika maeneo ya kilimo, ujenzi na viwanda.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Mstaafu, Emmanuel Maganga, alisema wanaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, kwa uamuzi wa kusimamia zao hilo ili kuhakikisha linafanya vizuri na kuzalisha mafuta ya mawese.
Alisema Serikali imeanzisha chuo cha Utafiti wa zao la Michikichi cha Kihinga ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu na sasa wana miche milioni 1.5.
Naye, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba, alisema wananchi wa mkoa wa Kigoma wanamkushukuru sana Waziri Mkuu na Serikali nzima kwa jitihada za kuhakikisha zao la michikichiki linafufuliwa na kupewa hadhi. “Sisi kwetu michikichi ni fursa, ni uchumi na ni fedha.”
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇