LATEST HEADLINES👉

Mar 20, 2020

CHID BENZ AKEMEA WANAOFANYA MZAHA MITANDAONI KUHUSU UGONJWA WA CORONA, ASEMA AMEACHA KUTUMIA DAWA ZA KULEVYA, ANAJIANDAA KURUDI KWENYE 'GEMU'

Msanii wa muziki wa Bongofleva Rashid Abdallah (Chid Benz) akimweleza jambo Naibu Waziri Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza, katika mazungumzo yao yaliyofanyika leo jijini Dodoma. Chid amemweleza Naibu Waziri kuwa wiki ijayo anatarajia kutoa video ya wimbo wake wa Beautiful na pia atatunga wimbo kuhusu virusi vya ugonjwa wa Corona.



Na Anitha Jonas – WHUSM
Mwanamuziki ambaye ni miongoni mwa wanamuziki waasisi wa muziki wa Bongofleva hapa nchini, Rashid Abdallah (Chid Benz), ametoa mwito kwa Watanzania kuacha kufanyia mzaha ugonjwa wa Corona hasa katika mitandao ya Jamii, kwa kuwa ni ugonjwa hatari duniani na ameahidi kutunga wimbo kuhusu janga hilo.

Amesema, Virusi vya ugonjwa wa Corona ni tatizo na janga kubwa linaloisibu na kuisumbua Dunia yote ikiwemo Tanzania hadi sasa, kwa hivyo siyo kitu au jambo la mzaha, isipokuwa cha msingi ni kila mtu kulichukulia kuwa ni janga kubwa hivyo kuomba Mungu na kujitahidi kujikinga kwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na serikali na wataalamu wa afya.

Chid Benz amesema hayo leo jijini Dodoma, alipofanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Habari, Utamadini, Sanaa na Michezo Juliana Shonza ambapo alitumia fursa hiyo kumwambia Naibu Waziri huyo kuwa kwa sasa  amebadilika na anataka kuwaonyesha Watanzania kuwa amefanikiwa kujikwamua katika dimbwi alilokuwemo la kutumia adawa za kulevya.

Msanii huyo alimwambia Naibu Waziri kwamba hadi sasa ana zaidi ya miezi mitatu bila kutumia kabisa dawa za kulevya na hataki tena kurudi kuzitumia, baadala yake anataka kurudi kwenye 'gemu' ili kuwafurahisha mashabiki wake ambao alisema anaamini anao wengi.

"Ninaelewa bahati haiji mara mbili lakini kwangu naiona imekuja zaidi ya mara moja kwa maana ya kuwa nimekuwa naanguka nainuka narudi kwa mashabiki wananipokea nakuendelea kukubali muziki wangu, hakika najiona ni wakati wa kuwafurahisha zaidi mashabiki na sitawaangusha.

“Ombi langu kwa serikali ni kupata ushirikiano na mapema wiki ijayo ninatarajia kutoa wimbo wangu mmoja uitwao Beautiful ambao nimeuiamba nikisifu uzuri wa mwanamke na pia nitatunga wimbo kuhusu janga hili la virusi vya ugonjwa wa Corona lililoingia nchini kwetu", alisema Chid Benz 

“Kati ya wasanii wenye kukubalika  na mashabiki zao wewe Chid Benz  ni mmoja wao na mashabiki zako ni wengi hivyo ningependa kukuona kuanzia sasa unalijenga zaidi  jina lako kwa kuonyesha kuwa umebadilika, katika kipindi hiki, nitafurahi zaidi kukuona unasonga mbele na hurudi tena katika matumizi ya dawa za kulevya na ninakuahidi Wizara itakuwa pamoja na wewe kukusaidia wakati wowote ,” alisema Shonza.

Shonza alimsisitiza msanii huyo kuwaonyesha  Watanzania kuwa anaweza na hata akipewa nafasi anaweza kujitumia vyema  na kuonyesha juhudi yake katika kufanya kazi na kuwa mbunifu katika kufanya kazi zake za usanii.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Pages