Chama cha Jumuiya ya Maulama wa Kiislamu (Jamiat Ulema-e-Islam) nchini Pakistan ambacho kinaipinga serikali ya sasa ya Imran Khan, Waziri Mkuu wa nchi hiyo, kimetangaza mpango wa pili katika kumuwekea mashinikizo zaidi waziri mkuu huyo ili ajiuzulu.
Fazal-ur-Rehman, Mkuu wa chama hicho amewambia waandishi wa habari kwamba mpango wa pili kwa ajili ya kuendeleza wimbi la maandamano dhidi ya serikali unahusu kuweka vizuizi na kufunga barabara kuu, mitaa pamoja na medani kuu za nchi hiyo kwa ajili ya kuishinikiza serikali ya sasa ya Islamabad. Fazal-ur-Rehman aliitisha kikao na waandishi wa habari akiwa pamoja na viongozi wandamizi wa chama cha Jumuiya ya Maulama wa Kiislamu (Jamiat Ulema-e-Islam) nchini Pakistan.
Wakati huo huo serikali ya Pakistan pia na katika juhudi zake za kukabiliana na wapinzani, imetangaza mpango wake mpya wa hatua kwa hatua ambao ni pamoja na kuweka zaidi ya askari polisi elfu 15 waliopewa mafunzo katika maeneo nyeti ya mji mkuu na miji mingine ya nchi hiyo. Yapata wiki mbili sasa tangu wafuasi wa Fazal-ur-Rehman walipoanzisha maandamano mjini Islamabad wakimtaka Imran Khan, Waziri Mkuu wa Pakistan ajiuzulu. Hata hivyo baadhi ya weledi wa masuala ya kisiasa wamenukuliwa wakisema kuwa vyama vingine vya upinzani nchini humo vimekataa kukiunga mkono chama cha Jumuiya ya Maulama wa Kiislamu (Jamiat Ulema-e-Islam) na kwa muktadha huo, chama hicho hakiwezi kufikia lengo lake hilo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇