Baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) mnamo Mei 8 2018, ilianza kutekeleza vikwazo vipya dhidi ya Iran. Vikwazo hivyo vya upande mmoja ni ukiukwaji wa wazi wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Pamoja na kuwa Marekani ilikuwa haina budi ila kuzingatia misamaha inayohusu ushirikiano wa nyuklia na Iran lakini sasa imefuta misamaha hiyo.
Kuhusiana na nukta hiyo, Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ametangaza kuwa, misamaha ya nyuklia inayohusiana na JCPOA imefutwa sambamba na kuwawekea vikwazo Wairani wawili wanaohusiana na mpango wa nyuklia. Katika ujumbe kupitia Twitter, Pompeo ameandika: "Ninahitimisha misamaha ya vikwazo ya miradi ya nyuklia inayohusiana na JCPOA nchini Iran na hilo litaanza kutekelezwa baada ya siku 60. Kuendelea kushadidi harakati za nyuklia za Iran kumelazimu ushirikiano huu usitishwe. Aidha katika ujumbe mwingine pia ameandika: "Tunawawekea vikwazo watu wawili wanaohusika katika kuongoza mpango wa uturubishaji madini ya urani nchini Iran ambao ni Majid Aghai na Amjad Sazgar. Wasomi wa Iran lazima wachague ima kufanya kazi zenye malengo ya amani au wakumbwe na hatari ya vikwazo."
Pompeo na Maseneta wa chama tawala cha Republican wakiongozwa na Seneta Tom Cotton wamekuwa wakitaka Iran iondolewe misamaha hiyo ya nyuklia na kufutwa sehemu zote zilizobakia za mapatano ya JCPOA ikiwa ni katika utekelezaji wa sera za mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran.
Misamaha hiyo ilikuwa inaruhusu mashirika ya Ulaya , China na Russia kushirikiana na Iran katika baadhi ya miradi yake ya nyuklia.
Idara ya Kudhibiti Mali za Kigeni katika Wizara ya Fedha ya Marekani nayo kupitia gazeti la Washington Post imeidhinisha kuondolewa misamaha hiyo ya nyuklia ya Iran. Nalo Shirika la Habari la Reuters limechapisha ripoti inayosema kuwa Marekani itaongeza kwa siku 90 muda wa misamaha ya ushirikiano na Kituo cha Umeme wa Nyuklia cha Bushehr. Ripoti hiyo imeongeza kuwa misamaha mingine iliyosalia ya ushirikiano wa Iran na mashirika ya Russia, China na Ulaya imefutwa.
Weledi wa mambo katika nchi za Magharibi wanaamini kuwa misamaha hiyo ilikuwa inaifanya Iran ipunguze motisha wa kuongeza kiwango cha urutubishaji urani na pia ilikuwa fursa ya kupata taarifa za kiintelijensia kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
Iran ina miradi ya pamoja ya nyuklia na baadhi ya nchi za kundi la 4+1 hasa Russia na China katika vituo vyake vya nyuklia.
Pamoja na kuwepo vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran baada ya Trump kutangaza kuiondoa nchi yake katika mapatano ya JCPOA, lakini bado Washington ililazimika kutotekeleza vikwazo katika baadhi ya sekta za ushirikiano wa nyuklia baina ya Iran na nchi za 4+1. Utawala wa Trump ulitekeleza misamaha hiyo sio kwa sababu ya kuwa na nia njema bali ulilazimika kufanya hiyo kwa sababu ushirikiano na Iran katika shughuli za nyuklia zenye malengo ya amani ni kati ya vipengee vya mapatano ya JCPOA.
Ni kwa msingi huo ndio serikali iliyopita ya Marekani ikalazimika kutekeleza misamaha katika baadhi ya vikwazo vilivyohusu uingizwaji Iran vifaa vya kutumiwa katika mpango wake wa nyuklia. Utawala wa Trump hata baada ya kujiondoa katika mapatano ya JCPOA mnamo Mei 2018 ulilazimika kutekeleza msamaha huo kwa nchi zingine zilizosalia katika mapatano ya JCPOA. Marekani ilitoa misamaha hiyo kwa dhana kuwa urutubishaji madini nchini Iran ungebakia katika kiwango cha chini. Pamoja na hayo, katikati ya mwaka 2019 Marekani ilioondoa baadhi ya misamaha ilikuyokuwa inahusu nchi wanachama wa JCPOA kununua maji mazito ya nyuklia kutoka Iran na pia urani ya Iran iliyorutubishwa kwa kiwango cha chini. Hatua hiyo ya Marekani ilikuwa ni ukiukwaji wa wazi wa mapatano ya JCPOA na azimio 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Marekani ilichukua hatua hiyo ili itumia ubabe katika kuzilazimisha nchi zingine zisishirikiane na Iran katika uga wa nyuklia.
Pamoja na hayo, Marekani imegonga mwamba katika sera zake za mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Iran. Hivi sasa utawala wa Trump unaonekana kukata tamaa na umeamua kuondoa misamaha michache iliyokuwa imebakia katika uga wa ushirikiano wa kinyuklia wa Iran na wanachama wa nchi za 4+1.
Brian Hook, mjumbe maalumu wa Marekani katika masuala ya Iran anasema stratijia ya Washington kuhusu Iran inahusu kuishinikiza kiuchumi, kuitenga kidiplomasia na kuizuia kijeshi.
Iran imesisitiza mara kadhaa kuwa, haitasalimu amri mbele ya mashinikizo na matakwa ya Marekani. Katika fremu ya matakwa ya utawala wa Kizayuni wa Israel, Marekani imekuwa ikipinga aina yoyote ya Iran kupata uwezo wa nyuklia hasa katika sekta ya urutubishaji urani. Pamoja hayo, Iran imekuwa ikitekeleza sera za 'mapambano ya juu kabisa' kukabiliana na sera za Marekani za 'mashinikizo ya juu kabisa.' Iran imepuuza mashinikizo ya Marekani na imekuwa ikiendelea kama akawaida na shughuli zake za nyuklia zenye malengo ya amani. Kwa hivyo iwapo nchi za kundi la 4+1 zitasitisha ushirikiano wa kinyuklia na Iran kutokana na mashinikizo ya Marekani, basi ifahamike kuwa, Iran itategemea uwezo wake wa ndani na wanasayansi wake katika kuendeleza miradi yake ya nyuklia.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇