Waziri wa Madini Dotto Biteko amewaruhusu wakazi wa kijiji cha Mundindi wilaya ya Ludewa mkoani Njombe kuendeleza mashamba yao kwa kulima mazao ya muda mfupi mpaka pale muwekezaji wa mradi wa liganga atakapowalipa fidia zao.
Hayo ameyasema alipotembelea mradi wa liganga uliopo mkoani humo baada ya wakazi wa kijiji hicho kulalamika kuwa wanazuiliwa kulima mashamba yao pasipo kulipwa fidia yoyote kitu ambacho kinawarudisha nyuma kimaendeleo.
Wananchi hao wandai kuwa walikubali kupisha mradi huo kwa kutoa maeneo yao huku wakipewa matumaini makubwa juu ya kunufaika na mradi huo lakini mpaka sasa hawajaona maendeleo yoyote ya kuendelea kwa mradi wala kulipwa fidia.
Waziri Biteko aliwapa ruhusu ya kufanya shughuli hizo za kilimo na kuwataka kuwa wavumilivu kwani kuchelewa huku kwa mradi ni kwaajili ya kuwasaidia wao wenyewe ili waweze kupata manufaa yenye tija badala ya kuharakisha kitu ambacho kinaweza kupoteza haki zao.
Alisema kuna majadiliano ya kupitia mkataba upya na kufanya marekebisho ya sheria ya uchimbaji chuma yanayoendelea kujadiliwa juu ya mradi huo uliopo katika kijiji hicho ambayo yataongeza manufaa kwa wakazi wa wilaya na mkoa huo na watanzania kwa ujumla.
“Nimesimama hapa kuwaomba kuwa muwe na subira kwakuwa ni bora tukawie kufika ili tukifika tufike kwa usahihi kuliko kufanya kwa uharaka na pupa baadae tukaanza kulaumina na ndiyo maana tunafanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuona kitu gani kinaendelea hivyo tunaomba muendelee kuwa wavumilivu serikali itakuja na majibu juu ya jambo hili”, Alisema Biteko.
Aliongeza kuwa kupitia mkataba huu watanzania wengi watapata ajira kwani mkataba wa awali ajira nyingi zingetoka kwa raia wa kigeni badala ya wazawa ambapo pia ulionyesha wageni kuchukua asilimia 80 ya mapato huku wazawa wakibakiwa na asilimia 20 na katika hiyo bado kulikuwa na misamaha mingi ya kodi.
Alisema imekuwa ni bahati majadiliano hayo yanafanyika huku uchimbaji huo ukiwa bado haujaanza wakati shemu nyingine hufanyika makubaliano baada ya uchimbaji.
Aliongeza kuwa kuna zaidi ya tani milioni 400 ambazo zipo katika mradi huo na zinaweza kuchimbwa kwa zaidi ya miaka hamsini hivyo ni lazima tuwe na mkataba wenye manufaa kwetu na kusahihisha mahala palipokosewa.
Katika ziara hiyo Biteko aliongozana na mkuu wa mkoa huo Bw. Christopher Ole Sendeka, mkuu wa wilaya ya Ludewa Andrea Tsere, Mkurugenzi wa wilaya ya Ludewa Sunday George pamoja na kamati ya ulinzi na usalama.
Mkuu wa mkoa wa njombe Christopher Ole Sendeka ( katikati) akimuonyesha waziri wa madini (kulia) Dotto Biteko eneo la mradi wa liganga. Kushoto ni mkuu wa wilaya ya Ludewa Andrea Tsere
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇