LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 14, 2019

NCHI ZA MAGHARIBI ZINATUMIA VIBAYA SUALA LA HAKI ZA BINADAMU KWA KIZINGIZIO CHA KUTETEA WATU

Akizungumza Alkhamisi katika bunge la Ujerumani, Heiko Maas alidai kwamba mamia ya watu waliuawa katika ghasia hizo na kwamba ukandamizaji uliotumika katika matukio hayo unapaswa kulaaniwa. Awali pia Jeseph Borell, Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya aliingilia wazi wazi masuala ya ndani ya Iran kwa kutumia kisiasa vurugu hizo za karibuni nchini na kutoa madai yasiyo na msingi dhidi ya Iran.
Misimamo hiyo ya kisiasa imechukuliwa na viongozi wa Ulaya kwa kisingizio cha kuwaunga mkono watu wa Iran katika hali ambayo nchi hizo zenyewe zinashirikiana kwa karibu na Marekani katika kutekeleza siasa za ugaidi wa kiuchumi dhidi ya taifa la Iran na hivyo kukiuka moja kwa moja misingi ya haki za binadamu. Misimamo ya kisiasa na ya undumakuwili ya nchi za Ulaya ina historia ndefu na ya hivi karibuni zaidi ya Mapinduzi ya Kiislamu inathibitisha wazi kwamba Ujerumani katika kipindi cha vita vya kulazimishwa vya Saddam dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ilishirikiana kwa karibu na dikteta huyo wa zamani wa Iraq kwa kumpa silaha za sumu na kemikali ambazo alizitumia kuwaua kinyama watu wa Iran na hata wa nchi yake mwenyewe.
Heiko Maas, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani
Ushirikiano huo bado haujasahauliwa na watu wa Iran wala Iraq. Nukta ya kutiliwa maanani hapa ni kwamba ushirikiano wa Uherumani na Marekani katika kutekeleza ugaidi wa kiuchumi dhidi ya Iran umepelekea kuzuiwa kuingizwa nchini bidhaa za msingi, yakiwemo madawa kwa ajili ya kutibiwa magonjwa sugu ya waathriwa wa silaha za kemikali zilizouzwa na Ujerumani kwa Saddam katika kipindi cha vita vya kulazimishwa vya miaka minane dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Mbali na hayo, wimbi la kutumwa katika eneo la Asia Magharibi silaha za kisasa zenye uharibifu mkubwa kutoka nchi za Ulaya ikiwemo Ujerumani, silaha ambazo hazina natija nyingine ghairi ya kusababisha jinai za vita, uharibifu na kuuawa kinyama watu wasio na hatia na hasa watoto na wanawake wa nchi kama vile Yemen, ni mfano mwingine wa wazi wa madai ya uongo yanayotolewa na nchi za Magharibi kuwa eti zinatetea haki za binadamu.
Kwa kutilia maanani mifano hiyo ya wazi ya ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na nchi za Magharibi, viongozi wa nchi hizo, akiwemo waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani wanapaswa kushauriwa waheshimu haki halisi za binadamu kwa msingi wa kutopendelea upande wowote na kuzingatia ukweli wa mambo badala ya kuchukua misimamo ya kindumakuwili na ya kisiasa dhidi ya nchi nyingine huru zinazojitawala.
Nchi za Magharibi zinakiuka wazi wazi haki za binadamu za watu wa Yemen
Kwa kutilia maanani vurugu na malalamiko ya hivi karibuni kufuatia kuongezwa bei ya mafuta ya petroli, serikali ya Iran ilisikia vizuri sauti ya malalamiko halisi ya wananchi na kuitenganisha na ya wazua vurugu na waharibifu wasio na nia njema na Mapinduzi ya Kiislamu.
Kuhusiana na suala hilo, Abbas Musawi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alisema siku ya Alkhamisi kwamba katika ghasia za hivi karibuni, Iran imembua wazi kuwa safu ya maadui na wauaji wa watu wasio na hatia pamoja na waungaji mkono wao wa kigeni ni tofauti kabisa na ya wananchi walio na malalamiko halali na ya msingi, na kwamba baada ya kufanyika uchunguzi, hatua za lazima na zinazofaa zitachukuliwa kwa madhumuni ya kuheshimu haki za watu wa Iran.
Misimamo ya nchi za Marekani na za Ulaya kuhusiana na machafuko ya karibuni yaliyotokana na nyongeza ya bei ya mafuta nchini Iran inathibitisha wazi kwamba nchi hizo zinataka kutumia vibaya machafuko hayo kwa shabaha ya kufikia malengo yao ya kisiasa na wala hazina nia yoyote ya kutetea watu wa Iran bali madai ya kutetea haki zao za binadamu ni sawa na machozi ya mamba.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages