Mamia ya raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamekimbilia nchini Uganda ndani ya mwezi mmoja uliopita kutokana na kushtadi mapigano ya kikabila nchini kwao.
Samuel Araali Kisembo, Mkuu wa Wilaya za Kikuube na Hoima magharibi mwa Uganda ameliambia shirika la habari la Xinhua kuwa, wamepokea wakimbizi zaidi ya 300 katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, ambao wanakimbia mapigano ya kikabila katika mkoa wa Ituri, mashariki mwa DRC.
Amesema wakimbizi hao wa Kongo DR waliowasili Uganda kupitia Ziwa Albert wamepelekwa katika kambi ya Sebigoro, na kwamba wanashirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uganda na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR kushugulikia maslahi ya wakimbizi hao.
Kwa mujibu wa UNHCR, Uganda ndiyo nchi ya tatu duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya wakimbizi wa DRC. Takwimu zinazonyesha kuwa, Uganda ni mwenyeji wa wakimbizi milioni 1.36 kutoka Kongo, Burundi na Sudan Kusini.
Mbali na mapigano ya kikabila, eneo la mashariki mwa DRC limekuwa likishuhudia hujuma za wanamgambo wa ADF ambao asili yao ni Uganda. Wapiganaji hao wa ADF wamekuwa wakiwashambulia raia, maafisa usalama na hata maafisa wa afya wanaopambana na ugonjwa hatari wa Ebola, mashariki mwa nchi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇