Karibu raia 200 wameuawa katika mikoa miwili ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika makabiliano baina ya maafisa usalama na magenge ya wanamgambo likiwemo kundi la waasi la ADF la Uganda ndani ya siku 31 za mwezi uliopita wa Disemba 2019.
Hayo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti ya Kongo ya Chuo Kikuu cha New York inayofuatilia mauaji ya raia katika eneo la Kivu tokea mwaka 2017.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na taasisi hizo, raia 197 wameuawa na maafisa usalama na magenge yaliyojizatiti kwa silaha haswa kundi la wanamgambo wa ADF katika mikoa ya Kivu Kusini na Kivu Kaskazini katika kipindi hicho cha mwezi mmoja.
Ripoti hiyo imeeleza bayana kuwa, mauaji hayo ya raia ndiyo mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika eneo la Kivu la mashariki mwa DRC tangu Taasisi ya Utafiti ya Kongo ya Chuo Kikuu cha New York ibuniwe mwezi Juni mwaka 2017 kwa ajili ya kufuatilia mauaji ya raia.
Ripoti hiyo imetolewa chini ya wiki moja baada ya waasi wa ADF kuua watu 11 katika kile kinachotajwa na asasi za kijamii kwenye eneo la Beni na jimbo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa Kongo DR kwa ni shambulizi la kulipiza kisasi baada ya waasi hao kushindwa kukabiliana na jeshi la nchi hiyo.
Katika miezi ya hivi karibuni, wanamgambo hao wa ADF ambao asili yao ni Uganda wamekuwa wakiwashambulia raia, maafisa usalama na hata maafisa wa afya wanaopambana na ugonjwa hatari wa Ebola, mashariki mwa nchi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇