Msemaji wa Ikulu ya Rais wa Uturuki amesema kuwa hadi sasa nchi hiyo haijafikia natija ya kuridhisha kuhusiana na pendekezo la Russia la kusitisha mapigano katika mkoa wa Idlib nchini Syria.
Akizungumzia suala hilo mbele ya waandishi habari siku ya Jumatano, İbrahim Kalın amesema kuwa duru kadhaa za mazunguzmo kati ya jumbe za Uturuki na Russia ambayo yamefanyika katika miji mikuu ya nchi hizo yaani Ankara na Moscow, kuhusu udharura wa usitishwaji vita katika mkoa wa Idlib hazijakuwa na natiha yoyote ya kuridhisha lakini akaongeza kuwa mazungumzo bado yataendelea.
Msemaji huyo wa Ikulu ya Rais wa Uturuki amedai kwamba nchi hiyo imepeleka zana zake za kijeshi huko Idlib kwa lengo la kulinda usalama wa raia katika mkoa wa Idlib nchini Syria na wakati huohuo kuilaumu jamii ya kimataifa kwa kutochukua hatua yoyote ya maana kuhusu mgogoro wa Syria.
Ni karibu miezi miwili sasa ambapo serikali ya Damascus imechukua hatua muhimu ya kuusafisha mkoa wa Idlib kutokana na uchafu wa makundi ya kigaidi yanayotekeleza shughuli zao za ugaidi katika eneo hilo kwa ushirikiano na msaada wa nchi za kigeni, na kufikia sasa imepiga hatua muhimu katika uwanja huo. Jambo la kusikitisha ni kwamba Uturuki imeteka na kukalia kwa mabavu ardhi ya Syria kwa madai ya kupambana na ugaidi.
Matamshi ya İbrahim Kalın yanatolewa katika hali ambayo Uturuki imekiuka moja kwa moja kujitawala kwa Syria na kuelekeza mabomu na makombora yake dhidi ya askari wa nchi hiyo kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Kwa kushikilia msimamo wake wa kuyaunga mkono makundi ya kigaidi yanaoendesha shughuli zake katika mkoa wa Idlib, Uturuki inajaribu kuakhirisha ushindi wa jeshi la Syria dhidi ya makundi hayo ya kigaidi na kisha kuyatumia kama chombo cha kutoa mashinikizo katika mazungumzo yake ya baadaye kuhusu hali ya kaskazini mwa Syria.
Pamoja na hayo, jambo lililo wazi ni kuwa Uturuki haiweze kuendelea kuzuia kushindwa kwa makundi hayo ya kigaidi. Idlib ni sehemu ya ardhi ya Syria na jeshi la nchi hiyo lina haki ya kupambana na magaidi walioko katika eneo hilo na kulirejesha mikononi mwa serikali ya Damascus kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Kwa msingi huo, ni wazi kuwa kuendelea kwa siasa za Uturuki katika eneo hilo hakutakuwa na natija nyingine ghairi ya kuharibiwa Idlib na kudhuriwa raia wanaoishi katika mkoa huo. Uturuki haiwezi kutumia kisingizio cha kulinda raia kama mbinu ya kuingilia masuala ya Syria. Hii ni kwa sababu tokea mwanzo wa mgogoro wa Syria, Uturuki imefuatilia waziwazi siasa zake za uingiliaji masuala ya ndani ya Syria kwa kuyadhamini kwa hali na mali makundi ya kigaidi kaskazini mwa nchi hiyo na pia kwa ushirikiano wa makundi mengine ya kimataifa ya kigaidi likiwemo la al-Qaida, makundi ambayo yametekeleza jinai za kutisha dhidi ya raia wa Syria.
Kwa maelezo hayo, ni wazi kuwa kuendelea mgogoro wa nchi hiyo ya Kiarabu unaochochewa na nchi za kigeni, hakutakuwa na natija nyingine ghairi ya kuvuruga zaidi usalama wa Syria na raia wa nchi hiyo kuendelea kutumiwa na makundi ya kigaidi kama ngao ya binadamu. Ni wazi kuwa Uturuki inapasa kutekeleza majukumu yake ya kimataifa na kuamua kuchangia juhudi za kurudisha usalama na uthabiti katika mkoa wa Idlib na hatimaye kushirikiana na serikali ya Syria katika kubomoa vituo vyote vya magaidi kaskazini mwa nchi hiyo.
Hata kama kwa sasa makundi ya kigaidi yanafurahia uungaji mkono wa serikali ya Uturuki lakini ni wazi kuwa makundi hayo hivi karibuni yatalazimika kuchagua moja kati ya mambo mawili, ima kusalimu amri mbele ya jeshi la Syria na kuwajibishwa kisheria kuhusu jinai yalizotenda au kuendelea kucheza mchezo wa kulinda maslahi ya Uturuki katika sehemu nyingine za dunia.
Hii ni kwa sababu kama Uturuki itafanikiwa kufikia malengo yake kaskazini mwa Syria, italazimika kuyatokomeza makundi hayo yote ya kigaidi ili yasije yakapenya na kuhatarisha maslahi yake katika ardhi ya Uturuki au italazimika kuyatumia kulinda maslahi yake katika maeneo mengine ya dunia kama vile Libya.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇