Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu amekutana na kufanya mazungumzo na kiongozi wa Baraza la Utawala la Sudan Luteni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan mjini Entebe, Uganda kwa lengo la kuanzisha uhusiano wa kawaida wa pande mbili.
Duru za habari zimeripoti kuwa, mazungumzo hayo kati ya Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na kiongozi wa baraza kuu la utawala la Sudan yalifanyika kwa siri hapo jana nyumbani kwa Rais Yoweri Museveni wa Uganda mjini Entebe.
Baadhi ya duru zimeripoti kuwa, kufuatia mazungumzo hayo, muda si mrefu ujao, ndege za utawala haramu wa Israel zitaweza kufanya safari zake kupitia anga ya Sudan.
Mazungumzo hayo yamefanyika siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo kufanya mazungumzo kwa njia ya simu na Al-Burhan na kumwalika kuitembelea Washington.
Kabla ya mazungumzo yake na Al-Burhan, Netanyahu alitangaza kuwa serikali ya Uganda imeafiki kujenga ubalozi wake katika mji wa Baitul Muqaddas (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni.
Katika miaka ya karibuni, utawala haramu wa Kizayuni umefanya harakati kubwa zinazolenga kupanua na kustawisha uhusiano wake na nchi za Kiafrika hasa zenye idadi kubwa ya Waislamu.
Mnamo mwezi Januari 2019, Netanyahu alifanya safari nchini Chad, hatua iliyopelekea kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya nchi hiyo na utawala haramu wa Israel.
Baada ya safari hiyo, maafisa wa Tel Aviv walitangaza kuwa, mbali na Chad, utawala huo wa Kizayuni umedhamiria kuanzisha uhusiano pia na nchi za Sudan, Niger na Mali.../
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇