LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 18, 2020

AWATAKA WAPINZANI KUKUBARI KUSHINDWA

 Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally amevitaka vyama vya upinzani nchini kujiandaa mapema kukubali kushindwa kama ambavyo CCM ilikubali kushindwa katika baadhi ya majimbo mwaka 2015.

Ameeleza kuwa CCM ikishindwa huwa inakubali kushindwa kama ambavyo walikubali mwaka 2015 katika majimbo mbalimbali nchini ikiwemo jimbo la Kigoma Mjini, hivyo amevitaka vyama vya upinzania navyo viige mfano huo wa CCM na waanze mapema kujiandaa kukubali kushindwa.


Katibu Mkuu ameyasema hayo, jana tarehe 17 Januari, 2020 alipokuwa akizungumza katika mkutano wa ndani na wajumbe wa mikutano mikuu ya kata, kamati ya siasa ya wilaya ya Uvinza, Waasisi, wazee maarufu, wenyeviti wa mashina, mabaraza ya Jumuiya ngazi ya matawi na kata, wenyeviti wa vijiji na serikali zao, Kata ya Kazuramimba wilayani Uvinza Mkoa wa Kigoma.

“wanaCCM tukishindwa hukubali kuwa tumeshindwa, tuliposhindwa Kigoma Mjini Ubunge na Halmashauri tulikubali na wao wajifunze pia kwamba unaposhinda, unayemshinda akubali na kuwa muungwana kuwa umemshinda, na akirudi awamu nyingine akakung’oa na wewe ukubali”.

Amesisitiza kuwa, “Nimekuja kutoa ujumbe Kigoma nzima, ikiwemo Kigoma Mjini kuwa, tumejipanga kushinda, wajiandae kukubali kushindwa, hivyo nimekuja kufunga mitambo ya ushindi wa maendeleo na kwa hali ya Kigoma ni lazima nifunge mitambo ya kimkakati, ndio maana nilianza Unguja, Pemba, nikaenda Tanga na kisayansi ilinitaka ndani ya masaa 48, niwe nimefunga Kigoma na nimefanya, kwa kuwa jana nilikamilisha Tanga, leo nimeifunga rasmi hapa”.

Aidha, katibu Mkuu pamoja na mambo mengine, amesisitiza uimarishaji wa Serikali za Mitaa ambapo amegusia baadhi ya sifa za wanachama wa CCM watakaowania nafasi za Udiwani ni lazima wawe ni watu ambao tutaamini wanaweza kuongeza tija katika maendeleo ya watu, wenye uelewa juu ya maisha ya watu, kwa kuwa serikali za mitaa ni kiungo muhimu kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

“Diwani wa CCM ni lazima awe na uelewa wa maisha ya watu na hii haihitaji shahada, inahitaji uelewa na ushirikiano na wananchi wenzake, wanamjua vizuri, anawajua vizuri anayajua mazingira vizuri, yupo tayari, je atatumika au anakwenda kutumikiwa? Ni lazima tuwe na uhakika atatufikisha mbali , hata Mbunge naye ni Diwani hivyo ni lazima awe na sifa za kiungo, na atatumika vizuri kwenye Baraza kuunganisha halmashauri na masuala ya kitaifa”.

Mkutano huo wa ndani umehudhuriwa na wanachama wa CCM na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma Ndg. Amandus Nzamba, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa Ndg. Kirumbe Ngenda, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga, Mbunge wa Jimbo la Uvinza Bi. Hasna Mwilima, Mbunge wa Viti Maalum Bi. Zainabu Katimba na Mkuu wa wilaya ya Uvinza Ndg. Mwanamvua Mlindoko.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages