Mchekeshaji
Emmanuel Mgaya 'Masanja' (kulia) akizungumza na wandishi wa habari
baada ya kumaliza kuhojiwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi
(kushoto) mchana wa leo.
Mkuu
wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi akizungumza na wandishi wa habari
baada ya kumaliza kumhoji Masanja baada ya jana kuagiza kuripoti
ofisini kwake.
Charles James, Michuzi TV
YAMEISHA!
Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas
Katambi kumsamehe mchekeshaji Emmanuel Mgaya 'Masanja' baada ya kuitikia
wito wake alioutoa jana.
DC
Katambi alimpa Masanja siku tatu kuripoti ofisini kwake ili kuhojiwa na
kueleza sababu ya yeye kurikodi kipindi chake akiwahoji wananchi wa
Dodoma maana ya Covid19 jambo ambalo kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya
lililenga kupotosha kwamba wananchi wake hawana uelewa na ugonjwa huo.
Kufuatia
wito huo jana hiyo hiyo Masanha aliripoti ofisi ya DC na kuelekezwa
kuja leo ambapo ameripoti na kuhojiwa na Kamati ya Usalama ya Wilaya
hiyo aliomba msamaha na kuahidi kutumia nafasi yake kushirikiana na
serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo wa Corona.
Akizungumza
na wandishi wa habari baada ya kumaliza mahojiano, Masanja amempongeza
DC Katambi kwa kuwa mwepesi wa kugundua kuwa kulikua na shida kwenye
kipindi chake alichorusha jambo linaonesha kweli yeye ni kijana na
anaenda na spidi ya Rais Magufuli katika kuwatumikia watanzania.
"
Niombe radhi kwa kueleweka vibaya lengo la kipindi chetu lilikua
kuelimisha na siyo kuleta mzaha, namshukuru Mkuu kwa wito wake huu ambao
umenisaidia pia kwa namna moja ama nyingine kujua wapi nilipoteleza.
Kama
Taifa tunapita kwenye kipindi kigumu kutokana na maambukizi ya ugonjwa
huu hivyo tuendelee kuchukua tahadhari zote kama tunavyoelekezwa na
wataalamu wetu ili tuzidi kuwa salama," Amesema Masanja.
Mchekeshaji
huyo ambaye pia ni Mchungaji amemuahidi DC Katambi kuwa atatumia kipawa
chake cha kuhubiri pia kuhamasisha watanzania kutumia vitakasa mikono
na kufuata masharti yote ambayo yanatolewa na viongozi.
Nae
DC Katambi amesema hana tatizo binafsi na Masanja wala kituo cha DW
ambacho muigizaji huyo anafanyia kazi bali walimuita kwa ajili ya
kuwekana sawa.
"
Sisi hatuna tatizo binafsi, ukiangalia kipindi kile maudhui yake ni
kama kuonesha kwamba watanzania wote na hasa wanadodoma hatuna uelewa na
virusi hivi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona.
Kitendo
cha kuweka watu wote waliokosea kujua maana ya covid19 ni kuuaminisha
umma kwamba Tanzania siyo mahali sahihi kwa kwa kipindi hiki maana
wananchi wake hawajui hata maana ya ugonjwa huu, kumbe ni njia
zilizotumika ndizo hazikua sawa, hivyo tumemhoji Masanja na baada ya
kuelewa na kuomba radhi tumemsamehe," Amesema Katambi.
Amesema
serikali imeendelea kuchukua hatua zote za kuhakikisha zinakabiliana na
maambukizi ya ugonjwa huo na kuwataka watanzania kuendelea kuchukua
tahadhari na kumuomba Mungu kama ambavyo Rais Magufuli alielekeza.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇