LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 8, 2020

'DRONE', NDEGE HATARI ISIYOKUWA NA RUBANI


1. UTANGULIZI
KATIKA andiko hili ambalo mdau una nafasi huru kuchangia mawazo yako, tutaona jinsi ndege ya kijeshi isiyokuwa na rubani, yaani 'Drone,' inavyofanyakazi, hususan katika kubaini mlengwa na kumshambulia kwa makombora.
Pia, tutaona baadhi ya madhara makubwa ambayo yamekuwa yakisababishwa na mashambulizi ya ndege hizo pale zinaposhambulia kile kinachoitwa magaidi.
2. MAANA YA 'DRONE'
Jina drone ni la lugha ya Kiingereza likimaanisha nyuki-dume, ambao jukumu lao ni kuwapanda malkia wa nyuki kwa lengo la kupandikiza mbegu zao.
Kwa kutumia nguvu kubwa nyuki-dume hao hupandikiza hizo mbegu zao kwa malkia kwa mara moja tu, ambapo muda mfupi baadaye madume hao hufa.
Hiyo ikiwa na maana kwamba, nyuki hao dume hupoteza maisha baada ya kupenyeza mbegu zao kwa malkia wa nyuki.
Hivyo, kutokana na hali hiyo ya 'drone-nyuki,' ndio maana katika siku za nyuma 'drone-ndege' zilikuwa zikipoteza uwezo wa kwendelea kutumika baada ya kushambulia adui mara moja; sawa na 'drone-nyuki.'
3. AINA ZA DRONE-NDEGE
Drone ndege zipo za aina nyingi, zikiwemo kubwa za kubeba mizigo mizito ya kijeshi, za kuzima moto, za kutafiti mazingira ya hali ya hewa, nk.
Aidha, hapa tutaangalia drone ndogo ambazo ni za matumizi ya kijeshi, hususan katika kushambulia maadui wanaolengwa.
Uzito wa hizo Drone ndogo za kivita ni kilo takribani 700, sawa na uzito wa basi dogo la abiria, yaani Hiace, ambapo drone ikiwa na makombora uzito huwa huongezeka kuwa kilo takribani 1000.
Kadhalika, gharama ya kununua Drone moja ya kijeshi ni kati ya dola za Marekani milioni 4 (sh. bilioni 9.2), ambapo Drone kubwa huweza kugharamu hadi dola milioni 120 (sh. bilioni 276).
Drone hutumika pale ambapo mazingira hayaruhusu binadamu kutumika kumshambulia adui, ambapo mpaka wakati huu serikali ya Marekani ndiyo inaongoza katika kutumia ndege hizo kushambulia na kuua.
Mathalani, idhini ya kutumia drone kushambulia popote duniani hutolewa na Rais wa nchi hiyo, wakati huu ni Donald Trump, huku pia mitambo ya kuziongoza ndege hizo ikiwa ndani kabisa ya nchi hiyo ya Marekani.
4. KITUO KIKUU CHA DRONE
Mojawapo ya mambo ambayo yatakushangaza msomaji ni kuwa kituo kikuu cha kuongoza ndege hizo za drobe za Marekani kipo katika Jimbo la Nevada la nchini humo.
Kituo kingine maarufu kipo katika mji wa Kandahar, nchini Afghanistan.
Mitambo ya kuongoza ndege hizo ina uwezo wa kuona kila kona ya dunia, huku ndege hizo zikiwa zimesambazwa katika vituo mbalimbali vya kijeshi vya Marekani vilivyotapakaa katika nchi mbalimbali, ikiwemo Barani Afrika.
Mathalani, katika chumba kimojawapo utakuta kuna vijana watalaamu ambao hutumia kompyuta kufuatilia nyendo mbalimbali za walengwa wa mashambulizi kutoka kwa drone.
Kimsingi, kinachofanyika ni makachero wa Marekani katika maeneo mbalimbali husika kufuatilia kwa makini nyendo za walengwa, hadi kufahamu wapi walipo katika wakati muafaka.
Kachero au makachero husika hutumia simu maalumu kutoa taarifa katika kituo kilichopo jirani na kituo kikuu chenye drone, ambapo kituo hicho hutuma haraka taarifa kamili kwa magwiji wa kompyuta za kuongoza drone kule Nevada.
Magwiji hao kwa kutumia mitambo ya setelaiti zilizopo angani huweza kutafuta na kuona eneo tajwa husika, ikiwemo mlengwa au walengwa, jengo au gari lililombeba mlengwa au walengwa.
Mara moja mitambo ya drone hujazwa taarifa hizo, yaani 'data' husika na kuamriwa kuanza safari kwelekea kwenye eneo alipo mlengwa au walengwa.
Wastani wa kasi ya drone kwenda eneo husika ni kati ya kilomita 250 na 350 kwa saa, na hivyo kuwa na uweza wa kuwasili katika shabaha husika ndani ya muda mfupi.
Kadhalika, ndege hiyo ina uwezo wa kusafiri umbali mrefu wa kilomita 2500 kumfuata adui, huku pia ikiwa na uwezo wa kumshambulia ikiwa umbali wa kilomita 8 kutoka angani hadi ardhini.
Pia, Drone ina uwezo wa kukaa angani kwa muda mrefu hadi kwa saa takribani 12, ikiranda randa angani kumtafuta adui au kuchunguza nyendo za washukiwa wa uhalifu, hususan ugaidi.
Waongozaji kule Nevada au Kandahar huweza kuiona ndege hiyo na pia kuona shabaha inayolengwa, ambapo huwa rahisi kuelekeza drone kulishukia eneo husika na kufyatua kombora dhidi ya shabaha inayolengwa.
Aidha, kwa mjibu wa mtaalamu wa kuongoza drone nchini Marekani ambaye sasa ni mstaafu, hukariri na gazeti la Guardian la nchini Uingereza akisema kuwa lugha inayotumika kati ya wao waogozaji (waliopo Nevada) na warushaji wa drone (mfano waliopo Syria au Afghanistan au Irak, nk) ni lugha ya kificho.
Mathalani, kachero huyo hukaririwa akisema kwamba waongozaji wa Drone wakishaona shabaha inayowindwa huweza kuwaambia warushaji wa ndege hiyo kuwa "nyasi zimechipua tayari kuvunwa," ikimaanishwa kuwa anayewindwa ameonekana mahali alipo.
Mara moja warushaji wa drone huwaambia waongozaji kuwa "kama gugu limeota, tuwahi kulikata," ikimaanishwa kuwa ni wakati muafaka kutuma Drone kushambulia.
Mara moja warushaji wanaporusha ndege hiyo kwenda angani, waongozaji "hudaka" masafa yake kwa njia ya setelaiti na kuanza kuidhibiti drone husika hadi kwenye eneo la shabaha husika.
Drone hubaki kuranda randa katika eneo hilo hadi pale shabaha husika inapoonekana wazi, ambapo ndege hiyo huishukia na kufyatua kombora.
5. WATOTO NI KINGA DHIDI YA SHAMBULIO LA DRONE
Mara kadhaa baadhi ya washukiwa wa ugaidi wamewahi kuwatumia watoto wao kama kinga, wakitambua kuwa kanuni za kimataifa zinakataza kuuwa watoto vitani.
Hivyo, mshukiwa wa ugaidi anapoonekana akiandamana na mtoto shambulio la drone huahirishwa.
Hiyo ni kwa sababu ya kuepusha lawama kwa serikali yenye kutumia ndege hizo dhidi ya watuhumiwa wa ugaidi, au washukiwa wowote ambao hutakiwa kushambuliwa.
6. NCHI ZENYE DRONE
Mpaka sasa ni nchi chache tu zenye kutumia kwa wingi ndege hizo zisizokuwa na rubani, ikiwemo Marekani, Israel, China, Iran, Italia, India, Pakistan, Urusi, Uturuki, Poland, na Iran.
Baadhi ya nchi hizo huunda zenyewe ndege hizo, ambapo mwaka jana 2019, matumizi ya ndege hizo yaliongezeka mno.
Nchi ambazo mashambulizi ya ndege hizo ni mengi ni pamoja na Afghanistan, Pakistan, Syria, Irak, Somalia, and Yemen, ambapo pia idadi ya mashambulizi inazidi kuongezeka kila siku.
7. MADHARA YA DRONE
Kuanzia mwaka 2015 hadi 2019, idadi ya mashambulizi kutoka kwenye Drone za Marekani nchini Pakistan dhidi ya kile kinachodaiwa kuwa ni kuangamiza magaidi, yaliua watu 3,949.
Kwa mujibu wa taasisi za Marekani zinazopinga nchi hiyo kutumia ndege hizo kuua watu, jumla ya raia waliopoteza maisha nchini Pakistan ni 962.
Raia hao walipoteza maisha wakati ndege hizo zikishambulia wale waliodaiwa kuwa ni magaidi, au raia hao kudhaniwa kuwa magaidi dhidi ya maslahi ya Marekani.
Nchini Yemen ambapo kuna vita ya wenyewe kwa wenyewe, huku serikali ya Marekani ikiunga mkono upande mmoja, jumla ya mashambulizi kutoka ndege hizo yalikuwa 206, ambapo jumla ya watu waliouawa ni 1,1174, wakiwemo raia 158.
Aidha, nchini Somalia ambapo Marekani inawakabili wanamgambo wa Al-Shabaab dhidi ya serikali ya nchini humo, jumla ya mashambulizi yalikuwa 23, ambapo jumla ya vifo ilikuwa 116, wakiwemo raia 12.
8. MASHAMBULIZI YA DRONE DHIDI YA "MAGAIDI"
Katika kuhitimisha ngoja tuangalie baadhi ya wahanga wakuu wa mashambulizi hayo ya Drone, walivyopoteza maisha kutokana na kuvamiwa na ndege hizo za Drone:-
i). Anwar al-Awlak (40)
Huyu alikuwa mwalimu wa mafundisho ya kiimani katika eneo la Mashariki ya Kati na barani Asia.
Serikali ya Marekani ilimtuhumu kwa kuajiri wanamgambo wapya wa kikundi cha kigaidi cha Al-qaed nchini Yemen, ambapo drone zilianza kumsaka.
Baada ya kumtafuta kwa muda mrefu, huku mara kadhaa shambulizi dhidi yake likiahirishwa kwa vile alikuwa anamtumia mtoto wake (mwenye umri wa miaka 16 raia wa Marekani) kama kinga, siku moja alionekana akipata chakula katika mgahawa mmoja nchini Yemen.
Drone ilitumwa na kuwasili katika eneo hilo na pia kuonekana angani, mwalimu huyo na wenzake walikimbilia kwenye gari lao na kuanza kutoroka wakiwa ndani ya gari hilo katika barabara kuu.
Hilo likawa ni kosa la kiufundi, kwani drone iliwaona na kulifuata gani hilo na kulishambulia kwa kombora kutoka umbali wa kilomita 7 angani.
Watu wote ndani ya gari hilo walipoteza maisha, akiwemo mwalimu Anwar, na mwandishi wa habari aliyedaiwa kuwa mwajiriwa wa kikundi Al-qaed.
ii). Mohammed Emwazi a.k.a Muhammad Jassim Abdulkarim Olayan al-Dhafiri a.k.a Jihad John (27)
Huyu ni yule ambaye kupitia video kadhaa miaka 2014 na 2015 alikuwa akionekana akiwakata vichwa raia wa Marekani waishio Mashariki ya Kati kabla ya kifo chake.
Miongoni mwa matukio aliyohusika ni mauaji nchini Syria ya raia 6 wa Mataifa ya Magharibi na 2 wa nchini Japan, wakiwemo waandishi wa habari na watoa misaada kwa wahanga wa vita.
Akiwa mwarabu mwenye uraia wa nchini Uingereza, John alitokea kuwa muuaji maarufu Mashariki ya Kati, ambapo alikuwa na mtindo wa kuwakata vìchwa watu hao huku matukio hayo yakioneshwa kwenye video.
Aidha, kutokana na vitendo hivyo vya kikatili, vilisababisha "Jihad John" kusakwa kwa upana zaidi, huku drone 3 zikitumika katika operesheni ya kumtafuta.
Siku yake iliwadia wakati akiwa anatoka kwenye jengo moja nchini Syria ili aingie kwenye gari lake, ambapo hizo drone 3 zilimuona na kumshukia kwa makombora 3 kwa pamoja na kumsambaratisha sawia.
iii). Abu Hussain al-Britani (21),
Huyu alikuwa ni mzaliwa wa nchini Uingereza mwenye asili ya nchini Pakistan, akiwa ni mwana propaganda na mtaalamu wa kompyuta za kikundi cha Al-qaeda.
Siku ya kwanza kushambuliwa nchini Irak drone ilimkosa, lakini kombara kutoka ndege hiyo liliua raia 3 na kujeruhi 5, huku yeye akisalimika na kutoroka kutoka eneo hilo.
Siku 10 baadaye ilitumika mbinu tofauti ili kumpata, ambayo ni kuunganisha mawasiliano ya simu yake na masafa ya setelaiti yanayoongoza drone.
Alipopigiwa simu tu, drone ilinasa mawimbi ya sauti kutoka kwenye simu yake na kuyafuata hadi ilipomuona kwenye kituo cha petroli akijaza mafuta kwenye gari lake.
Kombora kutoka kwenye drone hiyo lilisababisha kifo chake, pamoja wa watu kadhaa, wakiwemo 3 waliodaiwa kuwa walinzi wake.
iv). Kamal Derwish (29),
Huyu alikuwa raia wa Marekani mwenye asili ya nchini Yemen, ambaye alituhumiwa kuhusika katika kutoa mafunzo kwa magaidi nyumbani kwake nchini Marekani, kabla ya kutorokea Yemen.
Ikijibu shutuma za Wamarekani kuwa drone ya nchi hiyo imeua raia wao nchini Yemen, serikali ya Marekani ilidai kuwa Derwish alikuwa tishio kwa maslahi ya taifa hilo katika eneo la Mashariki ya Kati.
Siku ya tukio la kuuawa, mwanaharakati huyo alikuwa anasafiri na wenzake 4 kwenye gari lao kuitikia wito wa kwenda kukutana na wanaharakati wenzake katika eneo mojawapo la jangwa la nchini Yemen.
Baada ya kufika katika eneo husika, dereva wa gari lao alipiga simu kwa wenzao kuwa tayari wamefika katika sehemu ya kukutania.
Bila kutambua kuwa huo ulikuwa ni mtego, badala yake drone ilinasa masafa ya simu hiyo na kuyafuata hadi kutokea walipokuwa watu hao.
Drone hiyo ilifyatua kombora ambalo lilisambaratisha gari hilo, na kuua watu wote 5, akiwemo Derwish na dereva wao.
Hakika, matukio ya aina hiyo ni mengi mno, ambapo kwa mujibu wa utafiti wa televisheni ya Fox News nchini Marekani, asilimia 63 ya wananchi wa nchi hiyo wanapinga matumizi ya Drone, asilimia 32 wanakubali, na asilimia 5 hawana majibu.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages