Na; Mwandishi Wetu
Serikali imedhamiria kuandaa Mpango wa Taifa wa kuimarisha masuala ya utoaji huduma kwa Watu wenye Ulemavu ili kuwezesha kundi hilo maalumu kushiriki kwenye sekta mbalimbali hapa nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa alipokuwa akifungua mkutano wa wadau kuhusu masuala ya utoaji huduma kwa Watu wenye Ulemavu uliofanyika Disemba 11, 2019, Jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa Mkutano huo Naibu Waziri Ikupa alieleza kuwa lengo la Serikali kuandaa mpango huo ni mkakati mmoja wapo wa kuwezesha Watu wenye Ulemavu wanapata huduma bora ikiwemo elimu bora, afya, fursa ya kufanya maamuzi mbalimbali pamoja na kuwezeshwa kiuchumi.
“Utekelezaji wa Mpango huu utakuwa wa miaka mitano na Rasimu ya mpango huo imeshandaliwa na utakapo kamilika utasaidia kwa kiasi upatikanaji wa huduma bora na endelevu kwa Watu Wenye Ulemavu sambamba na kuimarika kwa utekelezaji wa Sera, Sheria, Miongozo pamoja na Mifumo mbalimbali ya Usimamizi wa kundi hilo maalum,” alisema Ikupa
Aliongeza kuwa mpango huo unalenga pia kuimarisha uwezo wa kitaasisi katika kushughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu, kuboresha utoaji huduma, kuimarisha shughuli za kiuchumi na ajira, upatikanaji wa taarifa na takwimu muhimu za watu wenye ulemavu, na pia ushiriki na ushirikishwaji wa watu wenye Ulemavu.
“Ninaamini maoni mbalimbali ya wadau yakayotolewa katika mkutano huu yatasaidia kwa kiasi kikubwa uimarishwaji wa mpango huo wa taifa wa utoaji huduma kwa watu wenye ulemavu,” alisema Ikupa
Sambamba na hayo, alielezea pia mkutano huo utatoa fursa kwa wadau kutoa maoni yao juu ya mwongozo wa usimamizi, uratibu na uendeshaji wa Mfuko wa Taifa wa Watu wenye Ulemavu ulioanzishwa kwa Sheria Na.9 ya mwaka 2010.
“Uwepo wa Mfuko huo utawezesha Watu wenye Ulemavu kukuwa kiuchumi na utawajengea uwezo wa kujiamini na kuanzisha miradi na shughuli mbalimbali zitakazowakwamua kiuchumi,” alieleza Ikupa
Aidha, Naibu Waziri Ikupa alitoa wito kwa wadau wa maendeleo kujitokeza kwa wingi na kuchangia mfuko huo ili kufanikisha lengo la kuimarisha maisha na huduma za watu wenye ulemavu, na pia alihimiza vyombo vya habari kutangaza mfuko huo.
Kwa upande Wake, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Ushauri kwa Watu Wenye Ulemavu, Dkt. Lucas Kija alieleza kuwa Watu wenye Ulemavu wamekuwa wakikabiliana na changamoto ambapo imepelekea wamekuwa wakikosa haki zao na huduma stahiki.
“Mpango huu wa Serikali utatoa mwongozo wa kuhudumia masuala ya watu wenye ulemavu katika sekta ya elimu, afya, ajira, uwezeshaji kiuchumi, miundombinu ili kuleta ustawi wa kundi hilo maalumu, hivyo mpango huo utaifanya jamii kuthamini Watu wenye Ulemavu,” alisema Lubago
Naye Afisa Programu kutoka Shirika la Foundation for Civil Society, Bi. Eveline Mchau alisema kuwa Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ili kufanikisha masuala mbalimbali ya Watu wenye Ulemavu hapa nchini.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇