Hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuzindua mpango kwa jina la 'Muamala wa Karne' tarehe 28 Januari mwaka huu ambao umewasilishwa eti kwa ajili ya kutatua mzozo wa muda mrefu kati ya Wapalestina na utawala wa Kizayuni, umepingwa vikali ndani na nje ya Marekani.
Katika hatua yake ya karibuni kabisa dhidi ya mpango huo; wawakilishi 107 wa chama cha Democrat katika Kongresi ya Marekani wameutaja mpango huo wa "Muamala wa Karne" kupitia barua yao kwa Rais wa nchi hiyo hapo jana kuwa usiowiana na suala la amani na kuupinga vikali. Mpango huo unadaiwa kuwa na lengo la kufikia amani kati ya Waisraili na Wapalestina. Huku wakibainisha kuwa vipengee vya mpango huo na pia muda wa kuzinduliwa kwake vimeibua hali ya wasiwasi, wawakilishi hao wa Bunge la Kongresi ya Marekani wameutaja Muamala wa Karne kuwa mpango ambao hauna azma thabiti na usio na nia njema; na kusisitiza kuwa mpango huo unaiandalia Israel njia ya kulikalia kwa mabavu milele eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Wawakilishi hao wamesisitiza pia kwamba mpango huo wa hila uliopendekezwa na Trump kwa ajili ya nchi ya Palestina ni majumui ya ardhi zilizotengana na ambazo zimezingirwa na vitongoji na miundomsingi ya utawala wa Kizayuni ambazo hazina mshabaha wowote na nchi.
Wawakilishi hao wa Kongresi ya Marekani aidha wameikosoa timu iliyoundwa na Trump kuandaa mpango huo na kuitaja kuwa kati ya makundi ya maadui wa nchi ya Palestina. Wameongeza kuwa hakuna Mpalestina yoyote wala kiongozi wa Palestina aliyeshirikishwa katika mashauriano kuhusu mpango huo wa Muamala wa Karne na kueleza wasiwasisi wao mkubwa kuhusu mpango huo. Wawakilishi wa Kongresi ya Marekani wamekosoa pia kitendo cha kuzinduliwa mpango huo katika kukaribia uchaguzi wa tatu wa utawala wa Kizayuni katika kipindi cha mwaka mmoja na tuhuma zilizotolewa ndani ya utawala huo dhidi ya Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni.
Andy Levin, Rashida Tlaib na Ilham Omar wabunge kutoka chama cha Democrat na Bernie Sanders, Elizabeth Warren, Chris Van Hollen na Chris Murphy maseneta wa chama cha Democrat wametangaza kuupinga mpango huo.
Donald Trump amechukua hatua kadhaa muhimu kwa maslahi ya Israel tangu aingie madarakani ambazo hakuna Rais yoyote wa zamani wa Marekani aliyedhamiria au kuthubutu kuzichukua. Miongoni mwa hatua hizo za Trump ni kuitambua Quds Tukufu kama mji mkuu wa utawala wa Kizayuni, kutambua rasmi kuunganishwa ardhi za Golan za Syria na ardhi nyingine za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel, kusitisha misaada ya kifedha kwa shirika la Kuwahudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa (UNRWA), kumfukuza Balozi wa Palestina huko Washington, kujitoa UNESCO na katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na mwisho ni kuruhusu kuunganishwa maeneo ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Pamoja na hayo, kutangazwa na kuwasilishwa mpango wa Muamala wa Karne inahesabiwa kuwa hatua muhimu inayodhihirisha uungaji mkono wa pande zote wa serikali ya Trump kwa utawala wa Kizayuni. Miongoni mwa malengo yanayofuatiliwa na serikali ya Trump kupitia mpango huo ni kuupatia ufumbuzi mzozo wa Wapalestina na utawala wa Kizayuni lakini kwa maslahi kamili ya utawala huo na kutoa huduma nyingi na za aina yake kwa Wazayuni mkabala na kuwaridhisha Wapalestina wakubali serikali ndogo zaidi (Micro State) katika ardhi ndogo sana ya Palestina, yaani katika ukubwa wa asilimia 12 tu ya ardhi yote ya Palestina. Njama hiyo inayotekelezwa kwa ahadi ya kuwapa Wapalestina msaada wa dola bilioni 50, inakusudiwa kuiletea serikali ya Trump mafanikio makubwa ya kisiasa katika uga wa kimataifa katika mwaka huu wa uchaguzi wa rais nchini Marekani na hivyo kumzolea kura za Wayahudi wa nchi hiyo na hasa lobi za Wazayuni khususan ile ya AIPAC, kuandaa uwanja wa kufanywa kuwa wa kawaida uhusiano wa Israel na nchi za Kiarabu khusuan nchi waitifaki wa Washington kama Imarati, Bahrain, Oman na Saudi Arabia na hatimaye kutoa pigo kubwa kwa mhimili wa muqawama katika eneo la Asia Magharibi, kwa madai ya kutokuwepo tena falsafa ya uwepo wa muqawama huo, yaani kupigania kadhia ya Palestina.
Pamoja na hayo yote, Wapalestina wote ikiwemo Serikali ya Ndani ya Palestina, makundi ya muqawama na wananchi wa kawaida wa Palestina, aghalabu ya nchi za Kiarabu na Kiislamu na pia wanachama wengine wa kundi la pande nne yaani Russia, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa wamepinga mpango huo wa Muamala wa Karne. Paul Larudee mjumbe wa Harakati ya Mshikamano wa Kimataifa dhidi ya Uzayuni ameutaja mpango wa Muamala wa Karne kuwa ni tishio hatari kwa uwepo wa Wapalestina na kueleza kuwa: Katika hatua itakayofuata; Marekani itazikalia kwa mabavu ardhi za Kiislamu kwa maslahi ya utawala ghasibu wa Israel. Hatua ya wawakilishi 170 wa chama cha Democrat katika Kongresi ya Marekani ya kutangaza kuupinga vikali mpango wa Muamala wa Karne ni pigo kubwa jingine kwa mpango huo na kwa njozi za Trump za kukaliwa kikamilifu kwa mabavu na utawala wa Kizayuni ardhi za Palestina.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇