LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

May 24, 2020

IDADI YA WAGONJWA WA CORONA YAZIDI KUPUNGUA NCHINI, YASISITIZWA TAHADHARI IENDELEE KUCHUKULIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia baada ya Swala ya Eid el Fitr, katika Msikiti wa Gaddaff, Jijini Dodoma, leo Mei 24, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

DODOMA, Tanzania
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema idadi ya wagonjwa wa Corona imeendelea kupungua huku baadhi ya vituo vikiwa havina wagonjwa na kwamba kwa mujibu wa takwimu za leo asubuhi Dar es Salaam kuna wagonjwa 11, Kibaha 16 na Dodoma kituo cha Mkonze wagonjwa ni watatu.

Akizungumza mara baada ya sala ya Idd El Fitr katika Msikiti wa Gaddaff jijini Dodoma, Waziri Mkuu amesema, licha ya wagonjwa kupungua bado hatua za kujikinga zinapaswa kuchukuliwa ili ugonjwa uendelee kupungu.

Amesema, takwimu kuonyesha maambukizi kushuka ni nzuri lakini jambo kubwa kwa sasa ni kuendelea kuchukua tahadhari ili kuzuia uwezekano wa mtu kuambukiza na kuambukizwa huku akiwataka wananchi kuendelee kuchukua tahadhari zote zinazotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Wataalam wa Afya.

“Naomba tuendelee kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni na njia zote zinazozuia maambukizi kutoka mtu mmoja hadi mwingine” amesema Majaliwa.

Hata hivyo amewataka wananchi kuutumia uhuru wa kufanya shughuli zao zote bila kuvuka mipaka na kumtaka kila Mtanzania kwa dini yake kumwomba Mwenyezi Mungu atuepushe na janga la Corona kama alivyoagiza Rais Dk. John Magufuli.

Akizungumza kuhusu amani, Majaliwa amesema, wananchi waendelee kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu ili kuidumisha amani iliyopo nchini na kuendelea kuifanya Tanzania kuwa ni kisiwa cha amani na mataifa mengi kuifanya kuwa kimbilio.

“Tanzania imekuwa mfano kwa nchi nyingine zinazotamani tunu hiyo na kuifanya nchi yetu kuwa kimbilio, tuendelee kuienzi ili iendelee kudumu” amesisitiza Waziri Majaliwa.

Awali, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rajab Mustapha amewaasa waumini wa madhehebu mbalimbali na wananchi kwa ujumla kuacha kufanya machukizo mbele za Mwenyezi Mungu ili atuepushe na majanga mbalimbali likiwemo la Corona.

“Tumeomba dua kwa Mwenyezi Mungu tumeitikiwa, tusirejee kumuasi, watu wasifanye mabalaa, wasishabikie kwa kufungua baa, ulevi, kwani Mungu atarudisha janga kuliko lilivyokuwa awali” amesema Sheikh Mustapha na kuongeza;

“Tuwe wenye kushukuru na siyo kukufuru rehema na Mungu, tuendelee kumwomba ili atokomeza kabisa janga hili la Corona na kumuelekea Mungu kwani Corona haitachukua muda wala haitapata nafasi nchini lakini kubwa ni kuendelea kuchukua tahadharai za wataalamu wa afya,” amesema Sheikh Mustapha.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages