LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 7, 2020

DK. NCHIMBI ATEMA CHECHE CHECHE

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Dkt. Rehema Nchimbi, akiwahutubia watumishi wa Umma wa mkoa wa Singida leo.

*Aanza 2020 kwa kumwagia sifa lukuki Mhe. Rais Magufuli
*Akataa Singida siyo masikini
*Asisitiza kazi, uadilifu
Na John Mapepele 
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi amesema leo kuwa  kila mtumishi  wa Serikali  katika mkoa wake kuanzia mwaka huu 2020 atatakiwa kuonyesha mafanikio yanayotokana na  mishahara wanayolipwa na Serikali kupitia kauli mbiu maalum  iliyoandaliwa na mkoa ya mshahara wangu upo wapi ifikapo mwisho wa mwaka  huu huku akiwaonya kuachana na mambo ya siasa na badala yake kufanya kazi kwa bidii ili kuunga mkono juhudi za  Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa  Rais John Pombe Magufuli.

Akizungumza na watumishi wa Umma  wa mkoa wa Singida katika mkutano maalum wa kwanza katika mwaka  huu 2020 mjini Singida leo, Dk. Nchimbi alisema mkoa umeamua kuiishi kauli mbiu hii baada ya kuona mafanikio ya kupigiwa mfano yaliyopatikana kutoka kwa wanufaika wa mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)  ulilenga  katika kunusuru kaya masikini na baada ya muda wa mradi  waweze  kusimama wenyewe uliozinduliwa Septemba, 2014  mkoani hapo na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa.

Alisema katika  mpango huo ruzuku ya shilingi elfu ishirini(20,000/=) ilitolewa kwenye kila Kaya yenye sifa katika Halmashauri 6 kati ya 7 za mkoa pamoja na fedha za masharti ya afya na elimu ambayo  kila kaya yenye mtoto anayesoma Shule ya Msingi  na Sekondari na wale  chini ya miaka 5 walipewa  kuanzia shilingi elfu mbili(2000) hadi elfu sita (6000), ambapo alisema ruzuku hiyo imekuwa  msaada mkubwa kwa kaya masikini katika kuwanunulia  sare, madaftari pamoja na kulipia matibabu hasa  kujiunga Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii(NHIF).

Aliongeza kuwa hadi kufikia mwezi Januari 2020, jumla  ya kaya 38,136 kutoka katika vijiji 278 zinanufaika na ruzuku hii na jumla ya shilingi  takribani bilioni thelathini na saba na milioni mia tisa (37,900,000,000) ziliwafikia walengwa.

Napenda kuwahakikishia kuwa  hakuna kipindi ambacho watumishi wa umma watakuwa na  maisha bora kama hiki kwa kuwa Serikali ya awamu ya Tano imeshaboresha kwenye kila sekta kama miundombinu,huduma za afya, elimu itashindwaje kuboresha maisha ya watumishi umma alihoji Dk. Nchimbi huku akisisitiza kuwa watumishi wazembe hawatavuka mwaka 2020 wataondolewa mara moja kupisha watumishi wanaoendana na kauli mbiu ya hapa kazi  tu.

Aidha Dk. Nchimbi alisema pamoja na kuhakikisha kuwa mishashara ya watumishi inaleta tija kwenye familia na kuboresha uchumi, tayari mkoa unatekeleza  mikakati mahususi ya  kilimo cha kisasa  cha pamoja cha zao la korosho kwa wananchi  wa Mkoa wa Singida  ambapo ametoa rai kwa watumishi na wananchi kujitokeza ili kupatiwa maeneo hayo ili kuyaendeleza kwa pamoja.

Hadi sasa Singida siyo, masikini, kame wala yenye njaa kama iliyokuwa ikitafsiriwa na baadhi ya watu hapo awali. Tayari hekta elfu kumi na mbili (12000)  za kilimo cha pamoja (block farming) zimepandwa mikorosho na zimeanza kuzaa korosho katika Wilaya ya Manyoni. Ninatoa shukrani na  pongezi zangu za dhati kwa Rais John Pombe Magufuli kwa kutupatia pikipiki 10 ili ziweze kusaidia katika kazi hii alisisitiza Dk.Nchimbi.

Alisema kutokana na tafiti zilizofanyika hivi karibuni zimeonyesha kuwa ardhi ya mkoa wa Singida ina ubora mkubwa wa kusitawisha zao la Korosho kwa muda mfupi ukilinganisha na maeneo mengi hapa nchini hivyo hakuna sababu ya watumishi na  wananchi kutochangamkia fursa hiyo adimu ambapo pia alionya kuwa wananchi ambao watabainika kuwa hawapo makini wataondolewa katika program hiyo.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages