Na Said Mwishehe, Michuzi Globu ya jamii.
JESHI la Polisi nchini limesema linasikitishwa na vifo vya watu 20 ambavyo vimetokea jana jioni mkoani Kilamanjaro kwenye kongamano la ibada ya Mchungaji Mwamposa huku likitumia nafasi hiyo kumtaka mchungaji huyo kujisajilimisha Polisi.
Limefafanua baada ya kutokea vifo vya watu hao walikuwa kwenye ibada ya mchungaji huyo, Mwamposa aliamua kukimbia na kwenda uwanja wa Ndege ambapo Polisi walipomfuatilia walimkosa, na hata walipofuatilia njia ya barabara nako hakupatikana.
Akizungumza leo Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini ,IGP Simon Sirro amesema mchungaji Mwamposa jana jioni wakati wa ibada yake aliwataka watu wakakanyage mafuta, hivyo bada ya kukanyaga mafuta wakianza kukanyagana na kusababisha watu 20 kupoteza maisha na wengine kujreruhiwa.
IGP Sirro amesema kati ya watu hao waliofariki mwanaume ni mmoja, watoto wanne na wanawake 15 na kwamba watu wengine wawili hali zao ni mbaya na sasa wamelazwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
"kwanza niwape pole watu waliopatwa na msiba huu ambao ni msiba mkubwa kwa nchi yetu.Pia tunamuomba Mwenyezi Mungu ndugu zetu ambao wameumizwa wakati wa kukanyaga mafuta wapone haraka na warejee kwenye shughuli za ujenzi wa nchi yetu. Tunamuomba Mwamposa ajisalimishe Polisi, tumemfuatilia uwanja wa ndege ametukwepa, tumefuatilia barabarani ametukwepa,"amesema IGP Sirro.
Hata hivyo amesema ni vema Watanzania wakawa makini kwani kinyume na hapo itakuwa shida sana na kuongeza iko haja kamati za ulinzi na usalama za wilaya na mkoa kuanza kuyafuatilia makanisa yote nchini na hasa makanisa madogo madogo ambayo sasa yamekuwepo kila mahali.
"Sio kwenye padri, mchungaji basi anataka kuwachunga kondoo wake waende kuuona ufalme wa Mungu, wengine wanahangaika na utafutaji tu wa maisha.Sio kwamba nahukumu lakini kuna mambo ya kujifunza,"amesema na kuongeza Mwamposa anafahamika na Polisi wanategemea atajisalimisha na kutoa ushirikiano.
Kuhusu Polisi iwapo walikuwepo kwenye kongamano hilo la Mwamposa, IGP Sirro amesema ameshatoa maagizo kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimajaro kufuatilia na iwapo walikuwepo polisi lazima waulizwe imekuaje hadi watu wakapoteza maisha na wao wakiwepo, kwani sheria lazima ichukue mkondo wake.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini ,IGP Simon Sirro
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇