By MZEE WA ATIKALI ✍️✍️✍️
1. USULI:
Jumanne ya leo, tarehe 7.4.2020, imetimia miaka 48 toka aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar, ndugu SHEIKH ABEID AMANI KARUME, alipouawa kwa kumiminiwa risasi nane na Luteni HOMOUD MOHAMMED BARWAN katika Afisi Kuu ya Afro Shiraz Party, Kisiwandui, Zanzibar.
Kwa mujibu wa "The Public Holidays Act, Cap. 35 (RE 2002)", sikukuu za kitaifa nchini ziko 17 na mojawapo ya sikukuu hizo ni "KARUME DAY". Hivyo, leo ni siku ya mapumziko.
Je, Mwanamapinduzi huyu alizaliwa lini na wapi, aliuawa vipi, na kwanini tunamuenzi?.
Twende pamoja.............
2. KARUME Azaliwa Zanzibar
KARUME alizaliwa tarehe 4.8.1905 katika kitongoji cha Pongwe, Mwera, Wilaya ya Magharibi A, Zanzibar.
3. Asili ya Ukoo wa KARUME
Bw. AMANI ABEID KARUME, baba yake KARUME, alikuwa ni muhamiaji aliyehamia Zanzibar, miaka mingi iliyopita, akitokea kwao Malawi.
Aidha, Bi AMINA KADIR @ AMINA KIDUTU, mama yake KARUME, alikuwa ni mtumwa aliyetokea Ruanda-Urundi, ambapo alitekwa akiwa na miaka 10 tu na alifika Zanzibar kwa kupitia Bwagamoyo. Bw. AMANI na Bi KIDUTU wakaja kuoana na wakajaliwa kupata watoto watano, mmojawapo akiwa ABEID AMANI KARUME ambaye alikuwa ndiye wa kwanza kuzaliwa.
4. KARUME Afiwa na Baba Yake
Mwaka 1909, KARUME, akiwa na miaka 4 tu, alifiwa na baba yake.
5. KARUME Aanza Shule
Mwaka huohuo wa 1909, KARUME alianza masomo kwenye shule ya msingi, Mwera. Mwaka 1913, Bi AMINA, mama yake, alimchukua na kumpeleka Unguja kuendelea na masomo hadi alipomaliza darasa la saba.
6. KARUME Aanza Kazi ya Ubaharia
Miaka hiyo, bandari ya Zanzibar ilikuwa ndio kitovu cha biashara ambapo meli nyingi za mataifa mbalimbali zilitia nanga bandarini hapo. KARUME, baada ya kumaliza shule, alivutiwa na kazi ya ubaharia na akajifunza kazi hiyo na kufanikiwa kuajiriwa kwenye kampuni ya "Golden Crown" na kuweza kusafiri nchi mbalimbali.
7. KARUME Afunga Ndoa ya Kwanza
Mwanzoni mwa miaka ya 1940, KARUME alifunga ndoa yake ya kwanza na Bi PILI AHMED AMBARI.
8. KARUME Afunga Ndoa ya Pili
KARUME alifunga ndoa ya pili na Bi ASHURA MAISARA.
9. KARUME Aachana na Wake Zake
KARUME aliachana na wake zake wote wawili yaani Bi PILI na Bi ASHURA, kutokana na matatizo mbalimbali.
Pamoja na mambo mengine, KARUME hakujaaliwa kupata watoto na wake zake hao.
10. KARUME Amuoa Bi FATMA
Baada ya kuwa ameachana na wale wake zake wawili wa mwanzo, KARUME alimuoa Bi FATMA GULAMHUSSEIN ISMAIL (Mama FATMA KARUME).
Harusi yao, iliyofana, ilifanyika Bumbwini Misufini huku makazi yao yakiwa mtaa wa Kisimajongoo, nyumba na. 18/22, Unguja.
Bi FATMA alizaliwa mwaka 1929 katika familia ya GULAMHUSSEIN ISMAIL na Bi MWANAISHA RAMADHANI. Kuhusu ndoa yao hiyo, Bi FATMA anadadavua-:
"Mzee Karume aliishaoa kabla ya kunioa mie, lakini hakupata watoto. Nilipoolewa mimi hakuwa na mke, hivyo mimi sikuwa mke mwenza".
11. Bw. & Bi KARUME Wapata Watoto
Mwenyezi Mungu aliwajaalia Bw. & Bi KARUME watoto wawili. Watoto hao ni AMANI, aliyezaliwa tarehe 1.11.1948, na ALI, aliyezaliwa tarehe 24.5.1950.
12. KARUME Awa Kiongozi Mpigania Haki
KARUME alipendwa na Vijana na wazee kutokana na ushupavu wake na uwezo wake wa kujenga hoja. Hivyo, alichaguliwa kuwa Kiongozi:
12.1 KARUME Awa KATIBU MKUU wa AA
Mwaka 1942, KARUME alisimikwa kuwa Katibu Mkuu wa chama cha "African Association" na mwaka 1953 akawa Rais wa chama hicho.
12.2 KARUME Awa Rais wa ASP
Tarehe 5.2.1957, KARUME alisimikwa kuwa Rais wa Afro Shiraz Party ambacho kilikuwa mstari wa mbele kupigania haki za wananchi.
13. KARUME Awa Rais Zanzibar
Tarehe 12.1.1964, KARUME alisimikwa kuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar kufuatia mapinduzi mujarab yaliyofanywa na wanamapinduzi mahiri yaliyomwondoa Sultani.
16. Rais KARUME Awa Makamu wa Rais TZ
Tarehe 26.4.1964, baada ya Tanganyika na Zanzibar kungana, Rais KARUME aliapishwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa nchi yetu.
17. Rais KARUME Aongeza Wake 3
Baada ya Uhuru na Muungano, Rais KARUME alioa wake wengine watatu; Bi NASRA, Bi HELEMU na Bi FADYA ambapo kila mmoja alizaa nae mtoto mmoja wa kike, kama Mama FATMA anavyotiririka-
"Baada ya kuwa Rais, Mzee KARUME alioa wake wengine. Wakati ule ziliingia ndoa sijui zinaitwaje!. Viongozi wengi walioa, na yeye Mzee KARUME alioa na akapata watoto wengine watatu".
18. Rais KARUME Mwanamaendeleo
Kazi ya ubaharia iliyopelekea asafiri mataifa mengi, ilimpanua mawazo na kumfanya Rais KARUME kuwa mtu wa maendeleo sana.
Ndani ya miaka nane tu tayari aliishaleta maendeleo makubwa kisiwani Zanzibar ambapo aliishajenga maghorofa, mabarabara, vituo vya afya, alinunua meli, alianzisha televisheni, aliwagawia heka 3 za ardhi wananchi wonyonge wote kwani kabla ya uhuru ardhi kubwa ilikuwa ni ya Wahindi na Waarabu tu.
19. Rais KARUME Alipenda Kucheza DHUMNA
Muda wa jioni, Rais KARUME alipenda kwenda Afisi Kuu ya ASP, Kisiwandui kucheza dhumna na makomredi wenzie kama vile MZEE THABIT KOMBO, SHAHA KOMBO, IBRAHIM SADALA na MTORO REHANI KINGO.
Saa 11 jioni ya tarehe 7.4.1972, Rais KARUME, kama kawaida yake, alienda kucheza dhumna ambapo aliingia ndani na walinzi wake wakabaki nje na kuwakuwa macomredi wenzake na wakaanza kucheza.
20. Rais KARUME Alikuwa Bingwa wa Dhumna
Rais KARUME alikuwa hodari sana wa kucheza dhumna. Siku hiyo, aliishamshinda SHAHA KOMBO na akamwambia MTORO REHANI ajitayarishe.
21. Rais KARUME Avamiwa na Kumiminiwa shaba!!!
Ilipofika saa 12.05 magharibi, kijana mmoja alishuka kwenye gari kisha, kwa kasi na bila kuonekana, alienda chumba alimokuwa Rais KARUME na wenzake, na akiwa kwa nje akapiga goti kisha akamlenga na kummiminia risasi Rais KARUME na risasi zingine zikapiga ukutani!.
22. Mlinzi wa Rais KARUME Amtwanga Risasi Muuaji
Kijana huyo alipomaliza kutekeleza uovu huo, akaanza kutimua mbio kutoka nje. Mlinzi mmoja wa Rais KARUME aliyekuwa ameskia milio ya risasi, alikimbilia ndani na kumtwanga risasi kijana huyo ambaye alifariki hapohapo. Kijana huyo alikuja kutambuliwa kuwa ni Luteni HOMOUD MOHAMMED BARWAN.
23. Rais KARUME Akimbizwa Hospitali
Rais KARUME alikimbizwa, mara moja, hospitali ya Mapinduzi ambako Daktari alieleza kwamba amefariki kutokana na risasi zilizompiga shingoni na kifuani.
24. Mama KARUME "Achanganyikiwa"!
24.1 Mama KARUME Asikia Tetesi
Mama KARUME alikuwa ametoka shamba na hakujua kilichojiri, kama anavyoelezea-:
"Nikiwa nyumbani akaja mdogo wangu, ALI DAUDI, akaniambia huko nje kubaya kuna marisasi, gari ya Mzee imepita kwa kasi lakini ye hayumo. Nikawapigia simu wanangu wakiwa kwao Mbweni. Nikamuuliza AMANI kama anajua Mzee yuko wapi. AMANI akasema nitulie kwani wao wanajua aliko. Nikampigia simu KISASI, aliyekuwa Kamishna wa Polisi lakini akapokea mkewe na kuniambia ameenda huko hospitali kufuatia kupigwa kwa Mzee. Nikaamua nami niende lakini majirani wakanizuia. Lakini nikalazimisha na nikaenda kwa kupitia vichochoroni".
24.2. Mama KARUME Akataliwa Kuingia Hospitalini
Mama KARUME alipofika hospitalini alikuta wanajeshi lukuki wametanda maeneo yote na hakuna mtu yeyote aliyeruhusiwa kupeleka pua yake!. Alipotaka kuingia, akazuiwa!.
24.3. Mama KARUME Afanikiwa Kuingia Hospitalini
Bahati nzuri, kati ya wanajeshi wale, alikuwepo HAJI MRISHO, kijana aliyelelewa na Mama KARUME ambaye aliwaambia wenzake- "Mama KARUME huyo, mpisheni aingie"!. Ndipo Mama KARUME alipofanikiwa kuingia.
24.4 Mama KARUME Apatwa na Uchungu Mwingi
Muda wote huu, Mama KARUME alikuwa anajua mmewe ameumizwa tu, hakuwaza kabisa kuwa amefariki. Alipooneshwa chumba na kuuona mwili wa mmewe ukiwa umewekwa kwenye strecha huku umefunikwa shuka, ghafla akapigwa na bumbuazi lakini akajipa moyo kuwa huenda mmewe bado anapumua.
Mama KARUME alipolitoa shuka hilo ghafla aliangua kilio kikubwa, akamkumbatia mmewe huku akiongea mambo yasioleweka na ikawa tafrani kubwa!!!.
Mama KARUME anaelezea-:
"Kuona hali yangu ilivyokuwa, bwana mmoja akamfuata Bi ASIA AMOURY aliyekuwa matron na kumueleza hali yangu ilivyokuwa. Bi ASIA akashauri wamueleze daktari. Daktari akawaambia waniache tu, wasinibugudhi, nifanye nitakacho hadi nitakaporidhika".
24.5. AMANI & ALI Wawasili
AMANI na ALI waliletwa hospitalini hapo na kumkuta mama yao katika hali ya kuchanganyikiwa. Walimwangalia marehemu Baba yao, kisha AMANI akamuuliza mama yake- "Je, umenifahamu mimi, mimi ni nani?". Mama KARUME akamjibu- "Nakujua, we si mwanangu AMANI". AMANI akamwambia mama yake- "Mzee ndio ameishafariki na hakuna chochote tunaweza kufanya kuibadili hali hii, kwahiyo twende zetu".
Hivyo, wakaondoka.
25. Hali ya Hatari Yatangazwa
Kufuatia mauaji hayo na kimuhemuhe kilichofuata, Baraza la Mapinduzi likatoa amri:
"Wananchi, hili ni Tangazo Muhimu sana la Baraza la Mapinduzi: Kuanzia saa mbili leo usiku hakuna ruhusa mtu yeyote kutembea kwenda popote. Watu wote mkae majumbani kwenu. Pia, angani na baharini hakuruhusiwi kupita chombo chochote. Asanteni".
26. TZ Yakumbwa na Simanzi
Kutokana na mauaji hayo, TZ nzima na hasa Zanzibar ilikuwa ni vilio na simanzi tupu!.
27. Serikali Yatoa Taarifa ya Mauaji
Kesho yake, siku ya Jumamosi, tarehe 8.4.1972, Serikali ilitoa taarifa rasmi kuhusu mauaji hayo.
28. Marehemu Rais KARUME Azikwa
Saa 3 asubuhi, siku ya Jumatatu, tarehe 10.4.1972, mwili wa marehemu Rais KARUME uliwekwa kwenye jengo la serikali Forodhani ambako mamia ya wananchi walienda kutoa heshma zao za mwisho na kisha jeneza kupelekwa Ikulu, kisha Afisi Kuu Kisiwandui na kisha kuzikwa ambapo maelfu ya wananchi na viongozi mbalimbali, akiwemo Baba wa Taifa, Mwalimu JK NYERERE, walihudhuria. Kwa hakika, ilikuwa ni huzuni kubwa mno!.
Hitma ya marehemu Rais KARUME ilisomwa tarehe 29.7.1972 kwenye klabu ya ukumbi wa wananchi na kuhudhuriwa na watu wengi.
29. MWISHO
Jumanne ya leo, tarehe 7.4.2020, Taifa linaadhimisha miaka 48 ya kuondokewa na marehemu SHEIKH ABEID AMANI KARUME, Mwanamapinduzi wa aina yake na wa kipekee. Kwa hakika, Taifa lilimpoteza Kiongozi shupavu sana.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇