Mahakama Kuu ya Zimbabwe leo amemteua binti wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Robert Mugabe kufuatilia mali zilizoachwa na kiiongozi huyo ili ziweze kugawanywa baina ya warithi wake.
Terrence Hussein aliyekuwa wakili wa Robert Mugabe amesema kuwa, mke wa rais huyo wa zamani wa Zimbabwe, Grace na watoto wake wameridhia dada yao, Bona Chikore afuatilie na kusimamia mali za Mugabe.
Jumanne iliyopita wakili Terrence Hussein alikuwa amewaambia waandishi habari kwamba mchakato wa kutambua mali za Mugabe utachukua muda, suala lililozusha shaka juu ya ripoti ya vyombo vya habari vilivyosema kwamba, kiongozi huyo wa zamani ameacha fedha taslimu dola milioni 10 na milki kadhaa katika mji mkuu wa Zimbabwe, Harare.
Wazimabwe wana hamu kubwa ya kujua kiwango cha utajiri wa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo aliyeitawala nchi kwa kipindi cha miaka 37. Baadhi ya Wazimbabwe wanadai kuwa Mugabe na familia yake wamejilimbikizia utajiri unaokadiriwa kufikia dola bilioni moja kwa mujibu wa madai yaliyofichuliwa na wanadipmosia wa Marekani mwaka 2001.
Hata hivyo wakili wake Hussein amekanusha madai kwamba Mugabe alikuwa akimiliki majumba ya kifahari nje ya nchi akisema yameenezwa na waandishi wa habari wa Marekani na Uingereza waliokuwa wakimuandama kiongozi huyo.
Gazeti la serikali la Zimbabwe liliripoti hivi karibuni la kwamba Robert Mugabe ambaye aliaga dunia mwezi Septemba mwaka huu ameacha kiasi cha dola milioni kumi lakini hajaacha tamko lolote kuhusu warithi wa mali hizo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇