Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Utawala na Serikali za Mitaa wakiwa katika eneo la mmoja wa Walengwa wa TASAF
(bi. Edith Makala ) wakishuhudia namna mradi wake ya kushona nguo aliouanzisha
baada ya kupata ruzuku ya TASAF unavyotekelezwa.
Mmoja wa walengwa wa TASAF Bi. Esther Mangi
Nkumbi (aliyevaa kitambaa cha bluu kichwani ) akiwaelezea wajumbe wa Kamati ya
kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa namna alivyonufaika na ruzuku
kutoka TASAF kwa kuanzisha shughuli ya kutengeneza sabauni za maji. Kulia kwake
ni Naibu Waziri wa Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora Dkt. Mary
Mwanjelwa akifuatiwa na Mkurugenzi
Mtendaji wa TASAF ,Bw. Ladislaus Mwamanga.
NA ESTOM SANGA- TASAF.
Wajumbe
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa
wameridhishwa na mafanikio ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini
unaotekelezwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF
ambao ameamsha ari ya Kaya za walengwa kuuchukia umaskini kwa vitendo.
Wakizungumza
baada ya kupata ushuhuda kutoka kwa Baadhi ya Walengwa wa TASAF na
kukagua shughuli za kujiongezea kipato zilizotokana na matumizi ya
ruzuku ya TASAF mkoani Singida Wajumbe wa Kamati hiyo wamesema matokeo
chanya yaliyopatikana ni kielelezo tosha cha namna juhudi za serikali
na wananchi katika kupambana na umaskini nchini zilinavyofanikiwa.
Mwenyekiti
wa Kamati hiyo Mhe. Steven Rweikiza akiwahutubia walengwa na wananchi
mjini Singida amesema hamasa ya kuuchukia umaskini miongoni mwa
Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ni kubwa na kushauri
juhudi zaidi zielekezwe katika kuboresha mazingira ya kukuza shughuli za
uzalishaji mali zilizoanzishwa na Walengwa hao ili ziwe endelevu.
‘’…….. hili ni jambo jema sana katika kupambana na umaskini hususani kwa Kaya za Walengwa ‘’ amesisitiza Mhe. Rweikiza.
Wakiwa
mjini Singida, Wajumbe wa Kamati kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali
za Mitaa wamepata ushuhuda kutoka kwa baadhi ya Walengwa wa TASAF wa
namna walivyotumia ruzuku waliyopata kuanzisha shughuli za kujiongezea
kipato ikiwemo mradi wa cherahani na utengenezaji wa sabuni, uboreshaji
wa makazi na kuhudumia familia zao hususani katika sekta ya elimu ,afya
na lishe .
Mmoja wa Walengwa hao Bi.Edith Brayson Makala (55)
ameeleza namna alivyotumia sehemu ya ruzuku ya TASAF kununua cherahani
na kuanzisha mradi wa ushonaji wa nguo ambao amesema umewezesha kubadili
maisha yake kutoka hali duni kabisa na sasa anaweza kuhudumia familia
yake yenye watoto watano.
‘’ …..ninamshukuru sana Rais John
Magufuli kwa msaada huu Mungu amubariki kwa kutukumbuka sisi wanyonge ‘’
amesisitiza Mlengwa huyo wa TASAF.
Kwa Upande wake Waziri wa
nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
George Mkuchika amesema mafanikio ya Kipindi cha kwanza cha Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini yamekuwa ya mafanikio makubwa na kumshukuru Rais
John Magufuli na Serikali yake kuruhusu kipindi cha pili kuanza ambacho
amesema kitatekelezwa kwa ufanisi zaidi ili wananchi wenye sifa za
kujumuishwa kwenye Mpango huo waweze kupata fursa hiyo.
‘’…….tumejipanga
vizuri na tunaagiza wahusika wote kuhakikisha kuwa shughuli za TASAF
kwenye maeneo yao zinasimamiwa vema ili kuleta tija iliyokusudiwa’’
amesema Waziri Mkuchika.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,bwana
Ladislaus Mwamanga amemshukuru Rais John Magufuli na Serikali yake kwa
kuendelea kuweka mazingira wezesha ya Mfuko huo kutoa huduma zake kwa
ufanisi na kuahidi kuwa jukumu hilo muhimu litanywa kwa ufanisi mkubwa
ili hatimaye walengwa waweze kupunguza adha kubwa ya umaskini .


No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇