Jeshi la Nigeria limewaokoa watu 241 waliokuwa wametekwa nyara na kundi la kigaidi la Boko Haram.
Katika taarifa, Wizara ya Ulinzi ya Nigeria imesema watu hao waliokolewa katika oparesheni iliyofanyika katika eneo la Gamoru jimboni Borno kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Nigeria John Enenche amesema mateka hao ni pamoja na wanawake 105 na watoto 136, ambao wameokolewa wilayani Mudu kwenye operesheni iliyofanywa na vikosi vya Lafiya Dole Jumapili, na sasa wako chini ya uangalizi wa madaktari.
Ameongeza kuwa, katika operesheni hiyo, vikosi vya usalama vya Nigeria vimewaua magaidi 14 wa kundi la Boko Haram na kunasa idadi kubwa ya silaha. Hali kadhalika amesema jeshi la Nigeria halikupata hasara yoyote katika oparesheni hiyo.
Kundi la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram lilianzisha shughuli zake za kigaidi mwaka 2009 kaskazini mwa Nigeria ambapo hadi sasa limepanua wigo wake hadi katika nchi za Niger, Cameroon na kaskazini mwa Chad.
Kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa, katika muongo mmoja wa shughuli za kundi la Boko Haram nchini Nigeria, zaidi ya watu elfu 30 wameuawa na wengine wanaokaribia milioni tatu kuwa wakimbizi.
Serikali ya Nigeria inayoongozwa na Rais Muhamadu Buhari imeendelea kulaumiwa na kukosolewa kutokana na kuzembea katika kukakabiliana na kundi hilo la kigaidi ambalo limevuruga usalama wa nchi hiyo na wa nchi jirani.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇