LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 12, 2019

FITINA KUBWA YA MAANDAMANO DHIDI YA SERIKALI KATIKA 'SIKU YA USHINDI' WA IRAQ

Itakumbukwa kuwa Haider al-Abadi, Waziri Mkuu wa wakati huo wa Iraq aliitangaza tarehe 10 Disemba 2017 kuwa ni mwisho wa Daesh na ushindi dhidi ya kundi hilo la kigaidi nchini humo. Siku hiyo inatambuliwa katika kalenda ya Iraq kwa jina la 'Siku ya Ushindi' na huwa siku ya likizo rasmi. Kwa kuzingatia umuhimu wa siku hiyo, Jumanne ya jana kulitolewa wito wa kufanyika maandamano katika maeneo tofauti hususan mjini Baghdad. Hata hivyo inaonekana kuwa wito huo wa maandamano haukutolewa kwa nia njema ya kutetea matakwa ya wananchi. Ushahidi unaonyesha kwamba hivi sasa Iraq inakabiliwa na fitina kubwa. Kwanza kabisa inatupasa kuashiria hatua ya kuchaguwa tarehe 10 Disemba kuwa siku ya maandamano hayo. Tarehe 10 Disemba ni miongoni mwa siku adhimu za ushindi wa taifa la Iraq dhidi ya kundi la kigaidi na la Daesh (ISIS), na kwa upande mwingine siku hiyo ni likizo rasmi nchini humo. Kuhusiana na suala hilo Ahmad Mulla Talal, mmoja wa wafanyakazi wa televisheni ya al Sharqiyah yenye nafasi kubwa katika kupotosha maandamano ya amani ya wananchi wa Iraq aliandika jana kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba Disemba 10 ni siku ya 'makabiliano ya wananchi na Najaf dhidi ya kundi la wabeba silaha la Hashdu sh-Sha'abi' nchini Iraq.' 
Hatua hiyo ni kutokana na mchango mkubwa wa Hashdush-Sha'abi na nafasi yake athirifu katika mapambano ya kulisambaratisha genge la Daesh, na hata katika miezi ya hivi karibuni imekuwa ikihujumiwa na vyombo vya habari na propaganda kali za wapinzani wake.

Tarehe 10 Disemba 2017 ilikuwa siku ya kuangamizwa rasmi genge la kigaidi la Daesh nchini Iraq

Suala la pili ni hili kwamba, baadhi ya wapinzani wametangaza wazi kwamba, maandamano ya jana yalikuwa fitina zinazoungwa mkono na makundi yanayochochea ghasia na machafuko nchini humo. Ni kwa sababu hiyo ndio maana watu wengi hawakushiriki katika maandamano hayo ya jana. Pamoja na hayo wachochezi hao wametumia mitandao ya kijamii kueneza propaganda za kuwachochea wananchi ili kushiriki kwenye maandamano hayo. Kwa maneno mengine ni kwamba, ndani ya jamii ya Iraq si tu kwamba hakukuwa na kauli moja juu ya suala la kushiriki wananchi kwenye maandamano hayo, bali akthari ya Wairaki waliyatilia shaka pia maandamano yenyewe. Sambamba na mito ya kufanyika maandamano hayo, wanaharakati wawili wanaojishughulisha na uratibu wa maandamano hayo walishambuliwa na kuuawa katika mji wa Karbala.
Fitina ya tatu inahusiana na radiamali ya baadhi ya shakhsia wa Iraq. Hii ni kusema kuwa, aaghlabu ya mirengo na shakhsia wa kisiasa nchini Iraq wametangaza kuwa wanaunga mkono maandamano ya amani ya wananchi.

Qais Khazali, Katibu Mkuu wa Harakati ya Asa'ib Ahl al-Haq ya Iraq

Pamoja na hayo Qais Khazali, Katibu Mkuu wa Harakati ya Asa'ib Ahl al-Haq ya Iraq alitahadharisha kuhusiana na maandamano ya jana na kutangaza kwamba, kungeshuhudiwa uharibifu mkubwa na mauaji ya watu wengi. Indhari hiyo ilionyesha weledi mkubwa wa viongozi wa kisiasa wa nchi hiyo kuhusiana na njama na fitina mpya za maadui wa Iraq.
Nukta ya nne ni kwamba maandamano ya Jumanne ya jana yalifanyika siku moja baada ya Taasisi ya Uwazi ya Iraq kutangaza kuwa, katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita kulitolewa kibali cha kutiwa mbaroni viongozi 226 wa zamani na wa sasa wa serikali ya nchi hiyo kwa tuhuma za ufisadi, wakiwemo mawaziri wawili wa sasa, mawaziri saba wa zamani, wabunge 10 na magavana 11 wa sasa na wa zamani. Waranti hiyo inaonyesha kwamba, vyombo vya sheria vya Iraq vimeanza mchakato wa kupambana na ufisadi na ili kufanikisha suala hilo kunahitajika hali ya usalama na utulivu wa kisiasa na kijamii nchini. Hata hivyo miito ya kufanyika maandamano kama haya yenye harufu ya fitina na hila, inazuia kufuatiliwa matakwa ya wananchi.
Nukta ya tano ni kwamba, uingiliaji wa nchi za kigeni katika masuala ya ndani ya Iraq, bado unaendelea. Katika uwanja huo, Jumapili iliyopita Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo iliwaita mabalozi wa nchi za Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Canada na kuwakabidhi malalamiko ya serikali ya Baghdad kuhusiana na sera zao za kuingilia masuala ya ndani ya taifa hilo. Hii ni baada ya nchi hizo kuitaka serikali ya Baghdad iyaunge mkono maandamano ya wananchi, katika hali ambayo nchi hiyo inasumbuliwa na  ghasia na machafuko yanayofanyika kwa makusudi na mpangilio maalumu.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages