Rais Yoweri Museveni ametangaza kuwa kuvaa barakoa ni jambo la lazima nchini humo kuanzia leo katika kipindi hiki ambacho marufuku ya kutotoka nje inalegezwa.
Hatua hiyo ilitangazwa Jumatatu usiku ambapo rais Museveni alihutubia taifa baada ya kumaliza siku 35 za marufuku ya kutotoka nje ama 'lockdown'.
Museveni amesema watu wanaweza kuvalia mpaka barakoa ambazo zimeshonwa kienyeji na vitambaa.
Hata hivyo, kumekuwa na mashaka kutoka kwa wataalamu wa afya juu ya ufnisi wa barakoa za kutengenezwa nyumbani.
Katika hatua nyengine, Museveni amesema kuwa kuruhusu shughuli kuendelea kama awali inabidi kufanyike kwa umakini na mpangilio ili kuzuia virusi kusambaa kwa kasi.
Kwa kuanzia, ameruhusu maduka ya jumla, karakana za kukarabati magari, maghala kufunguliwa. Pia ameruhusu wafanyakazi wa bima na idadi ndogo ya wanasheria kurejea kazini.
Masharti mengine yaliyosalia ya marufuku ya awali bado yanaendelea mathalani kufungwa kwa mipaka ya nchi, kutoruhusu usafiri binafsi na wa umma, mikusanyiko ya watu na marufuku ya kutotoka nje usiku bado yangalipo kwa kipindi kingine cha siku 14.
Museveni amesema hatua hizo mpaka sasa zimetoa mafanikio ambayo ni kuzuia kusambaa kwa kasi kwa virusi hivyo.
"Hauwezi kuacha kulala kwa kuota ndoto mbaya. Tutaanza kufunguka taratibu bila ya kuharibu mafanikio yetu. Mafanikio hayo ni wagonjwa 89, waliopona 55 na hakuna kifo hata kimoja," ameeleza Museveni jana usiku.
Idadi mpya ya maambukizi kufikia leo asubuhi nchini humo imeongezeka kutoka 89 mpaka 97.
Kati ya wagonjwa hao, Waganda ni 57. Mpaka kufikia Jumatatu, madereva 30 wa malori walikuwa wamekutwa na corona nchini humo, kati yao Wakenya 13 na Watanzania 12.
Hatua ya Uganda kulegeza masharti ya marufuku hizo yanaendana na Rwanda na Nigeria ambazo kuanzia jana asubuhi zilifanya hivyo
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇