Korea Kaskazini imekosoa sababu iliyotolewa na Marekani ya kutaka kuitishwa kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili jaribio la kombora la hivi karibuni lililofanywa na serikali ya Pyongyang.
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Korea Kaskazini amekitaja kikao kama hicho kwa mashinikizo ya Marekani kwamba ni cha kijinga na kwamba, Pyongyang haitasalimu amri mbele ya mashinikizo ya Washington.
Takwa la Marekani la kufanyika kikao cha Baraza la Usalama liliowasilisha Alkhamisi iliyopita ya tarehe 12 Disemba na Kelly Craft balozi na mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa. Hiyo inahesabiwa kuwa, hatua ya karibuni kabisa inayoashiria kushadidi mizozo na mivutano baina ya Washington na Pyongyang.
Hivi sasa serikali ya Marekani inakabiliwa na mashinikizo ya Korea Kaskazini na washirika wake kutokana na kutotekeleza ahadi zake mkabala na Pyongyang.
Sambamba na kukaribia uchaguzi wa Marekani, kwa upande mmoja Washington haina nia ya kupunguza vikwazo vyake dhidi ya Korea Kaskazini na hivyo kuchukua hatua mshabaha mkabala na Pyongyang; na katika upande wa pili haioni kama hatua za Korea Kaskazini za kurejea katika njia ya huko nyuma ni kwa maslahi ya Marekani.
Ni kwa kuzingatia uhakika huo, ndio maana katika hatua yake ya hivi karibuni kabisa iliyo dhidi ya Korea Kaskazini, serikali ya Rais Donald Trump imetaka kuitishwa kikao cha Baraza la Usalama ili kwa njia hiyo labda iweze kuikinaisha Pyongyang iendelee kufanya mazungumzo kwa kufuata matakwa ya Washington.
Hii ni katika hali ambayo, Korea Kaskazini imedhihirisha kuwa, nchi hiyo kinyume na ilivyokuwa huko nyuma takriban miaka miwili ya mazungumzo na Marekani, inafikiria kuyafanyia majaribio machaguo mengine.
Kimsingi inawezekana kusema kuwa, radiamali ya Korea Kaskazini inaonyesha kwamba, kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hakiwezi kuifanya Pyongyang ifuate mkondo inaotaka Marekani.
Katika anga na mazingira kama haya, Ijumaa ya juzi Waziri wa Ulinzi wa Marekani alihutubia katika Chuo cha Mahusiano ya Kigeni nchini Marekani na kutahadharisha kuhusiana na matokeo mabaya ya nchi mbi hizo kujiweka mbali na mazungumzo.
Mark Esper alisema: Kutokea vita katika Peninsula ya Korea litakuwa jambo la kuogofya. Hakuna mtu anayetaka kushuhudia hilo. Mimi nadhani kwamba, muda si mrefu tutakuwa majaribuni.
Korea Kaskazini ambayo imeipatia Marekani muda wa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu itazame upya misimamo yake ya huko nyuma, hivi sasa imevuta macho na masikio ya walimwengu na kuwafanya waielekee. Hii kwamba, katika muda huu uliobakia, Korea Kaskazini ikiwa na nia ya kutoa indhari kwa Marekani itafanya majaribio ya nyuklia au makombora ya kuvuka mabara au la, ni jambo ambalo bado halijajulikana.
Lakini kile ambacho kiko wazi na bayana ni kwamba, baada ya kupita miezi 20 tangu kuanza mazungumzo baina ya Washington na Pyongyang, imeeleweka kwa wote kwamba, Korea Kaskazini imechukua hatua na utendaji wa kuzingatia ukweli wa mambo na haiwezi kubadilisha njia yake kupitia vitisho au mashinikizo.
Kiujumla inaonekana kuwa, kinyume na matarajio ya Marekani, takwa la Washington kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siyo tu kwamba, halitaifanya Korea Kaskazini irejee katika meza ya mazungumzo, bali yamkini ikaifanya Pyongyang iwe na azma zaidi ya kukabiliana na hatua za chuki na hasama za Marekani.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇