WADHAMINI wa aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu, Ibrahim Ahmed na Robart Katula wamefungua maombi katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakiomba itolewe amri ya kukamatwa kwa mshtakiwa huyo kwa kuwa wao wameshindwa kumpata.
Madai hayo yamewasilishwa leo Februari 20, 2020 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati kesi dhidi ya Lissu ilipopangwa kwa ajili ya kutajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Mapema wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai kuwa kesi hiyo leo imepangwa kwa ajili ya kutajwa na kwamba amri za awali kuhusu mshtakiwa Lissu zinaendelea na Upande wa Jamhuri unaomba wadhamini waieleze mahakama wamefikia hatua gani.
Hata hivyo mdhamini Katula alidai kuwa wamefungua maombi mahakama hapo kwamba wameshindwa kumpata Lissu na wameiomba mahakama itoe amri ya kumkamata na maombi hayo yamepangwa kutajwa kesho.
Wankyo amedai kuwa ni kweli wamepokea nakala ya maombi ya wadhamini hao na kwamba wanasubiri kesho kwa ajili ya kutajwa.
Mbali na Lissu washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni, Wahariri Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh ambapo kwa pamoja wa pamoja wanakabiliwa na mashtaka matano ikiwamo kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.
Ilidaiwa kuwa kati ya Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa Jabir, Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifaza uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’
Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.
Mshtakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13 ,2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.
Ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇