LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 14, 2020

WAZABUNI CHANZO UCHELEWESHJI WA MIRADI

  Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) nchini Brigedia Jenerali Charles Mbuge  amesema kuwa baadhi ya wazabuni wanaouza vifaa vya ujenzi wamekuwa wakiuza vifaa kwa bei ya juu na kuchelewesha vifaa hivyo pale vinapohitajika, jambo linalopelekea baadhi ya miradi inayotekelezwa na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi hilo (SUMA JKT) kutokamilika kwa wakati.

Brigedia Jenerali Mbuge ameyasema hayo Februari 13, 2020 mjini Bariadi wakati akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya ujenzi inayotekelezwa na SUMA JKT mkoani Simiyu.

Ameongeza kuwa katika kukabiliana na changamoto hiyo, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limejipanga kuanzisha maduka ya vifaa vya Ujenzi vitakavyouzwa kwa bei ya  jumla ili kuwezesha upatikanaji wa vifaa kwa urahisi, haraka na kwa bei nafuu ikilinganishwa na wazabuni wengine.

“Tatizo moja ninaloliona kwenye utekelezaji wa miradi ni vifaa kuuzwa kwa bei ya juu sana na kucheleweshwa, tumeamua kuwa  na maduka ya vifaa ya jumla; tutatoa maelekezo kwa wakuu wa kanda za ujenzi watatupatia mahitaji yao, ili kuwawezesha kufanya kazi kwa wakati kama tunavyokubaliana na washitiri wetu,” alisema Brigedia Jenerali Mbuge.

Katika hatua nyingine Brigedia Jenerali Mbuge amesema jeshi hilo litaendelea kuwatumia vijana watakaomaliza mafunzo ya JKT katika shughuli zilizopo kwenye miradi inayotekelezwa na Jeshi hilo lengo likiwa kuwawezesha vijana hao kupata kipato na baadaye waweze kujiajiri badala ya kutegemea kuajiriwa pekee.

Vile vile ameahidi kuongeza nguvu kazi ya vijana katika mradi inayotekelezwa na SUMA JKT mkoani Simiyu kuongeza kasi na miradi hiyo iweze kukamilika kwa muda uliopangwa, huku akitoa wito kwa Taasisi mbalimbali kuipa kazi SUMA JKT,  ili iendelee kuwa kutoa gawio kubwa kwa Serikali, ambapo amesema mwaka 2018/2019 ilitoa zaidi ya shilingi bilioni moja na mwaka 2019/2020 linatarajia kupanda zaidi kutokana na uwepo wa vyanzo vya kutosha.

Awali akitoa taarifa, Katibu Tawala Msaidizi Seksheni ya miundombinu katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, mhandisi Mashaka Luhamba  amesema JKT wanatekeleza miradi minne mkoani Simiyu ukiwemo wa ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa,  wodi ya wazazi Hospitali ya Rufaa ya mkoa, ujenzi  jengo la wizara ya kilimo linalojengwa kwenye viwanja vya maonesho ya Nane nane pamoja na  kiwanda cha Chaki Maswa ( Maswa chalk) .


Aidha mhandisi huyo amebainisha kuwa ujenzi wa jengo la Mkuu wa Mkoa unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 18 kwa gharama ya shilingi bilioni 5.7  ambapo ujenzi rasmi ulianza mwezi Mei, 2019 na endapo fedha zitapatikana kwa wakati unatarajiwa kukamilika Novemba,  2020.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema ni vema SUMA JKT ikahuisha uharaka wa kutekeleza miradi kama jamii inavyoutarajia kwa kuwa jamii na Serikali imejenga imani kubwa kwa JKT kutekeleza miradi kwa wakati ikilinganishwa na wakandarasi wengine.

Mtaka ameongeza kuwa miradi inayotekelezwa na SUMA JKT iwe fursa kwa vijana waliopata mafunzo ya JKT na kumaliza mikataba yao ili waweze kupata kipato kitakachowasaidia kwenda kujitegemea na kujiajiri endapo hawataajiriwa.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages