Na Richard Mwaikenda
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imenunua vifaa
kinga kujihadhari na Corona wakati wa
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Pili na uwekaji wazi
Daftari unaotarajiwa kuanza Aprili 17 mwaka huu.
Taarifa hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji
mstaafu Semistocles Kaijage wakati wa mkutano na viongozi wa vyama vya siasa
kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam hivi
karibuni.
"Baada ya mashauriano na wadau wakuu, Tume imeona vyema kuendelea
na mazoezi hayo mawili kwa kuzingatia tahadhari
za kiafya kama inavyoshauriwa na Wataalam wa masuala hayo. Tayari Tume
imenunua vifaa kinga vinavyotakiwa kwa
ajili ya kuchukua tahadhari za maambukizi ya ugonjwa wa COVID – 19
unaosababishwa na virusi vya Corona na tayari imetoa maelekezo kwa watendaji wa
Uboreshaji kuzingatia miongozo ya afya," amesema Jaji mstaafu Kaijage.
Amesema kuwa, uwekaji wazi wa Daftari la
Awali utafanyika sambamba na Uboreshaji
wa Daftari Awamu ya Pili. Matukio hayo yataanza rasmi tarehe 17 Aprili, 2020
na kukamilika tarehe 04 Mei, 2020 kwa Nchi nzima.
Shughuli za Uwekaji wazi wa
Daftari la Awali na Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura zitafanyika
kwa siku tatu (3) tu kwenye kila Mkoa na katika route mbili
badala ya route tatu zilizopangwa hapo awali na yatazingatia,
wakati wote, tahadhari zinazoshauriwa na Serikali na Wataalam wa afya.
Katika Route ya kwanza matukio haya yatafanyika kuanzia tarehe 17
Aprili hadi tarehe 19 Aprili,
2020. Jumla ya mikoa 12 na vituo
vya uandikishaji Elfu mbili na tano (2005) vitahusika.
Katika Route hii ya kwanza, Mikoa
itakayohusika ni:- Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Mara, Simiyu na
Mwanza. Mikoa mingine ni; Shinyanga, Geita, Kagera, Kigoma na
Tabora.
Kwa upande wa Route ya pili mazoezi haya yatafanyika kuanzia tarehe 02
Mei, hadi 04 Mei 2020. Maeneo
yanayohusika ni Tanzania Zanzibar na mikoa 14 ya Tanzania Bara ambapo
vituo vya kuandikisha wapiga kura vipatavyo Elfu mbili na moja (2001)
vitahusika.
Mikoa ya Tanzania Bara itakayofikiwa
kwenye route ya pili ni Katavi, Rukwa, Singida, Dodoma, Iringa, Songwe,
Njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.
Jumla ya vituo vya kuandikisha Wapiga Kura
vitakavyotumika katika Awamu hii ni Elfu nne na sita (4006),
badala ya vile Elfu nane na thelathini na moja (8031) tulivyowaeleza
hapo awali. Kati ya hivyo, vituo Elfu tatu, mia tisa hamsini na sita (3,956)
vitakuwa Tanzania Bara na vituo Hamsini
(50) vitakuwa Tanzania Zanzibar. Tume iliwakabidhi viongozi wa vyama vya
siasa, orodha mpya ya vituo hivyo.
Uboreshaji huu utafanyika katika kila Kata
ambapo kutakuwa na Mwandishi Msaidizi na
BVR Kit Operator ambao watakuwa na orodha ya vituo vyote katika Kata
husika. Watendaji hawa watakuwa na uwezo
wa kuboresha taarifa za Mpiga Kura
yeyote atakayefika kituoni.
Aidha, Mpiga Kura atakayefika kituoni ataandikishwa
kulingana na kituo atakachopigia kura siku ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ndani ya Kata husika.
Kwa
upande wa uwekaji wazi wa Daftari la Awali, Orodha ya wapiga kura itabandikwa
katika kila kituo kilichotumika kuandikisha Wapiga Kura Awamu ya Kwanza.
Mpiga Kura ambaye
atakuwa amehakiki taarifa zake na kuhitaji kufanyiwa marekebisho ama Mpiga Kura
anayehitaji kumwekea pingamizi Mpiga Kura mwingine, atatakiwa kwenda kwenye
kituo cha Kata husika kilichopangwa.
Uwekaji wazi daftari utawahusu Wapiga Kura
wote, wakiwemo wale walioandikishwa mwaka 2015 na wale walioandikishwa katika
awamu ya kwanza ya Uboreshaji.
Aidha, utaratibu wa kuweka pingamizi kwa
aliyeandikishwa utafanyika kwa mujibu wa Kifungu cha 24 (1) cha Sheria ya Taifa
ya Uchaguzi na kifungu cha 30(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za
Mitaa.
Mtu yeyote ambaye jina lake lipo kwenye
Daftari la Awali la Mpiga Kura anaweza kuweka pingamizi dhidi ya kuendelea
kuwepo kwa jina lake mwenyewe au jina la mtu mwingine yeyote iwapo mtu huyo
atakuwa amepoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari au amefariki.
Vilevile, pingamizi
la Uandikishwaji linaweza pia kuwekwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Afisa
Mwandikishaji au Afisa Mwandikishaji Msaidizi.
Mpiga Kura anayetaka
kuweka pingamizi atatakiwa kufika kituoni na kujaza fomu maalum ambayo
inafahamika kama Fomu Na. 3B ambayo, pamoja na mambo mengine, itamtaka atoe
sababu za kuweka pingamizi hilo.
Mweka Pingamizi
anatakiwa kuwasilisha pingamizi ndani ya siku saba (7) kuanzia siku ya mwisho
ya Uwekaji Wazi wa Daftari la Awali katika eneo husika. Pingamizi hilo
litafanyiwa kazi na Afisa Mwandikishaji au Afisa Mwandikishaji Msaidizi ndani
ya siku saba (7) na kisha kutolewa uamuzi.
Uamuzi huo unaweza
kukatiwa Rufaa katika Mahakama ya Wilaya na Mahakama hiyo inatakiwa kutoa
uamuzi ndani ya siku 14 tangu tarehe ya Rufaa kupokelewa Mahakamani. Uamuzi wa
mahakama hiyo ni wa mwisho.
Uwekaji wazi wa
Daftari kama ilivyo kwa Uboreshaji wa Daftari utazingatia Sheria za Uchaguzi na
Kanuni zilizotungwa chini ya Sheria hizo.
Njia zitakazo tumika katika
uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura kama ifuatavyo:-
Kwanza, ni kwa Wapiga Kura
wenyewe kufika katika vituo walivyojiandikisha na kuhakiki taarifa zao katika
orodha itakayokuwa imebandikwa katika vituo hivyo.
Pili, ni kwa kutumia Mfumo wa Voters’
Interaction Systems (VIS), ambapo
Mpiga kura kupitia simu yake ya kiganjani atapiga namba *152*00# na kufuata maelekezo yatakayo mwezesha
kuhakiki taarifa zake. Huduma hii ni ya
bure.
Vilevile, kwa kupitia Tovuti ya
Tume (www.nec.go.tz), Mpiga kura atahakiki
taarifa zake katika sehemu iliyoandikwa “uhakiki” na kuendelea kufuata
maelekezo.
Tatu, ni kupitia kituo cha Huduma kwa Wapiga Kura (Call
centre) ambapo wananchi watapiga simu bure kupitia namba ya simu ya kituo
ambayo ni 0800782100 na kupata usaidizi katika kuhakiki taarifa zao.
Tume imeweka njia zote hizo ili kuwapa
urahisi Wapiga Kura wote kuhakiki taarifa zao.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇