NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
MBUNGE wa Jimbo la Chalinze ,Ridhiwani Kikwete amekabidhiwa boksi za vigae kiwango cha kwanza 200, zenye thamani ya sh .milioni Tisa kutoka kiwanda cha vigae KEDA (Twyford)kilichopo kata ya Pera ,ambapo zinaelekezwa katika sekta ya elimu na afya.
Msaada huo ni kwa ajili ya ujenzi wa zahanati iliyoko kata ya Bwilingu na shule ya sekondari Chahuwa pamoja na ofisi ya serikali ya kata ya Miono.
Akipokea msaada huo ,Ridhiwani alisema ,kata ya Miono imekabidhiwa boksi 105 na kata ya Bwilingu ni 95 .
“;Tunakishukuru kiwanda cha KEDA ,kimekuwa ni moja ya kiwanda chenye mchango mkubwa kwa jamii ,kinashirikiana na serikali na wanaChalinze katika kutatua shughuli za kijamii “; Tulipata wazo hili na wenzangu madiwani wa kata ya Miono na Bwilingu na tunashukuru tumesaidiwa ” alifafanua Ridhiwani .
Nae ofisa uhusiano wa kiwanda hicho ,Hussein Mramba alisema ,wanaunga mkono jitihada za serikali kwa asilimia 100 ,na wanamshukuru Rais dkt John Magufuli kwa kuinua sekta ya viwanda na biashara kwani wamekuwa wakichangia pato la Taifa na kutoa ajira mbalimbali .
Mramba alieleza ,wanaendelea kusaidia pale inapohitajika na wamekuwa wakishirikiana na serikali ya kata ya Pera kwenye shughuli za kijamii.
“Tupo vizuri pia na ofisi ya mbunge wa Chalinze ,tunashirikiana na nae ,ikiwa ni moja ya dhima ya kiwanda kusaidia changamoto zilizo ndani ya uwezo wa kiwanda
“
Kwa upande wake diwani wa kata ya Miono ,Juma Mpwimbwi alishukuru kupokea msaada huo na kusema Ridhiwani amekuwa na msaada mkubwa kwao kutafuta wadau ,ili kutatua baadhi ya kero . “Mungu akujaalie katika safari yako ya uongozi na naimani anaona unachofanya ndani ya uongozi wako na atakusaidia zaidi” alieleza Mpwimbwi.
Kiwanda cha KEDA,kipo eneo la Pingo ,kata ya Pera ,Chalinze,mkoa wa Pwani, ni moja ya kiwanda kikubwa nchini ambacho kinajishughulisha kutengeneza vigae vyenye viwango vya juu ,Afrika Mashariki na Kati
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇