Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen.
Nicodemus Mwangela akifunga Kongamano la Vijana katika Kilimo
lililofanyika Mkoa wa Songwe na Kuhusisha vijana takribani 700 kutoka
Mikoa ya Songwe, Rukwa, Mbeya na Katavi ambapo ameahidi kuwapatia ardhi
vijana wanaotaka kuwekeza katika Kilimo.
Vijana takribani 700 kutoka Mikoa
ya Songwe, Rukwa, Mbeya na Katavi wakiwa katika Kongamano la Vijana
Katika Kilimo ambapo wamejadiliana masuala mbalimbali na kuwekeana
maazimio yatakayo boresha ushiriki wa vijana katika Kilimo
………………………………………………………
Vijana wenye nia
ya kuwekeza katika sekta ya kilimo Mkoani Songwe wamepewa ahadi ya
kupatiwa ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo ndani ya muda mfupi baada
ya kuwasilisha maombi yao.
Mkuu wa Mkoa wa
Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amtoa ahadi hiyo leo wakati
akifunga Kongamano la Vijana katika Kilimo lililofanyika Mkoa wa Songwe
na Kuhusisha vijana takribani 700 kutoka Mikoa ya Songwe, Rukwa, Mbeya
na Katavi.
Brig. Jen.
Mwangela amesema Mkoa wa Songwe unayo ardhi ya kutosha kwa ajili ya
shughuli za Kilimo ambayo bado haijatumika hivyo kijana yeyote mwenye
nia ya kuwekeza katika Kilimo afike ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
“Mkoa una hekta
Milioni mbili, mpaka sasa tumetumia asilimia 30 kwa ajili ya kilimo na
asilimia ndogo kwa ajili ya makazi na misitu hivyo tunalo eneo la
kutosha, mvua za kutosha na ardhi nzuri pia tunazo hekta elfu 18
zinazofaa kwa ajili ya kilimo cha umwgiliaji hivyo ardhi bado ipo ya
kutosha.”, amesema Brig. Jen. Mwangela.
Ameongeza kuwa
kijana mwenye nia ya kuwekeza kwenye Kilimo akifika ofisi ya Mkuu wa
Mkoa ata taja Wilaya anayotaka kewekeza ili aelekezwe isipokuwa kijana
hatatakiwa kuchagua mwenyewe eneo maalumu ambalo tayari linamilikiwa na
watu wengine.
Brig. Jen.
Mwangela amewasisitiza Vijana kuchangamkia fursa ya kumiliki ardhi
kihalali kwakuwa bado inapatikana kwa urahisi ili baadaye wasihangaike
kuitafuta wakati wa uzee na kuongeza kuwa waache kulalamikia wazazi au
serikali kutokana na umasikini bali wajikite katika Kilimo.
Amesema asilimia
67 ya nguvu kazi ni vijana ambao hawana ajira ambapo nguvu kazi hii
ikibaki bila ajira ni aibu kwa vijana na taifa hivyo mkakati wa Wizara
ya Kilimo wa Kuhakikisha vijana wanajikita katika Kilimo ni mzuri na
utainua uchumi wa taifa kwa haraka.
Brig. Jen.
Mwangela ameongeza kuwa vijana wakishiriki kikamilifu katika Kilimo
uchumi utakua, viwanda vitaongezeka na wataweza kuyafurahia maisha
kwakuwa Kilimo hakijawahi kumtupa mtu na pia wasiache kuangalia fursa
katika sekta za ufugaji na uvuvi.
Aidha Brig. Jen.
Mwangela amewaeleza Vijana waliohudhuria Kongamano hilo kuwa Serikali
itawaunganisha na taasisi zinazotoa mikopo ya Kilimo isipokuwa
watatakiwa kuwa waamini na kurejesha mikopo hiyo.
Ameongeza kuwa
wapo baadhi ya watu ambao walipatiwa mikopo ya Kilimo na baadhi ya benki
lakini wamekuwa sio waaminifu kwa kutorudisha mikopo hiyo au kuwa
wasumbufu katika kurejesha mikopo hiyo hivyo vijana hao wasiige mifano
yao.
Naye Afisa
Programu kutoka Jukwa la Wadau wa Kilimo (ANSAF) Rehema Msami amesema
wamefanya utafiti kuhusu namna ambayo halmashauri zimekuwa zikitoa
asilimia 10 ya mapato yao kwa ajili ya wanawake, vijana na walemavu.
Msami amesema
utafiti wao umebaini kuwa vijana wengi wenye sifa hawapati mikopo hiyo
na hivyo kushindwa kuwa na mitaji ya kuwekeza katika shughuli mbalimbali
ikiwa ni pamoja na kilimo, pia baadhi ya vijana wanaopewa mikopo hawana
sifa na hivyo kushindwa kurejesha mikopo hiyo.
Nelusigwe Kibona
kijana Mkulima wa Mbogamboga kutoka Rungwe Mkoani Mbeya amesema
Kongamano la Vijana limempa elimu na mbinu nyingi za Kulima kisasa
pamoja na kutafuta masoko ya mazao yake.
Kibona
ameupongeza Uongozi wa Mkoa wa Songwe kwa kuwasaidia vijana kupata ardhi
kwa ajili ya Kilimo na kuiomba mikoa mingine iige mfano huo.
Kenedy Kyando
Kijana Mkulima Kutoka Vwawa Songwe amesema kuwa Vijana wengi hawataki
kujishughulisha na Kilimo kwa kukosa uvumilivu na kutaka fedha za haraka
huku akiiomba Serikali kufanya makongamano kama hayo mara kwa mara.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇