LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 27, 2019

RAIS DK. MAGUFULI AONGEZA SIKU USAJILI WA 'LINE' ZA SIMU

IKULU, CHATO
Rais Dk. John Magufuli amefanya usajili wa laini yake ya simu kwa kutumia alama za vidole na kutangaza nyongeza ya muda wa siku 20 kwa watakaoshindwa kufanya usajili huo ifikapo Disemba 31, 2019.

Rais Magufuli amefanya usajili huo leo Ijumaa, Disemba 27, 2019,  katika eneo la mji mdogo wa Chato Mkoani Geita.

Ametangaza nyongeza ya siku za usajili huo wa laini za simu ili kutoa fursa kwa wale watakaokumbwa na sababu mbalimbali zikiwemo kuugua na kukamilisha upataji wa namba ama Vitambulisho vya Taifa.

Rais Magufuli amesisitiza kuwa baada ya muda huo hakuna kisingizio chochote kitakachokubalika na ameagiza TCRA kuhakikisha laini ambazo hazijasajiliwa zinazimwa.

Amesema, usajili wa laini za simu kwa alama za vidole ni muhimu kwa usalama wa nchi ikiwemo kuepusha vitendo vya utapeli na ujambazi vinavyofanywa na wahalifu, ambao licha ya wengi wao kukamatwa na vyombo vya dola wameendelea kusababisha usumbufu na upotevu mali za wananchi hususani fedha.

Pamoja na kuwasalimu wananchi wa Chato Mjini waliojitokeza kushuhudia wakati akisajili laini yake kwa alama za vidole, Rais Magufuli amesikiliza maoni yao kuhusu zoezi hilo.

Baadaye mwananchi mmoja Steven Joseph Wandwi anayefanya biashara ya kuuza chipsi na mishikaki aliwaongoza wenzake kumuombea Rais Magufuli na kumshukuru kwa utumishi wake mzuri ulioongeza kasi ya maendeleo kwa Taifa hasa vijana ambao sasa wanachapa kazi bila bughudha. 

Kabla ya kwenda kusajili laini yake ya simu, Rais Magufuli ametembelea Mtaa wa Chato Kati na ametoa pole kwa familia ya Marehemu Atanasi Masansa Mnaku aliyefariki dunia juzi tarehe 25 Desemba, 2019 na mazishi yake yamepangwa kufanyika kesho.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages