Na Zainab Nyamka-Michuzi TV
IKIWA zimepita siku kadhaa toka itangazwe kwamba maambukizi ya virusi vya Corona nchini kupungua, tumeanza kushuhudia Watanzania waanza kuishi maisha yale yale...
Sijui ni nani ameturoga sisi watanzania, ina maana tumeshasahau? Au tunaendelea kuamini kuwa hautatupata tena?
Kauli ya Rais Dkt.John Magufuli iheshimiwe na kutekelezwa ila tusisahau wajibu wetu kama wananchi watiifu kwake. Ni sawa maambukizi ya Corona yameoungua lakini tuendelee kujikinga kwani ugonjwa upo ndani ya jamii yetu, hivyo tufuate maelekezo ya wataalamu wetu wa afya kama wanavyotuagiza.
Huko mitaani uvaaji wa barakoa, kutumia vitakasa mikono (sanitizer) , sabuni na maji ya kutiririka umepungua kwa kasi sana. Ina maana tumeshasahau ushauri wa wataalamu wa afya?Nauliza tu kwa nia njema.
Serikali kupitia kwa wataalamu wa afya wameendelea kutoa maelekezo kuwa wananchi waendelee kujikinga dhidi ya maambukizi ili kuepusha ongezeko la maambukizi mapya.Ipo nafasi ya kufuata maelekezo hayo kwa faida ya Watanzania wote.
Hata hivyo baada ya kupungua kwa maambukizi ya Corona na kuthibitishwa na Serikali kupitia Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ule utaratibu wa watanzania wakuvaa barakoa umetoweka ghafla, ununuaji wa vitakasa mikono umepungua na hata matumizi ya maji tiririka na sabuni umeanza nao kusahaulika.
Katika masoko, maeneo mbalimbali ya biashara, mitaani, kwenye vyombo vya usafiri ukikutana na mtu aliyevaa barakoa ni moja kati ya abiria 19.Yaani tunachukulia poa sana.
Tukumbushane elimu ambayo tumekuwa tukipatiwa na wataalam wa afya ya kujikinga na Corona imeishia wapi? Tumetakiwa kuishi na Corona kwa njia zinazostahili lakini sio kuishi nae kwa njia isiyo sahihi.
Wote kwa pamoja tukubaliane tunapovaa barakoa uwezekano wa kupunguza maambukizi ni mkubwa sana, kutokuruhusu maambukizi kwenda kwa mtu mwingine au kutoka kwa mtu mwingine, tunapopaka Vitakasa mikono lengo ni kuua virusi vya Corona vinavyoishi katika Viganja vyetu vya mikono kutoka katika sehemu iliyotayari na virusi hivyo.
Nikumbushe tu siku za karibuni Rais wa Chama cha Madaktari (MAT) Dk.Elisha Osati alizungumza kwa uwazi kabisa kuwa watanzania wanatakiwa waendelee kujikinga kwa njia zile zile tulizotumia wakati maaambukizi yalivyoshika kasi.
Akasisitiza kwa watanzania kuchukua tahadhari kuepusha maambukizi mapya katika kipindi hiki na wasikubali kabisa ali kirusi Corona kiwashinde.
Dk.Osati ameleeza ya kuwa asilimia kubwa ya sampuli wanazozipima kwa sasa hazina maambukizi chini ya asilimia 10 tofauti na awali cha Aprili ilikuwa imefikia kwa aslimia 90 kwa sampuli zote walizokuwa wanapima.
Hata hivyo binafsi katika pita pita zangu, nimeshuhuhudia wananchi wakiendelea na shughuli zao kama kawaida bila kujikinga na mahala kwingine yale madumu na matanki yakiwa hayana maji wala sabuni za kunawia na maji muda mwingine yakiwa hayana dawa yoyote.
Kama nilivyosema hapo awali na naomba kurudia wananchi hawana barakoa, kwenye daladala wamekaa karibu bila kujali na kusahau kama kuna adui mkubwa anayeiangamiza dunia mgonjwa mwenye maambukizi huwezi kumjua
Lazima tujitafakari, je tunahitaji kuishi na Corona kwa namna gani ili tuendelee na maisha yetu ya kila? Tuna la kujifunza kutoka kwenye mataifa mengine yaliyopata maambukizi makubwa ili na sisi tusifikie huko.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeendelea kusisitiza kuwa kinga ya ugonjwa wa Covid 19 itachukua muda mrefu kupatikana kitu kinachopelekea tuendelee kuishi nao.
Watanzania tufanye kazi ila tuendelee kuchukua tahadhari zaidi kuepuka ongezeko la wagonjwa wa Corona, tufurahie maisha.
Rais Dkt John Pombe Magufuli.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇