HOTUBA YA MWENYEKITI WA TUME YA TAIFA YA
UCHAGUZI
MHE. JAJI
WA RUFAA (MST.) SEMISTOCLES KAIJAGE (PICHANI) KWENYE MKUTANO WA TUME NA VYAMA VYA SIASA KATIKA
UKUMBI WA MIKUTANO WA MWL. NYERERE,
TAREHE
8 APRILI, 2020
•
Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi,
•
Waheshimiwa Wajumbe wa Tume,
•
Mkurugenzi wa Uchaguzi,
•
Msajili wa Vyama vya Siasa,
•
Viongozi wa Vyama vya Siasa,
•
Mwakilishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu,
•
Inspekta Jenerali wa Polisi,
•
Kamishna Mkuu wa Uhamiaji
•
Watendaji wa Tume,
•
Waandishi wa Habari,
Bwana Asifiwe!!!, Tumsifu Yesu Kristu!!!, Assalam Aleykum!!!.
Kwa niaba ya Tume ya Taifa ya
Uchaguzi, napenda kutumia fursa hii, kuwakaribisha katika mkutano huu muhimu
ambao madhumuni yake ni kupeana mrejesho
wa yale tuliyojadiliana katika mkutano wetu wa terehe 23 Machi, 2020.
Mkutano huo ulihusu utekelezaji wa
mazoezi ya uwekaji wazi wa Daftari la Awali na Uboreshaji wa
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Pili.
Napenda pia kuwashukuru kwa mwitikio wenu wa kuhudhuria katika mkutano huu, licha ya majukumu mengi mliyonayo. Uwepo
wenu ni muhimu na Tume inauthamini sana.
Ndugu Viongozi wa Vyama vya
Siasa,
Kama nilivyotangulia kusema mkutano huu umelenga zaidi katika kuleta
mrejesho wa yale yaliyojadiliwa katika mkutano uliopita. Mtakumbuka katika
mkutano ule, Tume iliahidi kuyafanyia kazi maoni na mapendekezo yenu kwa kukutana na kushauriana
na wadau wengine na pia kuwapa taarifa juu ya mabadiliko yoyote yatakayoweza
kutokea kabla ya Uboreshaji wa Daftari wa Awamu ya Pili.
Ndugu Viongozi wa Vyama vya
Siasa
Baada ya mashauriano na wadau wakuu, Tume imeona vyema kuendelea na
mazoezi hayo mawili kwa kuzingatia tahadhari za kiafya kama inavyoshauriwa na Wataalam wa masuala
hayo.
Tayari Tume imenunua vifaa kinga vinavyotakiwa kwa ajili ya kuchukua tahadhari za maambukizi
ya ugonjwa wa COVID – 19 unaosababishwa na virusi vya Corona na tayari imetoa
maelekezo kwa watendaji wa Uboreshaji kuzingatia miongozo ya afya.
Ndugu Viongozi wa Vyama vya
Siasa,
Kama tulivyowataarifu katika
Mkutano wetu uliopita, uwekaji wazi wa Daftari la Awali utafanyika sambamba na Uboreshaji wa Daftari Awamu ya Pili. Napenda kuwafahamisha kwamba, mazoezi hayo kama
nilivyowataarifu kwenye mkutano uliopita, yataanza rasmi tarehe 17 Aprili, 2020. Kwa
mujibu wa ratiba mtakayopewa, mazoezi hayo yatakamilika tarehe 04 Mei, 2020 kwa
Nchi nzima.
Ndugu Viongozi wa Vyama vya
Siasa,
Mazoezi ya Uwekaji
wazi wa Daftari la Awali na Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
yatafanyika kwa siku tatu (3) tu kwenye kila Mkoa na katika route
mbili badala ya route tatu zilizopangwa hapo awali
na yatazingatia, wakati wote, tahadhari zinazoshauriwa na Serikali na Wataalam
wa afya.
Katika Route ya kwanza mazoezi haya yatafanyika kuanzia tarehe 17 Aprili hadi tarehe 19 Aprili, 2020. Jumla ya
mikoa 12 na vituo vya uandikishaji Elfu mbili na tano (2005) vitahusika. Katika Route hii ya kwanza, Mikoa
itakayohusika ni:- Arusha, Kilimanjaro,
Manyara, Tanga, Mara, Simiyu na
Mwanza. Mikoa mingine ni; Shinyanga, Geita, Kagera, Kigoma na Tabora.
Kwa upande wa Route
ya pili mazoezi haya yatafanyika
kuanzia tarehe 02 Mei, hadi 04 Mei 2020. Maeneo yanayohusika ni Tanzania Zanzibar na mikoa 14 ya Tanzania Bara ambapo vituo vya
kuandikisha wapiga kura vipatavyo Elfu
mbili na moja (2001) vitahusika.
Mikoa ya Tanzania Bara itakayofikiwa kwenye route ya pili ni Katavi, Rukwa, Singida, Dodoma, Iringa,
Songwe, Njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.
Jumla ya vituo vya kuandikisha
Wapiga Kura vitakavyotumika katika Awamu hii ni Elfu nne na sita (4006),
badala ya vile Elfu nane na thelathini
na moja (8031) tulivyowaeleza hapo awali. Kati ya hivyo, vituo Elfu tatu, mia tisa hamsini na sita (3,956)
vitakuwa Tanzania Bara na vituo Hamsini (50) vitakuwa Tanzania Zanzibar.
Leo, Tume itawakabidhi orodha mpya ya vituo hivyo. Orodha ya vituo vya uandikishaji mliyogawiwa
kwenye Mkutano wetu wa tarehe 23/03/2020 haitatumika.
Ndugu Viongozi wa Vyama vya
Siasa
Uboreshaji huu utafanyika
katika kila Kata ambapo kutakuwa na
Mwandishi Msaidizi na BVR Kit
Operator ambao watakuwa na orodha ya vituo vyote katika Kata husika. Watendaji hawa watakuwa na uwezo wa kuboresha taarifa za Mpiga Kura yeyote atakayefika kituoni. Aidha, Mpiga Kura atakayefika kituoni
ataandikishwa kulingana na kituo atakachopigia kura siku ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ndani ya Kata husika.
Ndugu Viongozi wa Vyama vya
Siasa,
Kwa upande wa uwekaji wazi wa Daftari la Awali, Orodha
ya wapiga kura itabandikwa katika kila kituo kilichotumika kuandikisha Wapiga Kura
Awamu ya Kwanza.
Mpiga
Kura ambaye atakuwa amehakiki taarifa zake na kuhitaji kufanyiwa marekebisho
ama Mpiga Kura anayehitaji kumwekea pingamizi Mpiga Kura mwingine, atatakiwa
kwenda kwenye kituo cha Kata husika kilichopangwa.
Zoezi hili la uwekaji wazi
daftari litawahusu Wapiga Kura wote, wakiwemo wale walioandikishwa mwaka 2015
na wale walioandikishwa katika awamu ya kwanza ya Uboreshaji.
Aidha, utaratibu wa kuweka pingamizi kwa
aliyeandikishwa utafanyika kwa mujibu wa Kifungu cha 24 (1) cha Sheria ya Taifa
ya Uchaguzi na kifungu cha 30(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa. Mtu yeyote ambaye jina lake lipo kwenye
Daftari la Awali la Mpiga Kura anaweza kuweka pingamizi dhidi ya kuendelea
kuwepo kwa jina lake mwenyewe au jina la mtu mwingine yeyote iwapo mtu huyo
atakuwa amepoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari au amefariki.
Vilevile,
pingamizi la Uandikishwaji linaweza pia kuwekwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi,
Afisa Mwandikishaji au Afisa Mwandikishaji Msaidizi.
Ndugu Viongozi wa Vyama vya
Siasa,
Mpiga
Kura anayetaka kuweka pingamizi atatakiwa kufika kituoni na kujaza fomu maalum
ambayo inafahamika kama Fomu Na. 3B ambayo, pamoja na mambo mengine, itamtaka
atoe sababu za kuweka pingamizi hilo.
Mweka
Pingamizi anatakiwa kuwasilisha pingamizi ndani ya siku saba (7) kuanzia siku
ya mwisho ya Uwekaji Wazi wa Daftari la Awali katika eneo husika. Pingamizi
hilo litafanyiwa kazi na Afisa Mwandikishaji au Afisa Mwandikishaji Msaidizi
ndani ya siku saba (7) na kisha kutolewa uamuzi.
Uamuzi
huo unaweza kukatiwa Rufaa katika Mahakama ya Wilaya na Mahakama hiyo inatakiwa
kutoa uamuzi ndani ya siku 14 tangu tarehe ya Rufaa kupokelewa Mahakamani.
Uamuzi wa mahakama hiyo ni wa mwisho.
Kimsingi,
uwekaji wazi wa Daftari kama ilivyo kwa Uboreshaji wa Daftari utazingatia
Sheria za Uchaguzi na Kanuni zilizotungwa chini ya Sheria hizo.
Ndugu Viongozi wa Vyama vya
Siasa,
Napenda kutumia
nafasi hii kuwakumbusha tena njia zitakazo tumika katika uhakiki wa taarifa za
Wapiga Kura kama ifuatavyo:-
Kwanza, ni kwa Wapiga
Kura wenyewe kufika katika vituo walivyojiandikisha na kuhakiki taarifa zao
katika orodha itakayokuwa imebandikwa katika vituo hivyo.
Pili, ni kwa kutumia Mfumo wa Voters’ Interaction Systems (VIS),
ambapo Mpiga kura kupitia simu yake ya kiganjani atapiga namba *152*00# na
kufuata maelekezo yatakayo mwezesha kuhakiki taarifa zake. Huduma hii ni ya bure.
Vilevile, kwa
kupitia Tovuti ya Tume (www.nec.go.tz), Mpiga kura
atahakiki taarifa zake katika sehemu iliyoandikwa “uhakiki” na kuendelea
kufuata maelekezo.
Tatu, ni kupitia kituo cha Huduma kwa Wapiga Kura (Call centre) ambapo wananchi watapiga
simu bure kupitia namba ya simu ya kituo ambayo ni 0800782100 na kupata usaidizi katika kuhakiki taarifa zao.
Tume imeweka njia zote hizo ili kuwapa urahisi Wapiga
Kura wote kuhakiki taarifa zao.
Ndugu Viongozi wa Vyama vya
Siasa
Kama mnavyofahamu, Tume
hutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba, Sheria, Kanuni na Taratibu. Nitoe
rai kwenu viongozi wa Vyama vya Siasa
kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni na Taratibu za Uboreshaji na Uwekaji wazi wa
Daftari la Awali.
Nawasisitiza wananchi waliojiandikisha kwenye Daftari la Wapiga
Kura mwaka 2015 na wale waliojiandikisha katika Uboreshaji wa Daftari Awamu ya
Kwanza kujitokeza kwa wingi kuhakiki taarifa zao pindi Daftari litakapowekwa wazi katika maeneo yao na watumie njia
nyingine za uhakiki zilizoelezwa hapo juu. Pia watumie nafasi hiyo kuwawekea
pingamizi wananchi wasio na sifa za kuwemo kwenye Daftari la Wapiga Kura.
Aidha, niwaombe wananchi hususan
wale wenye sifa ya kujiandikisha kama Wapiga Kura wapya wasisubiri kujitokeza
siku ya mwisho ya zoezi, na hivyo
kusababisha msongamano, bali wafike vituoni mara tu zoezi litakapowafikia; na
watunze kadi zao.
Vilevile, ni muhimu kwa
wananchi kuendelea kuzingatia tahadhari za kiafya zilizowekwa katika vituo vya
kuandikisha wapiga kura ili kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa COVID - 19
katika kipindi chote cha zoezi hili muhimu.
Ndugu Viongozi wa Vyama vya
Siasa
Katika kuhitimisha,
napenda kuwashukuru tena kwa kuitikia
wito wetu na kuhudhuria mkutano huu; na zaidi kwa ushirikiano wenu wa siku
zote.
Baada ya kusema
maneno hayo, sasa naomba kutamka kwamba mkutano wetu umefunguliwa rasmi.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇