Na Mwandishi Maalum
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kipindi cha mwaka mmoja wa 2019 imeokoa zaidi ya shilingi bilioni 28 kwa kufanya upasuaji wa moyo kwa wagonjwa 1873 .
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma za matibabu ya moyo zilizotolewa na Taasisi hiyo kwa mwaka 2019.
Prof. Janabi alisema kama wagonjwa wote hao 1873 waliofanyiwa upasuaji hapa nchini wangetibiwa nje ya nchi Serikali ingetumia zaidi ya shilingi bilioni 56, lakini kwa wagonjwa hao kutibiwa hapa nchini matibabu yao yamegharimu kiasi cha shilingi bilioni 28.
“Fedha za matibabu ya wagonjwa hawa zimelipwa kupitia bima zao mbalimbali za matibu, wagonjwa wenyewe kujilipia, wadau mbalimbali kuchangia matibabu ya wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kulipa na Serikali kugharamia matibabu ya wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za matibabu”, .
“Utoaji wa huduma zetu umeongezeka kwa asilimia 29 ukilinganisha na mwaka 2018.Tumefanya upasuaji mkubwa wa kusimamisha moyo kwa wagonjwa 464 ambapo vifo vilikuwa asilimia 6 ya wagonjwa wote waliofanyiwa upasuaji”, alisema Prof. Janabi.
Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema Wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua kwa njia ya tundu dogo linalotobolewa kwenye paja kwa kutumia mtambo wa Cathlab (Catheterization laboratory) walikuwa 1409, wagonjwa sita walipoteza maisha ambapo ni sawa na asilimia 1.3.
Aidha Prof. Janabi alisema kwa mwaka 2019 waliona wagonjwa 108,946 wenye matatizo ya moyo. Kati ya wagonjwa hao wagonjwa wa nje walikuwa 105,142 na wagonjwa waliolazwa walikuwa 3,804 huku wanaume wakiwa ni asilimia 52 na wanawake asilimia 48.
Wagonjwa wengi wanaotibiwa katika Taasisi hiyo ni wale wenye matatizo ya Shinikizo la juu la damu, kutanuka kwa moyo, magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo, magonjwa ya valvu za moyo yanayotokana na maambukizi ya bakteria, umeme wa moyo kutokufanya kazi vizuri kwa muda mrefu, tatizo la ghafla la umeme wa moyo kutokufanya kazi vizuri au kwa haraka na mishipa ya damu ya moyo kuziba.
Alimalizia kwa kuwaahidi watanzania kwa mwaka wa 2020 wataendelea kutoa huduma bora na za utaalamu wa hali ya juu kwa wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo, kutoa elimu ya magonjwa ya moyo kupitia vyombo mbalimbali vya habari na kwa wananchi walioko nje ya mkoa wa Dar es Salaam kuendelea kupata huduma za Taasisi hiyo kupitia Hospitali zao za Mikoa na Wilaya.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇