WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amethibitisha kuwa Tanzania ina mgonjwa mmoja mwanamke (46) mwenye virusi vya Corona, aliyeingia nchini kwa ndege ya Rwandair kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akitokea nchini Ubelgiji.
Waziri huyo ameyasema hayo leo Jumatatu Machi 16, 2020, alipokutana na waandishi wa habari katika ofisi za Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Tafiti za Tiba (NIMRI).
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo na wizara yake, mgonjwa huyo ambaye alipita katika nchi za Sweden, Denmark na Ubelgiji kabla ya kurejea nchini, alipelekwa katika kituo maalum cha kuwahifadhi na kuwahudumia waathirika wa Corona kilichopo nje kidogo ya Hospitali ya Mawenzi mkoani Kilimanjaro ambapo anapatiwa matibabu na anaendelea vizuri.
“Nimeongea naye mgonjwa huyo leo tena mara kadhaa, anazungumza vizuri tu, lakini katika maelezo yake anasema alikuwa Ubelgiji, kwenye nyumba aliyofikia, mume wa mwenyeji wake alikutwa na maambuziki ya ugonjwa wa Corona.
“Alipofika hapa nchini alikuwa akikohoa, hakwenda nyumbani kwake, alijifungia hotelini na baadaye akaenda hospitali mwenyewe, walipomuona madaktari walimhudumia wakachukua sampuli na kuileta Dar es Salaam Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii ambapo walibaini kuwa ana virusi vya Corona,” amesema Mwalimu.
Aidha, amesema serikali inawafuatilia watu wote aliokutana nao mgonjwa huyo ili kuwaweka katika chumba maalum kwa ajili ya uangalizi kwa siku 14.
Ummy amewataka wananchi kutokuwa na hofu kwani mgonjwa huyo ametoka nao nje ya Tanzania na kwamba anaendelea vizuri lakini pia serikali imejitayarisha kudhibiti tishio la maambukizi hayo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇