Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
WAZIRI wa Usafirishaji wa nchi ya Finland, Sanna Marin ameapishwa leo na kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo akiwa na umri wa miaka 34 tu. Hii inamfanya kuwa Waziri mkuu kijana zaidi kwa sasa ulimwenguni. Jumapili wiki iliyopita alishinda kura za wabunge wa chama cha Social Democrat baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu Antti Rinne kujiuzulu Jumanne wiki iliyopita baada ya tuhuma kwamba alishindwa kudhibiti mgomo ulioanzishwa na wafanyakazi wa Posta na Muungano wa chama cha Kati (Centre Party) kudai hauna imani naye tena.
Waziri Mkuu mchaguliwa, Sanna Marin ameeleza kuwa na kazi kubwa ya kujenga imani. Alipohojiwa na shirika la habari la Reuters alisema;
“Sikupata kufikiria katika umri huu au jinsia yangu, ninafikiria tu juu ya sababu zilizonipelekea kuwa kwenye siasa na mambo yaliyowajengea imani wapiga kura kwangu” ameeleza.
Marin alianza kupanda katika uongozi mara baada ya kuongoza Mamlaka ya Mji wa Viwanda wa Tampere, akiwa na umri wa miaka 27 tu.
Chama cha Social Democrats ni kikubwa zaidi kwenye muungano unaoongoza serikali ya Finland. Marin alipata umaarufu mkubwa baada ya kumshinda kiongozi mkuu wa Muungano huo Bungeni Antti Lindtman.
Marin sio kiongozi pekee mkubwa ulimwenguni mwenye umri kati ya miaka 30, wengine ni Kiongozi wa Ukraine, Oleksiy Honcharuk( Miaka 35) na Waziri Mkuu wa Nchi ya New Zealand, Jacinda Ardern mwenye miaka 39.
Vyama vikuu katika Bunge la Finland vinaongozwa na wanawake, wanne kati yao ni kati ya miaka 30. Li Andersson (32) anaongoza Left Alliance; Maria Ohisalo (34) anayekiongoza chama cha Umoja wa Kijani, Chama cha Kati (Centre Party) kinaongozwa na Katri Kulmuni(32); na Bi. Anna-Maja Henriksson ambaye ana miaka 55, akiongoza Chama cha Swedish People's Party of Finland.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇